Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madaraka, demokrasia, fainali ya ‘kombe la damu’



“Ash-shab yurid isqat an-nizam” ni kauli mbiu ya Kiarabu inayomaanisha “Wananchi wanataka utawala ung’oke.”

Mwaka 2011, kauli hiyo ikawa alama ya vuguvugu la Arab Spring lililoanzia Tunisia na kusambaa hadi Misri, Libya na baadaye Syria.

Kwa wengi, ilikuwa ishara ya matumaini ya kuondoa tawala zilizotuhumiwa kwa ukandamizaji na kuanzisha enzi mpya ya demokrasia.

Tunisia na Misri zilitoa msukumo kwa mataifa mengine. Walibya waliamini kuwa kama mataifa hayo yaliweza kumwondoa mtawala, basi wao pia wangefanikiwa kumng’oa Muammar Gaddafi. Hata hivyo, gharama ya safari hiyo ilikuwa kubwa.

Wakati Tunisia ilipoteza mamia ya watu na Misri takriban watu 2,000, Libya ilipoteza zaidi ya watu 30,000 katika mapambano yaliyopewa jina la kupigania demokrasia.

Wakati huo Walibya walikuwa pia na kauli mbiu “Aysh Libya hurra” – “Idumu Libya huru.” Miaka 15 baadaye, taswira ya Libya inaibua maswali mengi.

Nchi imegawanyika katika maeneo yenye tawala tofauti, haina mamlaka ya kitaifa yenye nguvu, usalama umedorora na wananchi wamejikuta wakitawaliwa na makundi yenye silaha.

Kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine si jambo rahisi, huku biashara haramu ya binadamu ikiendelea kushamiri.

Syria nayo ilifuata mkondo huo. Kisa kilichoonekana kuwa kidogo kilichochea mfululizo wa matukio makubwa.

Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14, Mouawiya Syasneh, aliandika ukutani maneno ya Kiarabu yaliyomaanisha, “Zamu yako inafuata, Daktari,” akimrejelea Rais Bashar al-Assad ambaye kitaaluma ni daktari wa macho.

Tukio hilo lilitafsiriwa kama wito wa mapinduzi, na baadaye nchi ikaingia katika vita vya muda mrefu vilivyosababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu.

Mifano hiyo inaonyesha kuwa machafuko ya kisiasa mara nyingi huanza kwa matumaini makubwa, lakini huishia kuacha majeraha makubwa kwa taifa.

Historia inaonyesha kuwa baada ya vurugu, gharama zinazobebwa na wananchi huwa kubwa kuliko mafanikio yaliyotarajiwa.

Uchumi hudorora, taasisi za dola hudhoofika, na maisha ya wananchi hujaa hofu na sintofahamu.

Ni kweli kwamba kuondolewa kwa tawala zinazokandamiza wananchi kunaweza kufungua fursa za mageuzi.

Hata hivyo, uzoefu wa mataifa mengi unaonyesha kuwa mabadiliko yanayopatikana kupitia ghasia mara nyingi huzaa matatizo mapya.

Maelfu ya watu hupoteza maisha, wengine hupotea bila kufahamika walipo, huku maendeleo ya kiuchumi na kijamii yakikwama kwa miaka mingi.

Athari hizo zinaonekana pia katika huduma za msingi. Wakati wa machafuko, shule hufungwa, hospitali na vituo vya afya hushindwa kutoa huduma, biashara husimama na wananchi hulazimika kukimbia makazi yao.

Ndoto za elimu kwa vijana hukatizwa, wagonjwa hukosa matibabu na familia nyingi hulazimika kuwa wakimbizi ndani au nje ya nchi zao.

Mfano mwingine ni Sierra Leone, ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kati ya mwaka 1991 na 2002 vilisababisha takriban watu 50,000 kupotea na hadi leo hatima yao haijulikani.

Aidha, mamilioni ya watu walilazimika kuhama makazi yao na kutafuta hifadhi katika mataifa jirani.

Changamoto nyingine ni kwamba machafuko yanayolenga kuwaondoa viongozi wanaotuhumiwa kwa ukandamizaji wakati mwingine huibua watawala wapya wenye tabia zilezile au hata mbaya zaidi.

Historia inaonyesha kuwa si rahisi kwa viongozi waliopatikana kupitia mapambano ya damu kuendesha dola kwa misingi ya maridhiano, utu na kuheshimu haki za binadamu.

Mara nyingi huanza kuwashughulikia wale wanaowaona kuwa tishio kwa utawala wao.

Katika mazingira hayo pia hujitokeza fursa kwa wanajeshi kutwaa madaraka. Mara nyingi tawala za kijeshi huweka mbele nidhamu na usalama kuliko misingi ya demokrasia na uwajibikaji.

Hivyo, wananchi waliotoka barabarani wakidai uhuru na haki wanaweza kujikuta chini ya mfumo mwingine wenye ukomo mkubwa wa haki na uhuru wa kisiasa.

Mtafiti wa Kituo cha Utawala wa Demokrasia katika Chuo Kikuu cha Harvard, Christopher Wiley Shay, katika andiko lake “Swords into Ploughshares”, anaeleza kuwa tafiti zinaonyesha nchi zinazobadili tawala kupitia vurugu huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na ukiukwaji wa haki za kiraia kuliko zile zinazofanya mabadiliko kwa njia za amani.

Hakuna shaka kwamba maandamano na machafuko huwa ni ujumbe kwa watawala kusikiliza sauti za wananchi, kuheshimu utawala wa sheria na kufanya mageuzi yanayohitajika.

Hata hivyo, uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa gharama ya kuyafikia mabadiliko kupitia umwagaji damu mara nyingi huwa kubwa kuliko manufaa yanayotarajiwa.

Vilevile, watawala wanaotumia nguvu za dola kuua wananchi ili kuzima machafuko nao hubeba lawama kubwa kwa kuendeleza utawala wa damu.

Mwishowe, hakuna upande unaoweza kudai ushindi wa kweli wakati taifa limebaki na majeraha, uchumi uliodorora na wananchi waliopoteza maisha au matumaini yao.

Ndiyo maana ni muhimu kutafakari kwa kina kila wito wa mabadiliko unaoambatana na vurugu.

Demokrasia ni lengo muhimu, lakini inapopatikana kwa gharama ya maisha ya maelfu ya watu na uharibifu mkubwa wa taifa, kinachobaki si ushindi wa wananchi, bali ni kombe la damu ambalo hakuna anayelinyanyua kwa fahari.