Prime
Huu hapa ujumbe wa Msigwa kwa watawala
Muktasari:
- Msigwa ambaye alikuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema kwa miaka 10, alijiunga na CCM Juni 30, 2024 kabla ya kutangaza kurejea Chadema Mei 23, 2026 huku akitoa sababu kuu kwamba mauaji ya Oktoba 29, 2025 yalisukuma dhamira yake.
Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema njia pekee ya kuliponya Taifa na kulitoa katika hali ya sasa ni watawala kukubali makosa yao na kurejea kwenye misingi ya mazungumzo ya kweli na maridhiano.
Pia, amesema ili maridhiano yawe na maana, taasisi muhimu kama Bunge, Mahakama na Polisi ziachwe zifanye kazi zao kwa uhuru bila kuingiliwa na kwamba matatizo ya kisiasa yatatuliwe kisiasa na ya kiuchumi yatatuliwe kiuchumi.
Mchungaji Msigwa amebainisha hayo Juni 2, 2026 wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, jijini Dar es Salaam, akizungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa zikiwa zimepita wiki mbili tangu alipotangaza kurejea Chadema akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Msigwa ambaye alikuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema kwa miaka 10, alijiunga na CCM Juni 30, 2024 kabla ya kutangaza kurejea Chadema Mei 23, 2026 huku akitoa sababu kuu kwamba mauaji ya Oktoba 29, 2025 yalisukuma dhamira yake.
Katika ripoti ya tume ya matukio ya kabla na baada ya uchaguzi mkuu 2025 iliyongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande, ilionyesha watu 518 waliouawa, kujeruhiwa na waliopoteza mali za umma na za watu binafsi.
Kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2026.
Akizungumza katika mahojiano hayo, Mchungaji Msigwa amesema kukubali makosa na kuomba msamaha si jambo la aibu wala udhaifu, hivyo amewataka watawala kukubali kufanya makosa kwenye mauaji ya watu wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
“Watawala wakubali wamekosea na waombe msamaha. Turudi kwenye misingi ya Taifa lenye utu, upendo na kuthaminiana. Haya ndiyo mafundisho ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,” amesema.
Amesema kurejea kwenye misingi hiyo kunahitaji taasisi na vyombo vya dola kufanya kazi kwa uhuru bila kumilikiwa au kuathiriwa na mtu yeyote huku kila mwananchi akiwa chini ya utawala wa sheria.
“Kumekuwa na dalili za watu ambao hawapo katika mifumo rasmi kutoa maagizo. Kesi zinaamuliwa kabla ya kufikishwa mahakamani. Wapo majaji na askari polisi wazuri, lakini mfumo mzima hauakisi matakwa ya Watanzania. Kwanza watawala wakubali tumepotea, kisha turudi kwenye maridhiano,” amedai.
Mchungaji Msigwa amesema watawala wanapaswa kuomba radhi kwa Watanzania pale wanapokosea, akisisitiza kufanya hivyo si udhaifu. Ameongeza kumekuwa na matamko ya kiburi na maneno yasiyo na hekima kutoka kwa baadhi ya viongozi.
“Utashi wa uongozi umepungua katika kipindi hiki kigumu. Mauaji ya Oktoba 29 yamegusa kila upande; familia za polisi, wanachama wa Chadema, wanachama wa CCM na wananchi wengine. Watu wamepoteza maisha, jambo ambalo si dogo,” amesema.
Amesema historia inaonyesha kuwa mataifa mengi yanapopitia nyakati kama hizo, watawala huamini kuwa vitisho na ukandamizaji vitadhoofisha upinzani, lakini matokeo yake huwa ni kuimarika zaidi kwa upinzani.
“Soma historia. Angalia wangapi wametekwa na wangapi wamefariki katika mazingira ya kutatanisha. Jamii imefikia hatua ya kuona kifo si jambo la kushangaza tena. CCM na Serikali yake zinapaswa kujitathmini na kuona kuwa kuna mahali hali si salama,” amesema.
Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa amesema baadhi ya watu wanaamini tawala zilizopita hazikuwa na maono, lakini hawajifunzi kutokana na historia.
“Wanadhani viongozi kama Muammar Gaddafi hawakuwa na uwezo. Wale wanaojivunia majengo na nguvu walizonazo wanapaswa kujua kuwa hasira za umma zinaweza kubadilisha kila kitu kwa muda mfupi. Suluhisho ni kukaa mezani na kufanya mazungumzo; hakuna aliye mgeni katika Taifa hili,” amesema.
Kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2026.
Amesema ukandamizaji wa sauti za wananchi, vyama vya siasa na vyombo vya habari hauondoi tatizo bali hulikuza.
“Mgandamizo haupotei, hujikusanya na baadaye hulipuka kwa madhara makubwa. Ni maombi yangu kwa walioko madarakani wasidhani viongozi wa kiimla waliowahi kuongoza duniani walikuwa wajinga. Historia inaonyesha hata walipokuwa na mali na nguvu waliishi kwa hofu na mashaka,” amesema.
