Prime
Jinsi ya vyama kuishi bila mikutano ya hadhara
Muktasari:
- Baada ya Serikali kuzuia kwa muda mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, wachambuzi na wadau wa masuala ya siasa wamevitaka vyama kutumia mbinu mbadala ili vibaki hai.
Dar es Salaam. Siku 12 tangu Serikali isimamishe mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, wataalamu wameonya kusubiri zuio liondolewe kunaweza kuvipunguzia vyama ushawishi, hivyo vikijite katika matumizi ya teknolojia na mbinu nyingine mbadala.
Wadau hao wanasema zuio hilo si mwisho wa siasa, kwa kuwa historia ya siasa duniani inaonyesha vyama vilivyobadili mbinu badala ya kusubiri mazingira kubadilika, vilidumu na kujenga ushawishi kwa wananchi.
Kauli hizo zinakuja baada ya Serikali Juni 26, mwaka huu, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, ikieleza hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa nchi.
“Namwelekeza IGP Wambura (Mkuu wa Jeshi kla Polisi) asitoe vibali kwa kazi zozote zitakazokuwa zinahusiana na mikutano ya hadhara kwa kipindi hiki kwa chama chochote,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, bungeni jijini Dodoma.
Zuio hilo, lilipokewa kwa hisia tofauti, kwani baadhi ya vyama vya siasa na asasi za kirai vimekuwa vikilipinga, kwamba linakwenda kinyume na matakwa ya Katiba.
Tayari kuna tishio la baadhi ya wadau hao kwenda mahakamani kupinga amri hiyo, kwa kuwa Waziri wa mambo ya Ndani hana mamlaka hayo kikatiba wala kisheria.
Hata hivyo, Katambi ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amenukuliwa akisema hajavunja Katiba wala sheria za nchi bali anaangalia usalama wa nchi.
Kwa vyovyote vile, amri hiyo wadau wanasema inaweza kuviathiri vyama vya siasa na ili kuondokana na hilo, havina budi kuimarisha shughuli zake kwa kuwekeza katika mawasiliano ya kidijitali kupitia mitandao ya kijamii, mikutano ya mtandaoni na maudhui mbalimbali ya kidijitali yanayowafikia wananchi moja kwa moja.
Wadau hao vilevile, wanasema vinaweza kuimarisha mifumo yao ya ndani kwa kuzijengea uwezo ngazi za matawi, kutoa mafunzo kwa viongozi na wanachama, kufanya mikutano ya ndani inayoruhusiwa na kutumia tafiti za maoni kubaini mahitaji ya wananchi, ili kuepuka hali iliyoshuhudiwa miaka takribani 10 iliyopita wakati kulipowekwa zuio la mikutano ya kisiasa wakati wa utawala wa awamu ya tano wa Hayati John Magufuli.
Mitandao ya kijamii
Katika eneo hili, Mchambuzi wa Siasa, Thomas Kibwana amesema katika mazingira ya sasa, mitandao ya kijamii ndiyo jukwaa lenye uwezo mkubwa wa kuhakikisha vyama vinaendelea kuonekana mbele ya wananchi.
“Tumeshuhudia hali kama hii. Panapotokea ugumu wa mikutano ya hadhara, vyama huhamia kwenye majukwaa ya kidijitali na kuendelea kuwasiliana na wananchi na wafuasi wao,” amesema.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya wanaotumia intaneti imefikia milioni 58.9 mwaka 2025; idadi ya simu janja imefikia milioni 29.8 (sawa na asilimia 42.5% ya watumiaji wote).
Kibwana anasema uwekezaji katika maudhui bora ya kidijitali unaweza kusaidia vyama kuwasilisha sera, kujibu hoja na kuendeleza mijadala bila kukusanya umati.
Hata hivyo, amesema anaamini zuio hilo ni la muda kwa kuwa Serikali imeeleza sababu zake ni za kiusalama.
Hoja kama hiyo imetolewa pia na Mtaalamu wa Mawasiliano kwa Umma, Loth Makuza, aliyesema zuio linahusu mikutano ya hadhara, lakini halizuii mawasiliano kupitia majukwaa ya kidijitali.
“Mitandao ya kijamii inaweza kuwakutanisha viongozi na wanachama bila kuwa eneo moja. Hapo ndipo vyama vinapaswa kuelekeza nguvu zake,” amesema.
Amesema vyama vinavyowekeza katika majukwaa yao ya kidijitali vitaendelea kujenga umaarufu na kuvutia wafuasi wapya hata katika mazingira yenye vikwazo.
Kuwafikia wananchi
Kwa upande wake Mchambuzi wa Siasa, Dk Faraja Kiwelu amesema mikutano ya hadhara si mbinu pekee ya kujenga nguvu katika chama.
Amesema viongozi wanapaswa kuhamishia nguvu katika mikutano ya ndani, kampeni za nyumba kwa nyumba na mawasiliano ya karibu na wanachama.
