Kagoma wa Chadema atimkia CCM, aomba ridhaa kuwania udiwani Kiboriloni

Frank Kagoma (Kushoto) akikabidhiwa kadi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho, Wilaya ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, Faraji Swai.
Muktasari:
- Kagoma ambaye alikuwa diwani pekee wa Chadema katika baraza la madiwani lililopita, amejiunga na CCM leo Julai 2,2025 na kukabidhiwa kadi ya CCM na Mwenyekiti wa chama hicho, Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai.
Moshi. Aliyekuwa diwani wa Kiboriloni, kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Frank Kagoma amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kagoma ambaye alikuwa diwani pekee wa Chadema katika baraza la madiwani lililopita, amejiunga na CCM leo Julai 2, 2025 na kukabidhiwa kadi ya CCM na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai.
Baada ya kukabidhiwa kadi, Kagoma amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea udiwani katika kata hiyo.
Akizungumza baada ya kujiunga na CCM, Kagoma amesema lengo lake ni kuendelea na safari ya kuwatumikia wananchi.
"Gari nililokuwa nimepanda limepata shida pale Wami, nalazimika kushuka kupanda gari lingine ili niendelee na safari. Sasa naomba nije CCM ili nimsaidie Rais kufanya kazi yake,” amesema Kagoma.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai amesema Kagoma amefanya uamuzi sahihi kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano akiwa diwani amekuwa akitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Frida Kaaya amesema chama hicho kipo tayari kumpa mwanachama huyo ushirikiano kwa namna yoyote kwa lengo la kuleta maendeleo kama dira ya chama hicho inavyoelekeza.