Kinana: Demokrasia imekua, tatizo lipo kwenye utekelezaji wa sheria

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amesema demokrasia nchini imekua lakini kuna upungufu katika sheria za uchaguzi na jinsi ya kuzisimamia.


Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amesema demokrasia nchini imekua lakini kuna upungufu katika sheria za uchaguzi na jinsi ya kuzisimamia.

Kinana ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 22, 2023 katika mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

“Ukiniuliza kwa maoni yangu naona demokrasia imekua, kwa vipimo mbalimbali ukiacha kipindi fulani cha nyuma miaka michache iliyopita, mimi nadhani demokrasia imekua. Ukitazama kwa mfano kwenye vyombo vya uwakilishi serikali za mitaa na Bunge idadi ya vyama vilivyowakilishwa bungeni na idadi ya wabunge waliotoka vyama vingine nje ya CCM imekuwa ikiongezeka na kufika hata asilimia 40 ya wabunge."

"Na kama uchaguzi wetu ungeendelea hivyo mwaka 2020 nadhani idadi ingeongezeka zaidi na huenda 2025 ingeongezeka zaidi tena. Kwa hiyo ukiniuliza nitasema ni kweli demkorasia imekuwa. Je kuna mapungufu? Nakiri upo maana kila jambo jema lina upungufu," amesema Kinana.

Kuhusu upungufu huo amesema upo katika sheria na jinsi ya kuzisimamia wakati wa uchaguzi.

“Uhuru wa kuzungumza upo lakini kila uhuru una mipaka yake, Baba wa Taifa (Julius Nyerere) alifundisha kwamba uhuru bila nidhamu ni uwendawazimu na nidhamu bila uhuru ni utumwa kwa hiyo lazima kila uhuru uwe na mipaka yake."

“Lakini kwa ujumla uhuru upo wa kutosha wakati mwingine kuna kasoro katika utekelezaji wake. Nadhani Watanzania wanapiga kelele katika kusimamia sheria zinapowapa Watanzania uhuru wa kusema," amesema Kinana.