Amesema pia, mitandao ya kijamii itumike kuwasilisha sera, kujibu hoja za wananchi na kuonyesha shughuli za chama bila kutegemea mikusanyiko.
“Vyama viwekeze pia katika tafiti za maoni. Hiyo itasaidia kuelewa mahitaji ya wananchi na kuandaa ujumbe unaowagusa,” amesema.
Kosa la kuepuka
Katikati ya maoni hayo, Mchambuzi wa siasa, Dk Elias Mwakibete amesema kosa kubwa ambalo vyama vinaweza kufanya ni kusubiri zuio liondolewe ndipo virejee kwa wananchi.
“Siasa ni shughuli endelevu. Ukikaa kimya kwa muda mrefu, wananchi wataanza kukusahau,” amesema.
Amesema vyama viimarishe matawi yake na kushiriki shughuli za maendeleo, mazingira, elimu na afya ili viendelee kuonekana.
Pia, amesema mawasiliano kupitia redio, magazeti, televisheni na majukwaa ya kidijitali yataendelea kukifanya chama kisikike hata bila mikutano ya hadhara.
Imani kwa wananchi
Jambo jingine muhimu linaelezwa na Neema Sanga, mtaalamu wa mawasiliano kuwa umaarufu wa chama cha siasa haupimwi kwa ukubwa wa mikutano bali kiwango cha imani ya wananchi.
Amesema vyama vinapaswa kuwa na programu maalumu zinazowafikia vijana, wanawake na makundi mengine kupitia semina na mijadala ya vikundi vidogo.
“Teknolojia imebadili siasa duniani. Video fupi, mikutano ya mtandaoni na matangazo ya moja kwa moja vinaweza kuwafikia maelfu ya watu kwa wakati mmoja,” amesema.
Ameonya kuwa ukimya wa muda mrefu unaweza kufanya chama kipoteze umaarufu na ushawishi wake kwa umma.
Taasisi badala ya viongozi
Kwa upande mwingine, Mtaalamu wa Usimamizi wa Chapa, Daudi Mwang’ingo amesema vyama vinapaswa kujenga taasisi imara badala ya kutegemea umaarufu wa viongozi wachache.
Amesema mafunzo kwa makada, viongozi wa matawi na wanachama yataifanya ajenda ya chama kuendelea kusambaa hata bila mikutano mikubwa.
“Ziara ndogo, tafiti na mikutano ya kikatiba inayoruhusiwa vinaweza kusaidia kusikiliza wananchi na kuwa karibu nao,” amesema.
Pia, amesema ushirikiano na makundi ya kijamii, kitaaluma na kiuchumi unaweza kuongeza ushawishi bila kutegemea majukwaa makubwa.
Haya si mapya
Mwaka 1960, baada ya maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Serikali ya wakati huo chini ya utawala wa kibaguzi ilizuia mikutano ya Chama cha African National Congress (ANC).
Kutokana na mazingira hayo, ANC kilihamisha nguvu zake katika mitandao ya wanaharakati wa kijamii, vyama vya wafanyakazi, taasisi za dini na kampeni za kimataifa, mbinu iliyosaidia chama hicho kuishi kisiasa na mioyoni mwa wananchi hadi kilipoingia madarakani mwaka 1994.
Nchini Poland nako, Chama cha Solidarity kilipigwa marufuku kuendeleza siasa zake chini ya sheria ya kijeshi mwaka 1981.
Badala ya kutegemea mikutano ya hadhara, viongozi wake walifanya mikutano ya ndani iliyohusisha watu wachache katika maeneo mbalimbali.
Njia hizo zilikipa nguvu chama hicho na mwaka 1989 kilishinda uchaguzi na kubadilisha historia ya nchi hiyo.
Ushauri huo unatolewa wakati ambapo baadhi ya vyama, kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM), vimejikita katika mikutano ya ndani badala ya hadhara.
Tangu zuio hilo, wajumbe mbalimbali wa Kamati Kuu ambao ni walezi wa chama hicho katika mikoa wameanza kufanya vikao na wanachama katika maeneo yao, kuendeleza siasa zisizo za hadharani.
Mathalan, Julai 4 mwaka huu, Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye pia ni Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi alishiriki kikao na makada wa CCM Mkoa wa Dodoma, ambao yeye ni mlezi wake.
Aidha, tangu Julai 2 mwaka huu, Katibu wa Halmashauri Kuu, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Rabia Hamid, alianza ziara mkoani Manyara na baadaye Kilimanjaro, akishiriki vikao vya Kamati za Siasa za mikoa hiyo.
Rabia ni mlezi wa CCM katika mikoa hiyo na katika ziara hiyo amekuwa akishiriki vikao vya ndani kuendeleza siasa za chama hicho, licha ya Serikali kuzuia mikutano ya hadhara.