Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Bajeti ya kinyumenyume



Sijui ni kwa nini ikifika siku ya kusomwa bajeti ya Serikali, mawazo yangu yanaangukia Mei Mosi.

Nadhani ni woga unaotufanya tuzione siku hizi zikiakisiana. Kwa namna moja au ingine, tunayaona matukio haya yakiwa yanafanana kama watoto mapacha.

Nauona moyo wa Mtanzania wa kawaida ukimdundia shingoni kama ilivyo kwangu. Ni kama vile unaotaka kuchomokea mdomoni.

Tatizo ni kwamba kila jicho la Mtanzania lipo kwenye mfuko wa mwenzie. Siku ya Mei Mosi kila mmoja anasubiri kusikia mshahara ukipandishwa.

Utaona ajabu hata mwizi wa mifukoni anashangilia kupanda kwa mshahara. Ikitokea mshahara ukapandishwa, upesi wasafirishaji watapandisha gharama za nauli na wafanyabiashara wanapandisha bei za bidhaa muhimu.

Hilo hutokea si kwa kusudi la kukomoana, bali kila mmoja wao yupo hoi kwa umasikini. Kila jicho lipo kisogoni kwa aliye mbele yake: unayemdai naye anamdai wa mbele yake, hivyo anasubiri alipwe ili akulipe. Ikitokea mmoja tu kwenye mzunguko mzima akaongopa, anatengeneza msururu wa waongo nyuma yake.

Lakini hela nayo ina maajabu yake. Unapolipwa ndipo unapogundua kuwa umeshautumia mshahara wako kabla hujaupokea. Wakati huohuo, ubongo wako utamkumbusha kuwa umepoteza miadi ya daktari wako mara mbili.

Pia ulikosa kunywa maziwa tangu mwezi wa jana. Vilevile kwamba hujakula nyama katika mwezi mzima, na kwamba mavazi yako yameshapoteza nuru kwa uchakavu.

Hii ndio maana ya hela kupiga kelele. Bajeti ya Serikali ipo kama hivyo. Kwanza mnaangalia kwenye viroba visivyo na chakula. Mkitazama mapato, mnagundua kuwa hayatoshi hata kulipa madeni.

Huko mitaani kunanuka shida, wagonjwa wanaongezeka na miundombinu imezidi kumong’onyoka. Badala ya kuketi na kupanga mikakati ya mwaka huo, mnachutama kukuna vichwa ni wapi mtakopa mkawalipe wadai sugu, ili muwakope tena.

Mwaka huu Bajeti ya Serikali imepatia kwa kuongeza makali katika bidhaa zisizo za lazima kama kucha, nywele na kope bandia. Sio mbaya hata kwenye pombe na sigara.

Starehe zinaleta athari zinapoongezeka, hivyo ni lazima kuzipunguza ili kupunguza athari hizo. Ni sawa tu kuongeza tozo za mabomba ya shisha (kama ni halali kwa matumizi) ili watoto wetu wasije wakaangamia.

Lakini sijaiona bajeti ikijikita kupunguza makali kwa Mtanzania wa kawaida. Baada ya mtikisiko wa kupanda ghafla kwa gharama za maisha, hasa baada ya kiki za vita ya mafuta, mwananchi huyu analazimika kujitafuta upya.

Mpaka sasa ameshapoteza dira ya mzunguko mzima wa maisha yake. Mafuta yakipanda ni msala mkubwa, kwani yenyewe pia husafirishwa kwa mafuta.

Gharama za maisha hupanda katika mtindo wa Kalume-kenge. Bingwa alighairi kwenda shuleni. Baba akamtuma mbwa amlume, lakini naye akagoma.

Akaituma fimbo kumchapa mbwa, ikagoma. Akauambia moto uichome bakora, moto ukakataa.

Akayaambia maji yauzime moto, maji yakapinga amri. Akamwamuru mbuzi ayanywe yale maji lakini mbuzi hakutii. Akamuomba sultani mchinje mbuzi, sultani akakubali!

Mpaka mbuzi alipochinjwa ndipo alipoyanywa maji. Maji yaliponywewa yakauzima moto, moto ulipozimwa ukaichoma fimbo, ikamchapa mbwa, akamluma Kalume-kenge naye akaenda shuleni. Ni jambo lisilowezekana katika macho ya nyama, labda lingegeuzwa kinyumenyume.

Kwamba Kalume aende shule, mbwa amlume, fimbo imchape mbwa, moto uichome fimbo, maji yauzime moto, mbuzi anywe maji kisha Sultani amchinje.

Bajeti ya shilingi trilioni 62 kukutana na deni la shilingi trilioni 114, ni sawa na timu ya Kachaso FC ya mtaani Buza ikienda kupambana na Arsenal, mabingwa wa EPL.

Kachaso wataingia uwanjani wakiwa na wazo la kupenya kwenye tundu la sindano, tena “lisilowezekana kwa wanadamu linawezekana kwa Mungu”.

Katika wakati huu wa msuguano wa Marekani dhidi ya Iran, hadithi ya Kalume inajirudia kinyumenyume. Mmarekani alimtisha na akamtumia makombora Muiran, Iran wakaifunga njia ya mafuta ya baharini.

Mafuta yakaadimika na kupanda bei. Gharama za usafiri na usafirishaji zikapanda. Bei za bidhaa zikapanda, maisha ya Mtanzania yakawa magumu.

Kwa nini maisha yamekuwa magumu? Ni kwa sababu tangu awali Mtanzania wa kawaida alikuwa akipambania mlo wa kila siku moja. Hakuwa na akiba ya dharura.

Wasafirishaji walipopandishiwa bei ya mafuta, wakapandisha nauli kwa baraka za Latra. Hata yule muuza chakula aliongeza bei kupambana na gharama za usafirishaji. Mfanyabiashara ana ulinzi wa “soko huria”. Huyu Mtanzania tunayemsema, hakuongezewa mshahara wala posho ya nauli na chakula.

Kinakachoendelea ni mwananchi wa kipato cha chini kushindwa kununua kama zamani.

Mkate na maziwa vimewekwa kwenye orodha ya bidhaa za ziada au anasa. Amepunguza milo, kitu kinachosababisha biashara ndogondogo kukosa wateja.

Kwa kifupi, mtu mwenye kipato kikubwa anaweza kubeba ongezeko la bei kwa urahisi zaidi.

Lakini kwa mtu wa kipato cha chini ambaye tayari anatumia sehemu kubwa ya mshahara wake kununua chakula, kulipa nauli na kodi ya nyumba, hata ongezeko dogo la bei linaweza kuathiri sana maisha yake ya kila siku.

Ndiyo maana tunataka viongozi watakaotupitisha kwenye ujamaa wa Kichina. Tusimtegemee mtu kwa jambo lolote, zaidi ya kuwatengeneza wawe wateja wetu.