KONA YA MALOTO: Sauti kutoka kaburini kwa Mzee Ali Kibao inavyosikika
Kata ya Mzingani, Tanga, nyumbani kwa Ali Mohammed Kibao, ni eneo la tukio. Watu wanazomea, makofi yanapigwa na mayowe ya kushangilia. Ajabu, mkusanyiko ni wa msiba. Shughuli ni mazishi.
Ali ndiye kichwa cha habari cha msiba. Amefariki dunia. Mazingira ya kifo yanaogofya kupita kiasi. Mauaji yake ni ya kikatili.
Kisa nini watu wazomee msibani? Nini sababu ya makofi kwenye shughuli ya mazishi?
Maswali yote mawili jibu lake ni moja; hisia! Kifo cha Ali kinaumiza, kinashangaza, kinatatanisha. Mazingira yake ndiyo kiini cha utata.
Binadamu yeyote hapaswi kutendewa unyama aliofanyiwa Ali. Mtu unapanda basi, usafiri wa umma. Watu wenye bunduki wanavamia gari.
Wanajitambulisha kuwa maofisa wa usalama. Wanamfunga pingu. Wanamshusha. Wanakwenda kumpiga hadi kumuua. Kama haitoshi, wanammwagia tindikali. Ndivyo Ali alivyouawa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, amefika msibani kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, anamwambia Masauni: “Usiende tena kwenye msiba wa mtu aliyetekwa.” Watu wanapiga makofi.
Lema akaendelea kwa kumwambia Masauni kuwa alipaswa kuwa ameshajiuzulu.
Hapo yakafuata makofi pamoja na mayowe. Ali ni Mwislamu. Mazishi yanaongozwa kwa mila na desturi za dini ya Kiislamu. Sheikh, anayeongoza ibada ya mazishi, anausia kutopiga makofi msibani.
Inafuata zamu ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika. Pamoja na kusimulia mema ya Ali, naye anamtaka Masauni kuwajibika.
Kwa mara nyingine, umati unalipuka kwa makofi na vifijo. Mnyika pia anataka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene, naye ajiuzulu. Makofi mengine yakapigwa, watu wakashangilia.
Maelekezo ya kutopiga makofi na kushangilia, hayakuzingatiwa. Ukawadia wakati wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Buriani. Alipata wakati mgumu kuzungumza, maana alikutana na zomeazomea. Batilda ni mkomavu kisiasa, vinginevyo wazomeaji wangeweza kumtoa kwenye mstari. Aliweza kubaki mstarini hadi alipomaliza hotuba yake.
Waziri Masauni alikuwa kwenye wakati mgumu zaidi. Kuna wakati alilazimika kukatisha hotuba yake, sababu wazomeaji walimzidi nguvu.
Baada ya zogo kuwa kubwa, ilibidi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, asimame kutuliza fujo zilizokuwepo. Akawataka watu kutulia na kumsikiliza Masauni. Angalau baada ya hapo, Masauni aliweza kuhutubia hadi mwisho.
Mbowe alipozungumza, makofi na sauti za ushangiliaji vilirejea. Jibu la kwa nini viongozi wa Serikali walizomewa na wa Chadema walishangiliwa, wala halina mzunguko.
Taswira ya mazishi ya Ali, ungedhani ni Wapalestina, jinsi ambavyo huzika ndugu zao wanaouawa na Wayahudi. Wapalestina hubeba miili ya ndugu, vijana na watoto wao ambao huuawa, kwa hisia na sauti kubwa kumwelekea Mungu ili kufikisha ujumbe kwa ulimwengu kwamba wanatendewa ukatili na wanauawa kinyama, hivyo hawana wa kumlilia zaidi ya aliye juu.
Ndivyo ilivyokuwa katika mazishi ya Ali. Alikuwa mwanachama wa Chadema. Mwanamikakati na kiungo muhimu kwenye sekretarieti ya Chadema. Nadharia kuu ya kutekwa na kuuawa kwa Ali baadhi wanasema ni uanachama na uhusika wake wa kimkakati ndani ya Chadema.
Hiyo ndiyo sababu viongozi wa Chadema wanarusha lawama moja kwa moja kwa dola, juu ya kifo chake.
Majuma yamekatika tangu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, wanyakuliwe, wapelekwe kusikojulikana. Kiongozi wa Chadema, wilaya ya Sumbawanga, Rukwa, Dioniz Kipanya, naye inadaiwa alitekwa, hajulikani alipo.
Siku Ali anatekwa, ilikuwa inatimia miaka saba tangu Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, aliposhambuliwa kwa risasi, ambazo zimemsababisha ulemavu wa maisha hadi leo. Tukio la Lissu limebaki kuwa moja ya matukio yaliyokosa majibu. Waliomshambulia hawajatambuliwa mpaka sasa.
Mwandishi wa habari Azory Gwanda, anakaribia kutimiza miaka saba tangu alipotekwa. Kada wa Chadema, Ben Saanane, Novemba 2024, atafunga mwaka wa nane, tangu alipotoweka. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye, Julai 2024, alikamilisha miaka saba, tangu aliponyakuliwa.
Afrika, eneo ambalo ni hatari kabisa kwa usalama wa raia ni Ghuba ya Guinea, ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa vifo, utekaji watu na hata ubakaji wa wanawake Afrika Magharibi. Kutoka Ghuba ya Guinea, hadi mataifa mengi ya Afrika yenye usalama mdogo wa raia, vyanzo vyake huwa viwili tu; vita vya kiraia na kufeli kwa Serikali.
Nigeria, Liberia, Guinea Bissau, Sierra Leon, Ivory Coast, Jamhuri ya Kongo (Brazzaville), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ni mifano ya mataifa yenye usalama mdogo wa raia, kwa mujibu wa ripoti za dunia. Sababu kubwa ni historia ya nchi hizo kupigana vita vya kiraia, kisha kushindwa kwa Serikali kutuliza hali ya nchi.
Tanzania haina historia ya kupigana vita ya kiraia, halafu kwa jicho la juu, nchi imekuwa ikipita salama nyakati za uchaguzi na mabadilishano ya madaraka. Swali linaloshangaza wengi ni kwa nini utekaji na mauji vinashika kasi Tanzania?
Alisema Mbowe msibani kwa Ali, kuwa inawezekana waliokuwa wanazomea wakatafsiriwa kuwa hawakuwa na nidhamu kwa viongozi wa Serikali, lakini akawataka kufanya marejeo ya matukio mfululizo ya watu kutekwa, ambayo hayajapatiwa majibu.
Tukio la kijana mwanaharakati, Edgar Mwakabela “Sativa”, kutekwa na kutupwa msituni Katavi, bado halina majibu. Mkusanyiko wa matukio yote yanatengeneza hali ya kutoamini dola.
Shughuli za mazishi zilifanyika Mzingani, Tanga. Kisha Ali alisafirishwa kilomita 13.2 hadi kijijini kwake Darigube, Tanga, alikozikwa. Sauti zilizosikika mazikoni Darigube na mazishini Mzingani, hisia na maumivu yake, zifike hadi Ikulu, kwa Rais Samia.
Watu wanapoteza imani na vyombo vyao vya usalama, sababu matukio ya nyuma hayana majibu.