Mjadala kurefusha muda urais wazua mzozo Congo DR
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi
Muktasari:
- Kiongozi wa upinzani Congo DR, Martin Fayulu amejeruhiwa katika maandamano yanayopinga mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaodaiwa kufungua njia ya kuongeza muda wa Rais Felix Tshisekedi kubaki madarakani.
Dar es Salaam. Mvutano wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeingia katika hatua mpya baada ya Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kuanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba, hatua inayozua hofu ya kurefushwa kwa muda wa urais na kufufua mjadala mpana wa viongozi wa Afrika kutaka kubaki madarakani kwa muda mrefu.
Mvutano huo uliongezeka Ijumaa, Juni 12, 2026, baada ya upinzani kuitisha maandamano kupinga hatua hiyo mjini Kinshasa, tukio lililowalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kukabiliana na waandamanaji.
Katika machafuko hayo, kiongozi wa upinzani Martin Fayulu alijeruhiwa huku waandamanaji na makundi yanayounga mkono Serikali wakirushiana mawe, hatua iliyobadili sura ya maandamano hayo kuwa vurugu.
Maandamano hayo yalikuja siku tatu baada ya Bunge la Taifa la DRC, Juni 9, kupitisha muswada wa kuandaa kura za maoni, hatua ambayo ni sehemu muhimu ya mchakato wa kurekebisha Katiba.
Upinzani unaona hatua hiyo kama mkakati wa kuondoa kikomo cha mihula miwili ya urais kilichowekwa na Katiba, jambo ambalo linaweza kumruhusu Tshisekedi kuwania muhula mwingine baada ya kumaliza kipindi chake cha mwisho mwaka 2028.
Kwa upande wake, Chama tawala cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) tayari kimeanza kampeni ya kuhamasisha mageuzi ya Katiba, hali inayokoleza mvutano katika siasa za Taifa hilo.
Kwa upande wake, Rais Tshisekedi mwezi Mei mwaka huu alitangaza kuwa angekubali kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa tatu iwapo wananchi wangetaka hivyo.
Fayulu, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2018, nyuma ya Tshisekedi amekuwa mstari wa mbele kupinga mabadiliko hayo.
Kufuatia mapigano yaliyohusisha waandamanaji na wanaounga mkono azimio la Serikali Ijumaa, baadhi ya wafuasi wake walikimbilia makao makuu ya chama chake cha Commitment to Citizenship and Development.
Hatua hiyo ilisababisha jengo hilo kushambuliwa kwa mawe na mabomu ya maji katika vurugu hizo.
Mzozo huo unakuja wakati DRC bado inakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama, ikiwamo mapigano yanayoendelea mashariki mwa nchi na tishio la magonjwa ya mlipuko. Hata hivyo, mjadala wa kisiasa kuhusu Katiba umekuwa ukitawala ajenda ya taifa hilo.
Wachambuzi wa siasa za Afrika wanaona hali ya DRC kama sehemu ya mwenendo unaojitokeza katika baadhi ya mataifa ya bara hili ambako mabadiliko ya Katiba yamekuwa yakitumika kufungua njia ya viongozi kubaki madarakani kwa muda mrefu zaidi.
Mchambuzi wa siasa za Afrika, Dk Azaveli Lwaitama amesema utaratibu wa kubadilisha mambo ya msingi ya kisheria ni kubadili dira ya nchi, akisisitiza kuwa ni lazima yahusishe wananchi kwa ukamilifu ili kuepusha mizozo inayoonekana kwa mataifa mengi.
“Katiba ni kama dira, cha msingi hapa ni wananchi wanashirikishwa kwa kiasi gani. Maana watu wamekubaliana baadaye anaibuka mtu anapeleka bungeni kifungu kibadilike.
Wananchi wametunga katiba, kiongozi anatakiwa kukaa muda uliopangwa lakini kiongozi anaamua tu anaandaa muswada kupitia bungeni abadili utaratibu, hapo matatizo yanatokea,” amesema.
Aamefafanua kuwa viongozi wengi wanaobadilisha katiba kirahisi ili wadumu madarakani wanahusishwa na kuingia katika nafasi hizo kwa njiia zinazotiliwa shaka kidemokrasia, hivyo hufanya hivyo ili kujiimarisha kudumu madfarakani.
Mjadala huo unaendelea kuzua migawanyiko ya kisiasa, maandamano na wakati mwingine machafuko katika nchi mbalimbali za Afrika, huku ukitoa funzo kuwa mapambano ya kung'ang'ania madaraka yanaweza kuzidisha migogoro ya kisiasa na kudhoofisha taasisi za kidemokrasia.
Kwa sasa, DRC inaonekana kusimama katika njia panda. Serikali inasisitiza kuwa mabadiliko ya Katiba ni haki ya wananchi kuamua mustakabali wao, lakini upinzani unaona mchakato huo kama jaribio la kubadili kanuni za mchezo wa kisiasa ili kumpa Rais Tshisekedi nafasi ya kuendelea kubaki madarakani.
Hali hiyo imeifanya nchi hiyo kuingia tena kwenye orodha ya mataifa ya Afrika yanayokabiliwa na mivutano mikubwa inayochochewa na mjadala wa muda wa viongozi kukaa madarakani, ambayo wachambuzi wanasema inachangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa taasisi za Serikali zikiwemo Bunge na Mahakama.
Mchambuzi wa siasa na utawala bora, Dk Richard Mbunda amesema shida za nchi nyingi za Afrika hazina taasisi imara, za kueleweka ikiwemo mahakama, bunge na taasisi ndindodo kama Tume ya Uchaguzi, Ofisi ya msajiri wa vyama vya siasa na Tume ya utawala bora.
“Taasisi hizi zikiwa imara mambo haya yatakoma. Madaraka ni matamu sana, mtu akikaa pale anataka kukaa milele, wapo waliofanikiwa wakiwemo Museven (Yoweri), Mugabe (Robert), Kagame (Paul) na wengine lakini tumeendelea kuona mivutano na migogoro,” amesema.
Ameonya kuwa hata kwa waliofanikiwa kufanya mageuzi na kudumu madarakani, mwisho wa siku mambo haya yamekuwa yakiibua migogoro na machafuko kwenye nchi nyingi zinazopitia hatua hiyo.