Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MNEC Mbeya awavaa Chadema kumjadili Wasira, wao wajibu

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela akisoma Biblia kabla ya kikao chake cha dharura na wanachama na wafuasi wa chama hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.



Muktasari:

  • Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale amesema wanazo hoja nyingi na hawana muda wa kumjadili mtu

Mbeya. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Taifa (MNEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amewataka makada wa Chadema kujibu hoja za Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Stephen Wasira badala ya kumjadili.

Akizungumza leo Februari 16 2025 kwenye ziara yake maalumu aliyoitumia kukabidhi zaidi ya Sh30 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za CCM katika kata 31 za Wilaya ya Mbeya, Mwaselela amesema furaha ya chama hicho ni kuona uwapo wa vyama vya upinzani vyenye kujibu hoja na si kumjadili mtu.

"Siasa ni hoja, tukianza kumjadili mtu binafsi hatutafika, CCM inafurahia kuona vyama vya upinzani vyenye ushindani, waje watuambie tumekosea tuseme hatujakosea, waseme hatufanya hiki, tuje kuwaonesha ila hii ya kuparamiana hatutafika," amesema Mwaselela.

Amesema chama hicho kinafurahia kuwapo kwa vyama vya upinzani lakini vyenye kujenga hoja badala ya kumjadili mtu binafsi akieleza kuwa kwa sasa wameshindwa kujibu hoja za Wasira badala yake wameanza kumjadili.

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale akijibu hoja ya kumjadili Wasira alipozungumza na Mwananchi amesema wanazo hoja nyingi na hawana muda wa kumjadili Wasira.

"Kwa sasa asilimia kubwa ya nguvu katika siasa ni vijana, sasa iweje ajadiliwe huyo Makamu Mwenyekiti Wasira?” amesema Mbeyale.

Wanachama na wafuasi wa CCM wakishiriki kikao cha dharura cha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela.

Katika hatua nyingine, Mwaselela amewaonya wana CCM wanawachafua wenzao, akisema anayo orodha ya baadhi ya makada wanaotumia nguvu kubwa kufanya hivyo, akisema atapambana nao.

"Huu ni wakati wa kushikamana, lakini kuna watu wanachafuana na kuharibiana,  majina yao ninayo na niwahakikishie nitapambana nao, tujikite kuzungumza changamoto za wananchi tuwe viongozi wa mfano wa kukimbiliwa na siyo kukimbiwa na wananchi," amesema Mwaselela.

MNEC huyo ameongeza kuwa Sh30 milioni alizotoa Mbeya Vijijini ni sehemu ya hamasa katika kujenga ofisi za chama akieleza kuwa mkakati wake kufikia Julai, 2026 kata zote za Mkoa wa Mbeya ziwe na ofisi zao za kisasa.

"Wengine watauliza kwa nini nimeanzia Mbeya Vijijini, huku ni nyumbani na ibada njema huanzia nyumbani, lakini pia mimi ni mfanyabiashara, hivyo ninapopata chochote nachangia chama change," amesema Mwaselela.

Mwenyekiti wa CCM Mbeya Vijijini, Akimu Mwalupindi amesema mchango wa MNEC huyo usitafsiriwe kama sehemu ya kuomba ujumbe, udiwani au ubunge bali ni katika harakati za kukipa heshima chama.

Amesema mchango wa Sh700,000 kwa kila kata aliochangia MNEC huyo, utasaidia kuanza au kumaliza ujenzi wa ofisi za CCM katika maeneo hayo, akiomba wadau wengine kuhamasika.

"Mtu asitafsiri vinginevyo, huu mchango siyo wa kuomba ujumbe, udiwani au ubunge, tushukuru kwa sapoti hii na iwe chachu kwa wadau wengine kuhamasika kutusapoti ili tukijenge pamoja chama," amesema Mwalupindi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wilayani humo, William Simwali amemuomba MNEC huyo kuwafikishia maombi ya kuufanya Mji wa Mbalizi kuwa Halmashauri ya Mji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

"MNEC tunaomba katika vikao vyenu Taifa, tunaomba utufikishie maombi, huu mji umekua, isitoshe Mbeya DC ni kubwa mno, Mbalizi iwe halmashauri ya mji isaidie wananchi kupata huduma," amesema Simwali.