Mbowe: Hiki ni kipindi cha kupima viongozi
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amewaachia wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi kuamua nani atakayekiongoza chama hicho kwa nafasi ya uenyekiti katika miaka mitano ijayo
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema mashinikizo na msongo kinaoupitia chama hicho wakati huu ni kipimo sahihi cha uvumilivu, ustahimilivu, haiba na uwezo wa viongozi kutunza siri na kuilinda taasisi.
Amesema kwa kipimo hicho, anawaachia wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi kuona nani atafaa kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mbowe ametoa kauli hiyo zikiwa zimesalia siku 10 kufanyika uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti, ambao yeye anagombea kutetea kiti hicho, huku washindani wake wakiwa ni Makamu wake Bara, Tundu Lissu, Romanus Mapunda na Charles Odero. Uchaguzi huo utafanyika Januari 21, mwaka huu.
Mbowe amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Ijumaa, Januari 10, 2025 alipohojiwa katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds.
“Watoto wa mjini wanasema acha inyeshe tujue panapovuja. Kipindi cha shinikizo na msongo kama hiki ndiyo unaweza ukapima uvumilivu, ustahimilivu wa viongozi, haiba ya viongozi, uwezo wa kutunza siri za taasisi, uwezo wa kuilinda taasisi.
“Huwezi ukaibagaza taasisi unayotaka ukaiongoze kwamba imejaa rushwa halafu ukiambiwa baba basi toa mfano mmoja wa rushwa, na wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chama, kuhusu hiyo rushwa hebu ielezee leo tuione. Unatoka tu Mama Abdul… Mama Abdul, na Abdul fedha Abdul, ni mambo ya kihuni,” amesema.
Amesisitiza wana-Chadema ndiyo watakaoamua kwa kuangalia vigezo vyote hivyo, kwamba nani atakayekiongoza chama hicho na kikabaki salama.
Ameeleza kushangazwa na wanaoshinikiza aache kugombea nafasi hiyo, akisema nyuma yao kuna makundi ya wasio wanachama na wengine walishakikimbia chama hicho.
Pamoja na mashinikizo yote, amesema wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi ndiyo wenye uamuzi wa nani anayepaswa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa siku zijazo, hivyo amewaachia wao kazi hiyo.
Amesisitiza kuwa amekuwa akiangalia wanaochochea yeye aache kugombea, kwa upande wa pili wengi hawaitakii mema Chadema na kwamba huo si utamaduni wa chama hicho.
“Huo siyo utamaduni wetu na utamaduni huo hauwezi ukaiacha taasisi yetu salama, kwamba kiongozi unataka uongoze kwa kuwakanyaga wenzio halafu unajinasibu kwamba unafaa kuwa kiongozi wa taasisi,” amesema.
Mbowe amesema amejenga watu wengi kwenye siasa na amekuza vipaji kiasi kwamba hakuna kiongozi hata mmoja ndani ya Chadema anayeweza kusema hakupita mikononi mwake.
“Unaweza ukawapima viongozi kwa utulivu, busara, matendo na kauli zao. Kama ambao wanajiona wana busara kuiongoza taasisi hii, ambao wanafikiri wana haki ya kuachiwa taasisi hii, jambo jema. Tuna njia nyingi za kuwapima, tunafahamiana kwa muda na kwa wakati.
“Muda unatatua matatizo mengi sana. Naweza nikakaa na mtu kwa miaka 10 nisimjue, ukafika wakati nikamjua nikajiuliza huyu ndiye yeye ambaye tumeishi naye miaka 10, tumekula naye, tumelala nyumba moja, tumeumia pamoja. Yeye kawaje,” amesema.
Hofu Lissu kuondoka
Alipoulizwa iwapo Lissu atatoka katika chama hicho haoni kama kinaweza kupasuka, Mbowe amejibu Chadema ni kubwa kuliko mtu yeyote binafsi na wanachama hawapo ndani ya chama hicho kwa ajili ya sura za viongozi fulani.
“Chadema ni kubwa kuliko Lissu, Chadema ni kubwa kuliko Mbowe. Hiki chama kimebeba matumaini ya maelfu na mamilioni ya Watanzania wanaotumaini kwamba kitaleta mabadiliko katika nchi hii,” amesema.
Amesema kila mmoja ndani ya chama hicho ana wafuasi wake kwa njia yake na nguvu ya yeyote katika Chadema inatokana na umoja uliokuwepo.
“Ambaye anafikiri akiondoka Chadema ‘atasepa na kijiji’ wanavyosema vijana wa mjini, atachoka sana,” amesema.
Mbowe amesema kwa historia aliyonayo na Makamu wake Bara, Lissu, anashangazwa na maneno anayozungumza dhidi yake, huku akieleza hana ugomvi naye binafsi.
Amesema anasikitishwa na yanayoendelea kati yao, akisema si Lissu pekee, mgombea yeyote iwapo atashindwa kwenye chaguzi zijazo ataendelea kumuhitaji ndani ya chama hicho.
“Huwa ninakaa namuangalia Tundu Lissu ninayemjua, niliyekuwa naye, niliyeshirikiana naye, niliyefanya naye kazi binafsi, za kisheria, za kifamilia, za kisiasa, za kibunge, halafu anatoa kauli anazozitoa dhidi yangu. Siyo yeye tu, hata baadhi ya viongozi wengine kweli kibinadamu hainipendezi,” amesema.
Amesema anajipa ujasiri wa kuvumilia jambo hilo ili asijenge chuki na kisasi kwa sababu mambo hayo kwa ujumla yanapita. Hata baada ya uchaguzi iwapo atashinda, si Lissu pekee, hata wagombea wengine watakaoshindwa ataendelea kuwa nao.
Mabadiliko ya katiba
Alipoulizwa iwapo amewahi kukwaza mabadiliko ya katiba ya Chadema, Mbowe amesema hakuna yeyote aliyewahi kufanya hivyo na kwamba mwanachama na kiongozi yeyote bila kujali ngazi yake anaweza kupendekeza mabadiliko ya katiba.
“Utaratibu huo upo ndani ya katiba ya Chadema, hapajawahi kutokea kiongozi yeyote akaelekezwa kuhusu badiliko lolote likakataliwa,” amesema.
Ameeleza kuwa hoja ya madai ya Mbowe kukwaza mabadiliko ya katiba, imeibuliwa na Lissu, ambaye ndiye aliyekuwa miongoni mwa viongozi muhimu katika kujenga katiba iliyopo sasa.
“Katika haya mambo ya kisiasa kuna wakati zinajengwa propaganda ambazo ni sanaa ya kijamii na kisiasa inayojaribu kubadilisha ukweli kuonekana uongo na uongo kuonekana ukweli,” amesema.