Mahakama yatupilia mbali maombi ya mapitio kesi ya uchaguzi Kigoma Mjini
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando au Baba Levo (CCM).
Muktasari:
- Mahakama imetupilia mbali maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) baada ya kubaini waombaji hao wameshindwa kukidhi vigezo muhimu vya kisheria vinavyoruhusu mapitio ya uamuzi.
Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, imetupilia mbali maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), waliokuwa wakiomba mahakama ipitie upya uamuzi wake wa Desemba 16, 2025 uliotolewa katika shauri hilo la uchaguzi namba 28949/2025.
Katika maombi hayo, waombaji waliomba mahakama itengue amri iliyoambatana na uamuzi huo, wakidai kuwepo kwa dosari iliyotokana na utoaji wa msaada wa kisheria kwa walalamikaji kwenye shauri la awali.
Maombi hayo yaliwasilishwa chini ya Amri ya XLII Kanuni ya 1(1)(b) pamoja na kifungu cha 88(1)(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, yakitegemea hoja kuu ya kuwepo kwa ushahidi mpya, ambao haukuwepo wakati uamuzi wa awali unatolewa.
Katika shauri la awali la uchaguzi, walalamikaji Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, wanapinga ushindi wa mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando au Baba Levo kupitia CCM.
Uamuzi huo umetolewa Mei 4, 2026 na Jaji Projestus Kahyoza, aliyekuwa akiyasikiliza.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema ushahidi mpya uliowasilishwa kama msingi wa maombi ya mapitio haujitoshelezi na ni wa kutilia shaka, hivyo ikayatupilia maombi hayo.
Msingi wa maombi
Awali wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo la uchaguzi mapingamizi ya kisheria yaliibuliwa ikiwemo wajibu maombi wa kwanza hadi wa nne kutokuomba wala kulipa dhamana ya shauri kama ambavyo kifungu cha 140(2),(3),(5),(7) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 kinavyoelekeza.
Mahakama hiyo baada ya kusikiliza pande zote, ilitupilia mbali mapingamizi hayo baada ya kujiridhisha kuwa walalamikaji katika shauri hilo walikuwa ni wanufaika wa msaada wa kisheria, kwa hiyo hawakuhitaji kulipa au kuweka dhamana ya gharama za shauri.
Hata hivyo, katika maombi ya mapitio, waombaji walidai kuwa wamepata ushahidi mpya unaoonyesha kuwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoa msaada wa kisheria bila kuwa na usajili halali wakati huo, hivyo kufanya uamuzi wa awali kuwa na dosari.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo waleta maombi waliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Vivian Method pamoja na Wakili wa Serikali Mwandamizi, George Kalenda huku mjibu maombi wa kwanza hadi wa nne wakiwakilishwa na John Seka na Baba Levo akiwakilishwa na Daniel Rumenyela na Emmanuel Msasa.
Akiunga mkono maombi hayo, Wakili Vivian alitaja vifungu vinavyoipa mahakama hiyo mamlaka ya kufanya mapitio ya uamuzi wake kuwa ni Amri ya XLII Kanuni 1 (1) (b) pamoja na kifungu cha 88 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai.
Mbali na vifungu hivyo wakili huyo alirejea mashauri mbalimbali ikiwemo shauri la Emmanuel Jagero na wengine watatu dhidi ya Multimodal Transport Africa Ltd, shauri la mapitio namba 2/2012 linaloonyesha mamlaka ya mahakama hiyo katika mapitio na sababu zinazoweza kupelekea kufanya hivyo.
Alisema msingi wa maombi hayo ya mapitio ni hoja kuu moja ambayo ni upatikanaji wa ushahidi mpya unaoonyesha TLS ilitoa msaada wa kisheria kwa walalamika katika shauri hiyo pasipo kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.
Akitaja masharti yaliyoainishwa juu ya mahakama kufanya mapitio katika maamuzi yake, wakili huyo amerejea shauri la Mohamed Enterprises (T) Limited dhidi ya Thanh Hoa Ltd Co na kueleza upatikanaji wa ushahidi mpya ni sharti mojawapo la msingi kwa mahakama kufanyia mapitio uamuzi wake.
Amedai kwamba awali wakati shauri likiendelea hadi kumalizika hawakuwa na taarifa ya TLS kutokuwa na mamlaka ya kutoa huduma za msaada wa kisheria mpaka pale walipopata ufafanuzi kwa njia ya barua kutoka kwenye mamlaka husika.
Alidai kuwa Wizara ya Katiba na Sheria iliwafahamisha waleta maombi kuwa TLS ilipewa usajili wa kutoa huduma za msaada wa kisheria Aprili 29, 2019 kwa muda wa miaka mitatu ambapo usajili huo uliiisha Aprili 28, 2022.
Amedai kutokana na ushahidi huo mpya wamebaini kwamba kutokulipa dhamana ya gharama za shauri tajwa la uchaguzi kulipelekea dosari katika shauri hilo na kuwa ufafanuzi huo ulipatikana baada ya mahakama kuwa imeshatoa uamuzi wake.
