Prime
Mguu alioondokea Chongolo kukaribisha zama ngumu CCM
Daniel Chongolo kujiuzulu ukatibu mkuu CCM, linaweza kuwa jambo lisilo na uzani mkubwa. Mguu ambao ameondokea, unaweza kuchora mstari wa ujio wa zama za tofauti kabisa.
Kwa uongo au usahihi wa tuhuma za Chongolo, zilizomfanya aandike barua ya kujiuzulu, zinachagiza mwanzo mpya. Chongolo alimwandikia Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, barua ya kujiuzulu, Novemba 27, 2023.
Kabla ya kuandika barua hiyo, Chongolo alishughulikiwa mitandaoni. Nakala za mazungumzo baina ya watu wawili, ikidaiwa ni Chongolo na mwanamke fulani, zilivujishwa mitandaoni; Twitter, Instagram, Facebook na makundi ya WhatsApp.
Nakala hizo ambazo zilichukuliwa kwa mfumo wa picha za kioo cha simu (screenshot), zilibeba tuhuma kuwa Chongolo alikuwa ‘akichati’ kimapenzi na mwanamke huyo. Walikwenda mbali zaidi hadi kuombana na kutumiana picha za maungo ya siri.
Zipo tuhuma nyingine kuwa alikuwa akilewa kupitiliza na kupata ajali mara kwa mara, akiwa na wanawake. Kila kilichosemwa, kwa uongo au usahihi wake, bado ni tuhuma. Ukweli anao Chongolo na walioeneza habari hizo.
Kuna mambo nitayajengea hoja; kwanza ni barua ya Chongolo. Alimwandikia Rais Samia kuwa sababu ya kujiuzulu ni “kuchafuliwa mitandaoni”. Hajakanusha uhusika wa yaliyosemwa.
Chongolo kwa kuanzia, alipaswa kumwandikia Rais Samia kuwa yanayosemwa juu yake ni uzushi, kisha angeomba kujiuzulu kwa ajili ya kulinda heshima ya chama, Mwenyekiti na wana-CCM wote popote walipo. Angalau hapo angevuna huruma.
Kitendo cha barua yake kukosa sentensi hata moja ya kukanusha tuhuma dhidi yake, kinaweza kusababisha watu wengine wawaze kwamba Chongolo amejiuzulu kwa aibu, baada ya mambo yake ya faragha kuwekwa hadharani.
Mwingine atasogea mbele na kusema kuwa kama amejiuzulu kwa aibu, basi hajachafuliwa. Isipokuwa amejichafua mwenyewe kwa kufanya mawasiliano yasiyo na staha. Bila kuzingatia dhamana kubwa aliyoibeba kama mtendaji mkuu wa CCM.
Nafasi aliyoishikilia CCM imepata kukaliwa na watu wazito, Pius Msekwa, Rashid Kawawa, Horace Kolimba, Lawrence Gama, Philip Mangula, Yusuf Makamba, Wilson Mukama, Abdulrahman Kinana na Dk Bashiru Ally.
Chongolo alipaswa kutambua uzito wa nafasi aliyokuwa anaishikilia. Kwa kupima uzani wa chama, vilevile watangulizi wake. Tafakuri ambayo angejijengea ingemwongoza jinsi ya kuishi na kuenenda kwa hadhi stahiki.
Chongolo amekuwa mtendaji mkuu wa CCM. Chama kilichoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye amewahi kusema “ukipewa nafasi ya uongozi inabidi ujiheshimu.” Mwalimu alisema, huwezi kutaka kuwa kiongozi wakati unafungamana na wanawake wa barabarani.
Tusogee ngazi ya pili
Nakala za mawasiliano ya Chongolo ni mchezo mchafu. Ikiwa zile screenshot ni halisi, basi yule mwanamke aliyekuwa akiwasiliana naye ndiye amehusika kuvujisha. Swali hapa ni nani yupo nyuma ya huyo mwanamke?
Endapo screenshot hizo ni uongo, maana yake kuna kazi ilifanywa maalumu kumshughulikia Chongolo. Kutengeneza ujumbe na kuusambaza kumvunjia heshima na kumwondolea hadhi ya kijamii na kiuongozi.
Kwa tafsiri zote hizo, kinachokaribishwa CCM ni zama za kushughulikiana. Kundi fulani likiwa halina uhusiano mzuri na kiongozi fulani, linatengeneza majambo ya fedheha yenye kumhusu wasiyempenda, yanasambazwa mitandaoni, kisha analazimishwa kujiuzulu.
Ni kweli, Mwalimu Nyerere alipaswa kusimulia mkasa wa mke wa Mfalme Julius Caesar, Pompeia, kutuhumiwa kimapenzi nje ya ndoa. Japokuwa baraza la mfalme lilibaini hakukuwa na ushahidi juu ya tuhuma za Pompeia, bado Caesar alimtaliki kwa hoja kuwa “mke wa Caesar lazima awe juu ya tuhuma.”
Usahihi huohuo upo kwa Chongolo. Katibu Mkuu wa CCM anapaswa kuwa juu ya aina ya tuhuma ambazo Chongolo ametuhumiwa. Pamoja na ufahamu huo, zama hizi sio za Roma ya kale. Mitandao inaangusha dola, itakuwa mtu na cheo?
