Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiza alivyomkwepa Mbowe akatua kwa Zitto-2

Muktasari:

  • Kiza alianza kupenda siasa akiwa darasa la pili, alipojenga imani ya siku moja angemfuta machozi baba yake aliyegombea ubunge mara mbili na kushindwa.



Dodoma. Katika simulizi ya safari ndefu ya kisiasa iliyosheheni matumaini, changamoto na uthubutu wa muda mrefu, mbunge wa Kigoma Kaskazini (ACT- Wazalendo), Kiza Mayeye, ameeleza kwa undani namna ndoto aliyoiweka moyoni kwa zaidi ya miaka 30 ilivyotimia kupitia msimamo, ujasiri na safari yenye misukosuko ya kisiasa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi simulizi iliyoanza jana, Kiza anasema safari yake ya sasa si tukio la bahati tu, bali ni muendelezo wa historia ya familia yao iliyoanzia kwa baba yake, aliyewahi kugombea ubunge wa jimbo hilo katika chaguzi za ndani za Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1990 na 1995 bila mafanikio, akiishia katika kura za maoni.

Anasema tofauti kati yake na baba yake haiko tu kwenye kizazi, bali pia katika mazingira ya kisiasa na vyama walivyopitia. Yeye alilazimika kupita katika njia mbalimbali za kisiasa kabla ya kufikia mafanikio ya sasa.

Kiza anasema mapenzi yake kwa siasa yalianza akiwa bado mtoto wa darasa la pili, akishuhudia baba yake akipambana kisiasa bila mafanikio. Hapo ndipo alipojenga ndoto ya siku moja kuja kubadilisha historia hiyo.

Anasema anakumbuka akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino, Mwanza, alijiunga rasmi na Chama cha Wananchi (CUF), licha ya baba yake kuwa mwanachama na kiongozi ndani ya CCM.

“Nikiwa chuoni ndipo nilipojiunga rasmi na CUF, ingawa familia yangu, hasa baba yangu, alikuwa ndani ya CCM,” anasimulia mbunge huyo.

Anasema uamuzi wake ulijengwa na mambo mawili makuu; kwanza, alihisi CCM haikuwa na mazingira rafiki kwa matarajio yake ya kisiasa, na pili aliona CUF ilikuwa na mvuto kwa vijana na watu wa rika lake wakati huo.

Hivyo, anasema akiwa chuoni, alitumia hata fedha ya mkopo wa elimu kujihusisha na shughuli za chama, hali iliyomfanya ajulikane haraka ndani ya CUF na kufahamika hadi ngazi ya taifa.

Kiza anasema licha ya changamoto za kuwa kijana ndani ya siasa, aliendelea kujijenga kisiasa huku akipata nafasi ya kukutana na viongozi wa chama na kujifunza misingi ya uongozi.


Mgogoro wa CUF na mlango wa ubunge

Hatua kubwa ya kisiasa kwa Kiza, anasema, ilikuja mwaka 2017 wakati CUF ilipokumbwa na mgogoro kati ya katibu mkuu wake wa kipindi hicho, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu), na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba.

Anasema mgogoro huo uliigawa CUF katika makundi mawili, naye alikuwa upande wa Profesa Lipumba, akajikuta akiteuliwa kuwa mbunge wa Viti Maalum baada ya baadhi ya nafasi kubadilika ndani ya chama hicho.

“Niliambiwa nimepata uteuzi wa ubunge wa Viti Maalumu bila kutarajia. Ilikuwa furaha kubwa, ingawa ndoto yangu kubwa ilikuwa kugombea jimbo,” anasema Kiza.

Anasema uteuzi huo ulimjenga zaidi kisiasa na baadaye akateuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Wanawake wa CUF Tanzania Bara, ingawa ndani ya chama kulikuwa na misuguano na mpasuko mkubwa wa kimakundi.


Mivutano ya ndani ya chama

Kiza anasema wakati wa mgogoro huo, mawasiliano kati ya makundi yalikuwa magumu kiasi kwamba wabunge walikuwa hawasalimiani na kila upande ulimtazama mwingine kwa tahadhari kubwa.

“Wakati mwingine tulikuwa hatuzungumzi kabisa. Wabunge wa majimbo walituona kama tuko upande tofauti kabisa,” anasema.


Jaribio la kwanza la ubunge wa jimbo

Katika uchaguzi wa 2020, Kiza anasema alijitosa kwa mara ya kwanza kuwania jimbo la Kigoma Kaskazini, lakini hakufanikiwa.

Anasema matokeo hayo yalitokana na mambo mawili; kwanza, huenda muda wake wa mafanikio ulikuwa haujafika, na pili, kwa mtazamo wake, mchakato wa uchaguzi haukuwa wa haki na sawa.

Hata hivyo, baada ya changamoto hizo, Kiza anasimulia kipindi kingine muhimu anachosema kilibadilisha mwelekeo wa maisha yake ya kisiasa.

Anasema alikumbwa na ushawishi wa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mbunge huyo anasema aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alimtaka ahamie chama hicho, na hata maandalizi ya mapokezi yalikuwa yamekamilika Kigoma.

Lakini anasema kabla ya uamuzi huo kukamilika, alipokea simu kutoka kwa kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyemuomba wafanye mazungumzo ya haraka.

Anasema mazungumzo hayo yalimweka katika mtihani mkubwa wa kisiasa. “Zitto aliniuliza swali lililobadili mwelekeo wangu kwamba nataka kuhamia Chadema ili tuanze kushambuliana majukwaani?”

“Baada ya swali hilo, niliamua hapo hapo kubaki ACT – Wazalendo, nikasitisha mawasiliano na Chadema,” anasema Kiza.

Baada ya kujiunga na ACT - Wazalendo, Kiza anasema aliaminika na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Kigoma.


Mwelekeo wa ACT - Wazalendo

Alipoulizwa anaikadiriaje ACT - Wazalendo, Kiza anasema kina mustakabali mzuri na anaamini kinaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi katika siasa za Tanzania iwapo uchaguzi utafanyika kwa haki na uwazi.

Kiza, ambaye sasa anaongoza jimbo lenye vijiji 46 na vitongoji 280, anasema maendeleo ya jimbo la Kigoma Kaskazini yanaendelea na anawaomba wananchi kuendelea kumuamini.

Anasisitiza kuwa kila ahadi aliyotoa inalenga kutekelezwa ndani ya kipindi chake cha uongozi, akisema dhamira yake ni kuhakikisha maendeleo yanamfikia kila mwananchi jimboni humo.

Mtazamo kuhusu demokrasia

Akizungumzia demokrasia nchini, Kiza anapinga dhana kwamba vyama vya upinzani vipo ili kuonesha kuwa nchi ina demokrasia.

Anasema dhana hiyo ni potofu kwa sababu vyama vya siasa vya upinzani vinapambana kwa nguvu zote, na katika baadhi ya maeneo vinastahili kushinda uchaguzi, lakini matokeo yanakwenda upande mwingine.