Aidha amedai walichukua hatua stahiki ili kupata ufafanuzi juu ya TLS kutoa msaada wa kisheria na kwamba mpaka uamuzi unatoka, hawakuwa wamepata ufafanuzi huo na kuiomba mahakama itengue uamuzi wake na amri zake za Desemba 16, 2025.
Kwa upande wao, wajibu maombi wa kwanza hadi wa nne kupitia wakili wao John Seka walipinga maombi hayo, wakieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa ni wa kutilia shaka kwa kuwa haukuambatana na cheti cha usajili kinachodaiwa kuisha muda wake.
Ameeleza kuwa cheti cha usajili wa TLS, yaani cheti namba LAP-2019-0003 si sehemu ya kumbukumbu za mahakama kwenye shauri hilo la mapitio na wala hakikuwa sehemu ya kumbukumbu za shauri mama ambalo uamuzi wake unaombewa mapitio.
Amedai kuwa cheti kilichopo mahakamani ni Legal Aid Certificate na siyo Certificate of Registration ya TLS na kuwa barua kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Februari 12, 2026 ni mawasiliano ya ndani kati ya taasisi mbili za Serikali na haionyeshi kama imehusisha TLS kwa namna yoyote ile.
Kwa mujibu wa wakili huyo TLS imekuwa ikitoa msaada wa kisheria tangu ilipoanzishwa mwaka 1954 na hata kabla ya sheria ya msaada wa kisheria kupitishwa, hivyo anaamini suala la TLS kutoa msaada wa kisheri lipo chini ya kifungu cha nne cha Sheria ya TLS.
Akirejea hoja yake ya kuyachukulia maombi hayo kwa tahadhari kubwa, wakili huyo ameonya kwamba upo uwezekano wa mahakama hiyo kuwa ya kwanza kusema TLS haina mamlaka ya kisheria ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi na kuomba mahakama itupilie mbali maombi hayo.
Uamuzi Jaji
Katika uchambuzi wake, Jaji Kahyoza ameeleza kuwa sheria inaweka masharti matatu muhimu kwa mahakama kufanya mapitio ya uamuzi wake, kuwepo kwa ushahidi mpya muhimu, ushahidi huo kuwa wa kuaminika na usio na shaka, na kwamba ushahidi huo haukuweza kupatikana licha ya juhudi zote kabla ya uamuzi wa awali.
Mahakama ilieleza kuwa hatua za kutafuta ushahidi zilichelewa kuchukuliwa, kwani barua ya kuomba ufafanuzi iliandikwa Desemba 12, 2025, wakati tayari shauri lilikuwa limefunguliwa Novemba 14, 2025 na usikilizwaji ulikuwa umekamilika.
Kwa mtazamo wa mahakama, hatua hizo zilipaswa kuchukuliwa mapema zaidi, na kuchelewa huko kulionyesha ukosefu wa juhudi za kutosha.
Pili, kuhusu uhalali wa ushahidi, mahakama ilieleza kuwa barua ya Katibu Mkuu pekee haitoshi kuthibitisha madai bila kuambatana na cheti halisi cha usajili wa TLS.
Mahakama imesisitiza kuwa anayetoa madai ana wajibu wa kuthibitisha kwa ushahidi thabiti, na katika kesi hii, kutowasilishwa kwa cheti hicho kulifanya ushahidi huo kuwa na mashaka.
Jaji Kahyoza alieleza kuwa hata katika mashauri ya madai ambapo kiwango cha uthibitisho ni “uwezekano zaidi ya nusu”, bado ushahidi uliowasilishwa haukufikia kiwango hicho.
Aidha, mahakama ilikumbusha kuwa mapitio si njia ya kurejea hoja au ushahidi ambao ungeweza kuwasilishwa katika shauri la awali, bali ni kwa ajili ya kusahihisha makosa yaliyo wazi au kushughulikia ushahidi mpya ambao haukuweza kupatikana kwa wakati.
“Kwa mtazamo wangu na kwa hali ya kawaida hatua kama hizi zilipaswa kuchukuliwa mara baada ya shauri kufunguliwa, kwa kuzingatia kuwa shauri hilo linamhusisha AG, ni wazi ofisi hizi zilikuwa na nafasi ya kuliona suala hili mapema na kuchukua hatua stahiki,” amesema Jaji.
“Nasema hivyo kwa sababu ofisi hizo ni sehemu ya Serikali kama ilivyo Wizara ya Katiba na Sheria, haiingii akilini ni kwa namna gani ushahidi huu usingeweza kupatikana kabla ya uamuzi kutolewa wakati wahusika wote si tu sehemu ya Serikali, bali wote wapo ndani ya wizara moja,” amesema.
Jaji amefafanua katika maombi ya sasa kwa msingi wa ushahidi huo mpya ni cheti cha usajili cha TLS, ilikuwa muhimu mwenye kutoa madai hayo kuwasilisha cheti husika ili kuthibitisha madai yake na cheti hicho kingeweka msingi mzuri wa maamuzi ya mahakama.
“Katika shauri letu la sasa nimebainisha bayana kigezo cha kwanza na cha tatu havijatimizwa, hivyo hata pasipokuangalia kigezo cha pili ni wazi takwa la ushahidi mpya kama nguzo muhimu la maombi ya mapitio linakuwa halijatimizwa,” amehitimisha.