Mitandao iliiangusha dola ya Muammar Gaddafi Libya, ikapindua serikali Tunisia, ikazua vuguvugu la mapinduzi nchi za Kiarabu (Arab Spring). Kama CCM wasipozingatia, siku zijazo watajikuta wanaamuliwa viongozi wao na mitandao.
Watamweka Katibu Mkuu huyu au kiongozi mwingine yeyote kwenye chama, wasiomtaka watakoroga yao mpaka aondolewe. Hili lililoanza kwa Chongolo, lisiposhughulikiwa kwa umakini mkubwa kwa namna ya kudhibiti mazoea kujirudia, linaweza kualika zama ngumu mno CCM.
Mkazo ngazi ya pili
Screenshot zinazodaiwa kuwa za Chongolo zilivujishwa siku chache kuelekea mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM. Mtu yeyote anaweza kuwaza kwa haraka kwamba kilicholengwa ni cheo cha ukatibu mkuu CCM.
Chongolo anapaswa kukitendea haki chama chake kwa kutoka na kuwaweka bayana watu ambao ana ugomvi nao. Je ni siasa? Chuki dhidi yake ni nje ya siasa? Kauli ya Chongolo inaweza kuifanya CCM iwe imara mbele ya safari.
Ukimya wa Chongolo unaweza kujenga wasiwasi kwa kila aliye ndani ya chama. Je, nani mwingine atafuata? Chongolo kachomolewa na screenshot za WhatsApp na mwanamke, anayefuata atakorogewa jambo lipi?
Tathmini hoja kwa hoja tangu aya ya kwanza, kuna jambo ambalo halibishaniwi. Ni kuhusu Chongolo kuundiwa shambulizi. Kwa mantiki hiyo, yeye mhusika atakuwa anawajua wabaya wake. Ni akina nani? Wamefikiria nini? Ni vita ya ukatibu mkuu? Urais? Ni mambo nje ya CCM, lakini mahasimu wake wakaamua kumning’iniza kupitia chama?
Taifa limebakiza miaka miwili kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu. Katibu Mkuu ni kiungo muhimu katika kumpata mgombea. Je, makundi ya urais ndiyo yamemning’iza Chongolo? Kama ndivyo hii ni hatari sana kwa Mwenyekiti wa chama.
Utamaduni wa CCM siku zote ni kumvalisha kofia ya uenyekiti, rais atokanaye na chama hicho. Hilo lipo kikatiba. Kingine ni kumwacha Rais ambaye ni mwenyekiti wao, agombee muhula wa pili wa urais bila kupingwa.
Sasa, ikiwa Chongolo atakuwa amesulubishwa na makundi ya urais, je, shabaha ni mwaka 2025? Kama ndivyo, je, kuna watu ndani ya CCM wamejiandaa kumpinga Rais Samia kwenye mbio za urais Uchaguzi Mkuu ujao? Ni CCM gani itakuwa inatengenezwa?
Nani ajaye?
Kutoka jina moja hadi jingine, miongoni mwa wanaotajwa kufaa kushika ukatibu mkuu baada ya Chongolo, muhimu ni kujiuliza CCM kwa sasa wanahitaji mtendaji mkuu wa aina gani?
Kwanza nafasi ya Katibu Mkuu imechafuliwa. Katibu Mkuu CCM ajaye anapaswa kuwa na hadhi ya kurejesha heshima ya cheo hicho. Atakapotangazwa, kabla hajafanya kazi yoyote, jina lake liwe linatosha kufukia mashimo yaliyoachwa.
Chongolo akiwa Katibu Mkuu CCM, amefanya kazi na makatibu watatu wa idara ya itikadi na uenezi. Kila mwaka aliingia mpya. Jicho lenye kutazama mambo kikawaida, litasema makatibu hawakutosha. Jicho la tatu litaona shida ipo kwa Katibu Mkuu.
CCM inavyofanya kazi, Mwenyekiti ni mkuu wa chama lakini Katibu Mkuu anakuwa mtendaji mkuu, ndiye mwenyekiti wa sekretarieti ambayo ni kamati tendaji ya chama. Wajumbe wa sekretarieti wanafanya kazi chini ya Katibu Mkuu.
Haiwezekani wasaidizi siku zote wawe hawafai, kiongozi awe malaika asiye na makosa. Kwa namna yoyote, mabadiliko ya kila mwaka sekretarieti ya CCM tangu Rais Samia alipokuwa Mwenyekiti, yaliashiria uongozi usiotosha wa kiongozi wa sekretarieti ambaye ni Chongolo.
Katibu Mkuu CCM ajaye anapaswa kuwa kiongozi ayakayeifanya sekretarieti itulie, ifanye kazi kwa maelewano. Hatakiwi kuwa kama Chongolo, aliyebadilisha wajumbe wa sekretarieti mara kwa mara.
Kama Chongolo kaadhibiwa kwa sababu ya makundi, basi Katibu Mkuu CCM ajaye anatakiwa awe na uwezo wa kumsaidia Mwenyekiti wa chama kuunganisha makundi yote na kuwezesha CCM izungumze lugha moja. CCM imefunikwa mitandaoni na vyama vya upinzani. Hoja nyingi hasi mitandaoni dhidi ya CCM, hazipati majibu yenye kutosheleza.
Katibu Mkuu CCM ajaye, anatakiwa kutambua udhaifu wa chama hicho mitandaoni, kazi ifanyike.