Mama Mongela awafunda UWT

Rais Mstaafu wa Bunge la Umoja wa Afrika, Getrude Mongela

Muktasari:

  • Wakati Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), ukiwapongeza, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Taifa wa UWT kuchaguliwa kushika nafasi hizo, Rais Mstaafu wa Bunge la Umoja wa Afrika, Getrude Mongela amewafunda jinsi ya kurejea katika UWT ya mwaasisi wa umoja huo, Sofia Kawawa 

Dodoma. Rais Mstaafu wa Bunge la Umoja wa Afrika, Getrude Mongela amewataka viongozi wa Taifa wa Umoja wa Wanawake wa CCM, (UWT), kuondoa uoga wakati wa kuelezea matatizo ya wanawake nchini.

Mongela ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 9, 2022 wakati wa kongamano la kuwapongeza Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Samia Suluhu na viongozi wa Taifa wa UWT kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.

“Kazi yenu ya kwanza nyie wawili (mwenyekiti na makamu wa UWT), kuacha uoga. Matatizo yetu sisi wanawake tunahitaji tusemewe na watu wasio waoga. Mkiona kuna matatizo nyie, tunanyanyasika, mwende moja kwa moja hata mbele ya mtutu kuzungumza,”amesema.

Amesema hayo ameyaona kwa Kawawa ambaye alikuwa akienda moja kwa moja kwa Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere na kumwelezea bila kumogopa.

Mongela amesema wanawake watamsaidia Rais Samia asizibe mwanya wa wanawake kwa kunyooshewa vidole na kwamba yeye hawezi kulifanya pekee yake bila msaada wa watu wengine.

 “Hawezi kuifanya kazi hii pekee yake, ni sisi katika wilaya zetu, ni sisi katika sehem zetu wote tutakaomshika mkono aweze kufanya yale tufike mahali tusiseme kwanini tumchelewa kuwaweka wanawake,” amesema.