Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kenya kutumia Sh40.6 bilioni kulipa fidia waathirika wa maandamano

Muktasari:

  • Ni maandamano ya uchaguzi mkuu na kupinga muswada wa fedha. Waliouawa na waliopotezwa kulipwa fidia. Waathirika zaidi ya 1,000 kunufaika na fidia.



Nairobi. Serikali ya Kenya inayoongozwa na Rais William Ruto imetenga Ksh2 bilioni, sawa na Sh40.6 bilioni za Tanzania, kwa ajili ya kuwalipa fidia waathirika wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, vikiwamo vya ukatili wa polisi.

Ukiukwaji huo ulitokana na maandamano ya mwaka 2017 na 2022 yaliyohusishwa na migogoro iliyotokana na uchaguzi mkuu, maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha wa mwaka 2024 na maandamano ya Sabasaba ya mwaka 2025.

Waathirika zaidi ya 1,000 wanatarajiwa kuanza kupokea fidia hizo wiki ijayo, na hiyo inafuatia utambuzi na uhakiki wa waathirika katika kile Rais Ruto alichosema ni mwanzo wa kufunga sura chungu katika historia ya nchi hiyo.

Fidia hiyo itatolewa kwa kuzingatia vigezo vikuu sita, ambavyo ni ukiukwaji wa haki ya kuishi, ukatili wa kingono, uhuru dhidi ya mateso, haki ya uhuru na usalama, uharibifu wa mali na wale waliopotezwa kwa nguvu.

Chini ya mpango huo, familia ambazo wapendwa wao waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi au kuuawa katika maandamano nchini humo zitalipwa fidia ya chini ya Sh50.8 milioni za Tanzania, pamoja na gharama za matibabu.

Mbali na kulipa fidia hiyo, Serikali pia itabeba gharama zote za matibabu zilizotumika kabla ya kifo cha mwathirika, huku familia za waliopotezwa kwa nguvu zikilipwa fidia ya Sh30.4 milioni.

Kulingana na mapendekezo ya mpango huo, wale waliopata majeraha makubwa ya mwili watalipwa fidia ya Sh20.3 milioni, huku waathirika wa mateso yaliyofanywa na vyombo vya dola wakipendekezwa kulipwa fidia ya Sh40.6 milioni.

Fidia ya majeraha ya wastani ya kimwili inapendekezwa kuwa angalau Sh10.1 milioni, huku waathirika wa madhara madogo ya kimwili na waliokamatwa au kuzuiliwa kiholela wakilipwa fidia ya Sh1 milioni.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya la leo, Jumanne, Juni 16, 2026, mpango huo pia unapendekeza kulipwa fidia ya Sh2 milioni kwa kila mfanyabiashara ambaye biashara yake iliathiriwa na matukio hayo ya maandamano na vurugu.


Alichokisema Rais Ruto

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo jana, Jumatatu, Juni 15, 2026, jijini Nairobi, Rais Ruto alisema malipo hayo ni utekelezaji wa ahadi iliyotokana na imani ya Wakenya kwamba nchi yao haiwezi kuendelea kupitia njia ile ile yenye maumivu.

“Kwa muda mrefu sana, wakati Wakenya wametumia haki hizi za kikatiba za kuandamana, mara nyingi matokeo yamekuwa vurugu, majeraha, kupoteza maisha, uharibifu wa mali, uchungu na migawanyiko.

 “Vijana wamebeba makovu ya kimwili na kihisia. Maofisa wa polisi wamejeruhiwa. Jamii zimeachwa zikiwa na kiwewe,” alisema.

Akisisitiza kuwa kumekuwa na matukio ambapo mwitikio wa maandamano ya umma umesababisha matumizi ya nguvu kupita kiasi, ukiukwaji wa haki na kupoteza maisha, Rais Ruto alisema kila hali kama hiyo inapotokea, Kenya hupata hasara, demokrasia hudhoofika na mchezo wa lawama huanza.

Machi 2026, Rais Ruto aliiagiza Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) kuandaa mpango na kuwasilisha mfumo wa fidia kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu ndani ya siku 60.

Hatua hiyo ilifuatia shinikizo la umma kuhusu vifo, majeraha na ukiukwaji wa haki uliohusishwa na maandamano ya hivi karibuni, lakini wigo wa mfumo huo wa fidia ulioandaliwa na KNCHR umehusisha pia matukio mengine zaidi ya maandamano.

Katika ripoti yake, KNCHR ilirekodi madai 1,815 na kupokea mengine 1,022 kutoka kwa Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) nchini Kenya, huku madai mengine yakipokelewa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya.

Mwenyekiti wa KNCHR, Claris Ogangah, alisema ripoti hiyo imebeba ushahidi wa mashuhuda, wakiwamo wanawake na watoto wasio na sauti, ambao walijeruhiwa, walipata ulemavu au walipoteza wapendwa wao walipokuwa wakitumia haki yao ya kuandamana.

“Tume inakiri kwamba si kesi zote zinazoripotiwa zinastahili kutambuliwa kama ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaostahili fidia, kwani baadhi ni vitendo vya uhalifu vilivyotengwa, vikiwamo vilivyofanywa na askari polisi na raia wengine, ambavyo vinapaswa kupitia mchakato wa haki ya jinai,” alisema Ogangah.

Kwa upande wake, Profesa Makau Mutua, ambaye ni mwenyekiti wa timu ya wataalamu wa fidia kwa waathirika, alisema: “Jopo sasa linakabidhi majina haya kwa ajili ya uthibitisho na litaanza kutoa fidia baada ya wiki moja kuanzia sasa.”

Aliongeza: “Ripoti hii ni kukiri kwamba mateso yenu yameonekana na kwamba Serikali inakubali jukumu lake la kuyarekebisha,” akieleza kuwa hiyo ni hatua muhimu ya upatanisho kutokana na madhila waliyoyapitia waathirika.

Kulingana na ripoti ya KNCHR, watakaolipwa fidia wapo katika makundi sita ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ambayo ni pamoja na haki ya kuishi (waathirika 245), unyanyasaji wa kijinsia (waathirika 75), uhuru dhidi ya mateso (waathirika 135), uhuru na usalama wa watu (waathirika 473), haki ya kumiliki mali (waathirika 138) na kutoweka au kupotezwa kwa nguvu (waathirika 35).