Kwa mujibu wa Mchungaji Msigwa, dunia haivumilii uhalifu wa aina yoyote kwa muda mrefu, akitolea mfano wahusika wa uhalifu wa kivita waliowahi kuwajibishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Anaamini katika maridhiano
Mchungaji Msigwa amesema anaunga mkono mchakato huo lakini anataka uwe wa kweli na si wa kisanii kama ambavyo ilifanyika huko nyuma.
“Napenda maridhiano, lakini si maridhiano ya ujanja ujanja kama yaliyopita. Yawe ya kweli kama ilivyokuwa Afrika Kusini ambapo watu waliomba msamaha na kukiri makosa yao,” amesema.
Amesema changamoto iliyopo Tanzania ni kwamba baadhi ya watu wanazungumzia maridhiano huku wakiwa bado na nia ya kisiasa inayokinzana na dhana hiyo.
“Maridhiano yanahitaji uwanja wa siasa kuwa sawa kwa wote. Kwa sasa uwanja huo hauko sawa kwa sababu CCM inanufaika zaidi. Pia, hatuna Katiba inayodhibiti ipasavyo madaraka ya Rais,” amesema.
Msigwa amekosoa pia utendaji wa baadhi ya taasisi za dola, akidai Bunge ni dhaifu na baadhi ya vyombo vya sheria na usalama havitekelezi majukumu yao kwa uhuru.
“Ili maridhiano yawe na maana, vyombo vya dola lazima viwe huru. Polisi wafanye kazi yao kwa haki, Mahakama na Bunge vitekeleze wajibu wao bila shinikizo,” amesema.
Amesema vyama vya siasa vinapaswa kushindana kwa sera na hoja badala ya kutumia mifumo ya dola kupata ushindi.
“CCM watoke na watu wao, nasi vyama vya upinzani tutoke na watu wetu. Tushindane kwa kuwashawishi wananchi. Njia zilizotumika zamani haziwezi kuisaidia nchi,” amesema.
Kuhusu nafasi ya Chadema katika maridhiano, Mchungaji Msigwa amesema chama hicho hakiwezi kuachwa nje kutokana na kile alichodai kuwa ni mateso na changamoto ambazo wanachama wake wamepitia.
“Maridhiano hayawezi kuwa na maana bila Chadema kushiriki. Kuna wanachama waliopigwa, kutekwa, kufungwa na kunyimwa haki zao za kisiasa,” amesema.
Kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akifanyiwa mahojiano na waandishi waandamizi wa Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2026.
Amesisitiza madai ya Chadema katika maridhiano hayapaswi kutafsiriwa kama masharti magumu bali kama sehemu ya kueleza changamoto walizopitia na kuzitafutia suluhisho la kudumu.
“Huwezi kuwapiga watu halafu ukawafundisha namna ya kulia. Kuna watu wameuawa, wamefungwa na wengine kujeruhiwa. Haya ni masuala yanayopaswa kujadiliwa kwa uwazi,” amesema.
Uzoefu aliojifunza
Mchungaji Msigwa amesema uzoefu wake wa kisiasa umemfundisha mwanasiasa hapaswi kupinga au kutetea kila jambo kwa sababu tu ya misimamo ya chama chake.
“Mtu akiwa upinzani huamini kupinga kila kitu, na akiwa CCM huamini kutetea kila kitu. Mimi nimejifunza kuangalia masuala ya msingi kwa maslahi ya Taifa, ingawa bado nipo Chadema,” amesema.
Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana nchini, ikiwamo kuongezeka kwa madarasa, vituo vya afya na kupungua kwa vifo vya mama na mtoto, lakini akasisitiza maendeleo hayo hayawezi kuhalalisha ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Nimejifunza mengi ndani ya CCM, lakini maendeleo hayawezi kuwa sababu ya kuhalalisha mauaji au ukiukwaji wa haki. Hayo ni mambo mawili tofauti ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa uzito wake,” amesema.
Wito kwa Watanzania
Mchungaji Msigwa ametoa wito kwa Watanzania kurejea katika misingi ya utawala bora ambapo kila taasisi itekeleze wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
“Vyombo vya ulinzi vifanye kazi ya ulinzi, wanasheria walinde sheria, wanahabari wahabarishe umma. Dola haipaswi kuziba midomo ya watu au kuogopa kukosolewa. Mbinu hizo hazijawahi kuleta matokeo chanya,” amesema.
Amesema hata waliowahi kushindwa katika nyakati tofauti hawakuwa wajinga, bali mara nyingi mifumo ya nchi ilishindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Wito wangu ni kurejea kwenye misingi. Tuelewe majukumu ya Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Polisi, Bunge na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Tukifanya hivyo, tutaendelea kuishi kwa amani na utulivu,” amesema.
Itaendelea kesho.