Mnyika atoa maagizo nafasi za waliohama Chadema

Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika akihutubia wananchi wa mjini Bariadi mkoa wa Simiyu katika viwanja vya Salunda. Picha na Samwel Mwanga
Muktasari:
- Mnyika ameitaka Sekretarieti ya Chadema na viongozi wa mikoa na wilaya, kuandaa utaratibu wa haraka wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa mujibu wa katiba ya chama, akisisitiza umuhimu wa kuitisha vikao maalumu kwa ajili ya kufanya tathmini na kupendekeza viongozi wapya.
Simiyu. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ameagiza kujazwa kwa haraka nafasi zote za uongozi zilizoachwa wazi na wanachama waliokihama chama hicho au kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Mnyika, hatua hiyo ni ya msingi katika kuimarisha muundo wa chama, kuboresha uendeshaji wa shughuli zake na kuendeleza harakati za kisiasa katika ngazi zote za uongozi.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana, Mei 15, 2025, katika viwanja vya Salunda, Bariadi mkoani Simiyu, Mnyika alisema kuwa hatua hiyo inalenga kukijenga upya chama kwa kuziba mapengo yaliyosababishwa na viongozi waliotangaza kujiondoa au kujichukulia hatua za kinidhamu, na hivyo kurejesha kasi na ufanisi wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ni lazima tuzibe mapengo haya haraka kupitia utaratibu wa kikatiba ili kuhakikisha chama kinaendelea kusimama imara na kutimiza majukumu yake kwa wananchi,” alisisitiza Mnyika.
Mnyika alisema kuwa hatua hiyo ni ya dharura na muhimu katika kulijenga upya chama, hasa baada ya baadhi ya viongozi na wanachama kujiondoa au kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka misimamo ya chama, ikiwemo kampeni yao ya kitaifa ya "No Reforms, No Election."
“Sekretarieti ya chama na viongozi wa mikoa na wilaya waandae utaratibu wa haraka wa kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa Katiba na kanuni zetu. Lazima tufanye tathmini ya kina na kupendekeza viongozi wapya kupitia vikao halali vya chama,” alisisitiza Mnyika.
Alisema ombwe la kiuongozi lililojitokeza katika baadhi ya maeneo limeathiri shughuli za kiutawala, kisiasa na uhamasishaji wa wanachama, jambo ambalo linaweza kudhoofisha harakati za chama ikiwa halitashughulikiwa mapema.
Mnyika alieleza kuwa kujaza nafasi hizo ni hatua ya msingi si tu kwa ajili ya utendaji wa chama, bali pia kuhakikisha kuwa Chadema inaendelea kuwa sauti madhubuti ya upinzani, na chombo cha kweli cha kupigania mabadiliko ya kisiasa nchini.
Katika mkutano huo, Mnyika alisisitiza kuwa msimamo wa Chadema kuhusu kutoshiriki uchaguzi bila kufanyika kwa marekebisho ya msingi ya mfumo wa uchaguzi uko pale pale.
Alisema mabadiliko hayo ni pamoja na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, kuruhusiwa kwa wagombea binafsi, na kuwepo kwa fursa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani.
“Huu ni msimamo wa chama kupitia vikao halali na tayari tumeuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Wananchi wanatuunga mkono kwa wingi katika mikutano yetu, jambo linalotupa moyo kuendelea kuelimisha na kushinikiza mabadiliko haya ya msingi,” alisema.
Alifafanua kuwa kutosaini kanuni mpya za maadili za uchaguzi kuliwafanya kuondolewa rasmi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 pamoja na chaguzi ndogo zote kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, lakini bado chama kiko imara na kinaendelea na kampeni zake za kitaifa.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Kanda ya Serengeti, Rosemary Kirigini, alisema kuwa uungwaji mkono wa wananchi katika mikutano yao umekuwa mkubwa kiasi cha kuilazimu Serikali kutumia vyombo vya dola kuwahujumu.
“Wananchi wanaonesha mshikamano mkubwa nasi. Serikali imejaribu kutuzuia kufanya mikutano kwa kutunyima viwanja, kama ilivyotokea hapa Simiyu. Lakini tumekuja huku nje ya mji na bado mmekuja kwa wingi. Hii inaonyesha nguvu ya wananchi,” amesema Kirigini.
Aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuitisha meza ya mazungumzo ya kitaifa ili kuweka mazingira ya uchaguzi huru na wa haki, akisisitiza kuwa Chadema haikusudii kususia uchaguzi, bali inahitaji mazingira bora ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Godbless Lema, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amesema kuwa wale wanaojiondoa katika chama wasiwafanye wanachama waliobaki kukata tamaa, kwani kuondoka kwao ni sehemu ya mikakati ya mahasimu wa kisiasa wa chama hicho.
“Wanaoondoka ni sehemu ya mkakati wa serikali na CCM kutaka kukidhoofisha chama chetu. Lakini hawatafanikiwa kwa sababu Chadema iko mioyoni mwa Watanzania. Wengine hawawezi kutununua sisi hatufiki bei. Tutaendelea kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati hadi haki itendeke,” amesema Lema.
Mkutano huo wa Bariadi ni sehemu ya mikutano ya kitaifa ya Chadema inayolenga kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini, huku pia ukitumika kama jukwaa la kushirikisha wananchi katika maamuzi na misimamo ya chama hicho kikuu cha upinzani.