Prime
Mbowe akubali kushindwa Chadema, ampongeza Lissu

Freeman Mbowe na Tundu Lissu wakijadili jambo baada ya kurudi ndani ya ukumbi wa Mlimani City leo Januari 22, 2025.
Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameamua kubadili 'jenerali' katikati ya vita, baada ya kumchagua Tundu Lissu kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Mgombea nafasi ya Mwenyekiti Chadema Taifa, Tundu Lissu akijadiliana jambo na John Heche ambaye amegombea nafasi makamu mwenyekiti wa chama hicho Bara wakati wakiwa ndani ya ukumbi wa Mlimani City leo Jumatano Januari 22, 2025.
Lissu ameshinda nafasi hiyo dhidi ya mshindani wake Freeman Mbowe aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 21 katika mkutano wa uchaguzi ulioanza asubuhi ya jana Jumatatu na unaendelea leo Jumatano, Januari 22, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo wa wajumbe, unahitimisha safari ya miaka 21 ya uenyekiti wa Mbowe aliyepokea wadhifa huo kutoka kwa Bob Makani tangu mwaka 2003.
Lissu anakuwa mwenyekiti wa nne wa Chadema akitanguliwa na Edwin Mtei, Bob Makami na Mbowe.
Licha ya matokeo ya jumla kutotangazwa baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu matokeo yatatangazwa baadaye, lakini ukumbini shangwe limetawala.

Mgombea uenyekiti Chadema Taifa, Tundu Lissu akifurahia akiwa ndani ya ukumbi wa Mlimani City kabla ya matokeo rasmi ya uenyekiti wa chama hicho kutangazwa.
Msingi wa shangwe hilo ni kura za nafasi ya uenyekiti zimemalizika kuhesabiwa na mawakala wa Lissu kwa namna moja au nyingine wamepenyeza matokeo ya awali.
Katika ukurasa wa kijamii wa X wa Mbowe ameandika ujumbe wa kukubali kushindwa akiweka na picha aliyopiga na Lissu na kuandika: “Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa chama chetu Chadema uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu.”
Wajumbe kabla ya matokeo
Ukimya ulitawala kwa timu inayomuunga mkono Mbowe, huku ile ya Tundu Lissu ikionekana kufurahia.
Hizo zilikuwa rasharasha za matukio ya ukumbini kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, katika uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa Chadema.
Ulifika wakati wajumbe wanaomuunga mkono Lissu walionekana kukumbatiana, kupeana mikono na kupongezana.
Hatua hiyo ilifuatiwa na furaha inayoashiria ushindi kutoka kwa baadhi ya wajumbe hao na hawakuwa wametulia ukumbini hapo.
Wajumbe hao wa timu Lissu walionekana kukaa vikundi vikundi na mmoja mmoja alichomoka kwenda kwenye kikundi kingine, huku wakinong'ona na kupeana mikono.
Yote hayo yaliendelea katika kipindi ambacho matokeo rasmi ya uchaguzi huo hayajamtangaza Mbowe, Lissu wala Charles Odero kuwa ndiye mshindi.
Kwa upande wa wajumbe waliojinasibu kumuunga mkono Mbowe, walikuwa kimya na macho ya wengi yalielekezwa kwenye runinga zilizokuwepo ukumbini hapo zinazoonyesha mawakala wakihesabu kura.
Dakika chache baadaye, wafuasi wa Lissu walisimama ukumbi mzima na kushangilia, hatua iliyosababisha Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika awaamrishe watulie.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa anayemaliza muda wake, Freeman Mbowe akikumbatiana na Makamu wake Bara, Tundu Lissu wakati wakiwa katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Sambamba na hilo, alitangaza kukamilika kwa hatua ya kuhesabiwa kura na wanaopaswa kusaini fomu za matokeo wameshafanya hivyo.
Hata hivyo, amesema nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, uchaguzi wake ulipaswa kurudiwa kwa kuwa hakuna mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50.
Duru ya pili ya upigaji kura, iliwahusu Said Mzee Said na Said Issa Mohamed ambao ndio wagombea walioongoza kwa kura.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi