Mafyatu wanataka muungano si mgongano

Juzi Tunda Lishe alilikoroga. Si alihoji mantiki ya Zenj kuua Tanganyika hata kutaka wadanganyika wawe na pasipoti kuingia Zenj. Baada ya kukinukisha, si kiliuma. Machawa na mazwazwa wajikombao wapate shibe si walilidhalilisha hata Bungo!

Alianza mmoja aliyetaka eti Wadanganyika waingie Zenj kwa pasi ilhali Wazenj waingie bwerere na kuishi watakavyo. Tunda alihoji mantiki ya Wazenj kumiliki ardhi Danganyika ilhali Wadanganyika wasiimiliki Zenj, na uraia pacha japo hakuuita hivyo (Wazenj wana Uzenj lakini Wadanganyika hawana Udanganyika).

Bila aibu, tunaambiwa Tanzia hairuhusu uraia pacha. Iweje Wazenj wana vitambulisho vya uraia tena wao na si wetu tunaodai unatokana na muungano huu mgongano? Nani anamtawala nani?

Lishe alipomwaga upupu, walizuka mazwazwa wanaojifanya kumpenda na kumtetea mama asiwakatishe kuramba asali kama alivyowahi kudai Mgoshi Makambale. Walibwabwaja na kubwata kuwa Tunda na chata lake la CHAKUDEMA watengwe, wakaripiwe, hata kulaaniwa. Je, kuna mantiki gani kuwachukia wanaosema ukweli? Najua sensitivity a.k.a unyeti wa ninachoandika. Nitafyatua kama ifuatavyo kwa uchache tu japo kifyatu:

Mosi, kinachoitwa muungano si chochote, bali mgongano hata mnyonyano, hasa tukizingatia kuna ubaguzi katika kuuendesha. Iweje Zenj ambayo ni ndogo kuliko mikoa yote bara iwe na rahis badala ya mkuu wa nkoa, sirkal, na taasisi zake huru halafu tuzugane kuwa tumeungana?

Muungano wa kweli ni kama ndoa. Wawili wauingiao huwa na haki na stahiki sawa bila kunyonyana, kugongana, kutobozana, kutishana na kuchukiana. Hivi ni kosa kusema kuwa muungano wetu mgongano uliua Danganyika japo ulishindwa kuizika?

Pili, mafyatu tunapaswa kufyatuka. Tuhoji tujue ukweli ili haki itendeke. Haiwezekani tujione tuko sawa wakati wenzetu wana rahis wao hata bendera. Tukiwa wakweli, unaweza kulinganisha uzalishaji kiuchumi na uchangiaji wa pande mbili za mgongano?

Zenj ina ukubwa wa eneo wa kilomita za mraba 2,462. Danganyika ina kilomita za mraba 944,841 kwa hesabu za ngumbaru, Zenj ni ndogo kwa Danganyika mara 383.769694314. Hii maana yake nini? Kama tutatenda haki ikatendeka, kila fedha inayomilikiwa na Tanzia, Zenj ikipewa shilingi moja, Danganyika yapaswa kupewa 384.

Kama ingekuwa kampuni, Zenj ikiwa na hisa moja, Danganyika inakuwa nazo 384. Haya ni mahesabu rahisi yaliyowapiga chenga walioasisi hiki kiini cha mgongano. Na huu ni ukweli hata kama mchungu. Namba huwa hazidanganyi.

Tatu, tukubaliane kutokubaliana ili tuweze kukubaliana kwa busara kuwa muungano si chochote, bali mgongano na chanzo cha migongano isiyoisha hadi tunaanza kutaka mafyatu wa upande mmoja wabebeshwe pasi za kusafiri kwenda Zenj.

Tukifanya hivyo, Wadanganyika watakuwa na tofauti gani na Wakenya na Waganda na wengine? Tofauti ni kwamba hawa wengine hawatumii njuluku zao kuwagharimia na kuwastarehesha wanaojiita wenzao wakati wao wakiumia kwa kujiumiza kutokana na siasa za zamani.

Kwa wasiojua mantiki ya huu mgongano, wajue, tuliunganishwa na Wamarekani kuepuka Zenj kuwa Kyuba ya Afrika kama lilivyoandika Jarida la The New York Times (Machi 28, 1964, uk 18). Nanukuu: “Like Cuba, Zanzibar now turns steadily eastward for inspiration. Washington prays that President Karume, a stubborn if not impressively intelligent man, will emulate such nonaligned leaders as Tanganyika's Nyerere. But Karume is almost surely Zanzibar's Kerensky.”

Tafsiri: “Kama Kyuba sasa Zanzibar, kwa uthabiti, imeelekea mashariki kwa ajili ya msukumo, Washington inasali au kuomba kuwa Rais Karume, mtu msumbufu kama siyo mwenye akili ataigiza viongozi wasiofungamana kama Nyerere wa Tanganyika. Hata hivyo, Karume ana uhakika wa Zanzibar ya Kerensky.”

Alexander Fyodorovich Kerensky (Aprili 22, 1881 hadi Juni 11, 1970) alikuwa mwanasheria na mwanamapinduzi wa Kirusi aliyeongoza serikali ya mpito ya Urusi kuanzia Julai hadi Novemba 1917, kabla ya kujiunga na serikali ya kimapinduzi ya Urusi.

Kuna mfanano baina ya Karume na Kerensky. Wote waliunganisha serikali zao kuepa kupinduliwa na waliowapindua. Serikali zao zilidumu kwa miezi minne, Kerensky kuanzia Julai 21, 1917 hadi Novemba 7, 1917 na Karume kuanzia Januari 12, 1964 hadi Aprili 26, 1964.

Wote walipoteza urais, Karume akawa Makamu wa Rais na Kerensky Waziri wa Vita. Tofauti na Karume, Kerensky na alioungana nao waliunda taifa lenye muungano wa kweli wakati Karume aliunda mgongano a.k.a muungano unaoendelea kuzua minong’ono toka pande zote.

Nne, nini kifanyike? Kama kiongozi wa mafyatu, mafyatu wameniambia kuwa wanachotaka ni muungano wa kweli kama ndoa wenye sirkal moja kama Urusi. Wanataka Zenj iwe mkoa, tena ambao utakuwa ndiyo wa pili kwa udogo, hasa ikizingatiwa kuwa mkoa mdogo Danganyika ni Dar es Salaam, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,393.

Leo sifyatui mengi. Muhimu nimetumia namba kuondoa mgongano na usanii wa kisiasa vilivyoleta ubaguzi wa kikatiba. Hivyo, wanaomzomea Tunda Lishe ndio wapaswao kuogopwa, kuzomewa, kukaripiwa na kulaaniwa.

Mafyatu wanataka muungano si mgongano. Hivi leo nimekunywa ngapi?