Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lwakatare: Profesa Lipumba akigombea naondoa jina langu

Muktasari:

  • Lwakatare ni mmoja wa wanachama waliochukua fomu kuwania uenyekiti wa CUF kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba 13 – 15, 2024 badala ya Septemba 15, 2024 iliyokuwa imepangwa hapo awali.

Dar es Salaam. Kada mkongwe wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Lwakatare, mmoja wa waliochukua fomu kuwania uenyekiti wa chama hicho, amesema endapo mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba atagombea tena, yeye ataondoa jina.

Lwakatare ni miongoni mwa waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba 13 – 15, 2024 badala ya Septemba 15, 2024 iliyokuwa imepangwa hapo awali.

Kinyang’anyiro hicho, kitahusisha uchaguzi wa viongozi kwenye nafasi tatu za mwenyekiti, makamu mwenyekiti (Tanzania Bara na Zanzibar) na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho lililopo kwa mujibu wa katiba.

Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu, Lwakatare amesema Profesa Lipumba alimtamkia kwamba hatagombea tena nafasi hiyo, hivyo hatarajii kumwona kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Profesa Lipumba aliniambia mwenyewe kwamba hagombei, bahati nzuri wamejitokeza wagombea wengi, alinihakikishia yeye hagombei. Kwa hiyo akigombea nitakuwa mtu wa kwanza kushangaa,” amesema Lwakatare.

Amesisitiza kwamba akikuta jina la Profesa Lipumba kwenye kinyang’anyiro hicho, ataondoa fomu yake kwa sababu huko kutakuwa ni kuviziana, jambo ambalo hakubaliani nalo kwenye uchaguzi wa viongozi wa chama.

“Nimeambiwa kwamba wamejitokeza watu tisa kuwania nafasi ya mwenyekiti, hapo Profesa hayumo, akiingia naye atakuwa wa 10.

“Nikikuta kuna fomu ya Profesa (Lipumba), mimi ya kwangu naiondoa…kwa sababu amenitamkia mara tatu kwamba hagombei, sasa tutakwendaje namna hiyo kwa kuviziana,” amehoji Lwakatare.

Mwananchi limefanya jitihada za kumtafuta Profesa Lipumba, lakini hakupatikana, hata hivyo, baadhi ya watendaji wa chama hicho, wamethibitisha kwamba wafuasi wake wamemchukulia Profesa.

Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa amesema idadi ya waliochukua fomu hadi sasa katika nafasi ya mwenyekiti Taifa ni saba akiwemo mwenyekiti wa sasa, Profesa Lipumba ambaye alichukuliwa fomu na wanachama.

“Lipumba amechukuliwa fomu na wanachama wa CUF, baada ya kumuomba na kumbembeleza ndipo alikubali achukuliwe. Wanaamini anaweza kuwafikisha mbali kwa kuwa wametoka naye mbali na amekuwa akizunguka wilaya zote kuwatembelea,” amesema Ngulangwa.

Ngulangwa amesema kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Zanzibar, pande zote za muungano, watu sita wamejitokeza kila upande.

“Katika idadi hiyo, ni wachache wamerejesha fomu hadi sasa lakini kwa kuwa muda bado, ngoja tusubiri watakuja kwa kuwa muda bado wanao,” amesema Ngulangwa.

Alipoelezwa kuhusu Profesa Lipumba kuchukuliwa fomu, Lwakatare amesema hilo siyo jambo kubwa, lakini mwenhyekiti huyo akitia saini yake na kuirejesha, yeye hatashiriki kwenye uchaguzi huo.

“Kuchukuliwa fomu siyo ishu kubwa, ishu ni yeye mwenyewe kusaini hiyo fomu,” amesema Lwakatare ambaye amewahi kuwa mbunge wa Bukoba Mjini kupitia CUF na Chadema na Kiongozi wa Upinzani Bungeni.