Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Tusiwashe moto tusioweza kuuzima

Hata kama ni kweli kuna maisha baada ya maisha haya, lakini maisha tunayoishi si mazoezi ya maisha hayo yatakayofuata. Maisha ni imani, lakini tofauti ya imani na maisha ni kwamba imani ni usadiki wa jambo hata kama huna hakika nalo. Mtu anaweza kuamini ushirikina hata kama hajauthibitisha, na anaweza kuamini mizimu pamoja na kwamba hajawahi kushuhudia uwepo wake.

Mara nyingi watu wenye ushawishi wameweza kujenga na kubomoa imani za waumini. Tukiacha Mitume na Manabii ambao tumeambiwa kuwa ndio walioshuhudia mambo makubwa moja kwa moja, sisi tulioambiwa habari hizo tukajenga uwezo wa kuwaaminisha wenzetu kwamba nasi tunaweza. Tunawaondoa kwenye imani za kale na kuwaleta kwenye imani za kisasa zenye utofauti mkubwa na zile za mapokeo.

Imani za kale zilitufundisha kutokuhangaikia mambo ya kidunia. Tumweke Mwenyezi Mungu mbele yetu, na mengine yote yatakuja kwa ziada. Maana yake ni nini? Ni kuishi kwenye taratibu za kiimani kama kufanya kazi na kuridhika na kipato, kutokuuana, kutofanya ngono zembe kama kuzini au kumtamani mume au mke asiye wako na kadhalika. Lakini waja wakaanza kuharibikiwa mdogomdogo baada ya “wabunifu” kuja na suluhisho la tamaa za binadamu.

Wakati huo watu walishaanza kuchoka kutumia akili zao za kawaida. Waliona mambo yakienda ndivyo sivyo pamoja na kwamba walikuwa wakiishi kiimani. Walipigwa na watu waliowaahidi kuwatatulia matatizo yao ndani ya jamii, lakini wananchi kwa shida zao wakajikuta wakiongozwa na wapigaji hao. Yule waliyemlea hadi akakua na kumwita “Mheshimiwa” alizibadili shida zao kuwa mtaji wake. Akajenga maghorofa na kujinunulia magari ya kifahari kwa kodi zao. Lakini mwishoni akawafanya wananchi kuwa misukule yake; akitangaza shida misukule ililazimika kuzitatua. Hapo nina maana ya rushwa na ufisadi.

Wahanga walipotafuta utetezi wakajikuta wakiingia mikononi mwa viongozi wa dini. Kumbuka hata enzi za biashara ya utumwa tuliingizwa kwenye mfumo kwa mtindo kama huo. Walianza kuja wapelelezi, kisha madalali na hatimaye tukaingizwa utumwani. Mambo yalipokuwa mabaya wakaja na suluhisho la kiimani.

Kwenye msafara wa mamba kenge hawakosekani. Walikuwepo mashehe na wachungaji walionyoosha mstari. Walituambia kwamba dini haitaki makandokando, ukiitaka inakubidi uache swaga zote na ubebe msalaba wako. Lakini kwa bahati mbaya wahuni wakajiweka hapo na kuwaaminisha watu wote kuwa wao nao ni sehemu ya mashehe na wachungaji, na ndio shubiri ya maradhi ya waumini, kwani hao waliowatangulia waliyashindwa.

Tatizo la imani ni kubwa. Mtu akishaamini anaweza kupuuza makandokando yote, akashikilia imani anayolishwa. Kuna watu hawaamini hospitali wala shule kwa sababu wameaminishwa hivyo. Wapo waumini walioaminishwa kutajirika kwa maombi bila kufanya kazi, wakati uhalisia unaonesha kuwa kazi ndio msingi wa maisha.

Pamoja na Serikali kutoingilia moja kwa moja shughuli za kiimani, uangalifu mkubwa unahitajika ili kuwanusuru watu wetu. Hivi majuzi wenzetu Wakenya wameanza mapambano dhidi ya imani potofu zisizo na tija. Wameanza kuwakemea viongozi wa kiimani wanaowapotosha wananchi kwa faida zao binafsi. Kwa mfano yule aliyewaamuru waumini kufunga hadi kufa.

Haya yalishawahi kutokea nchini Uganda baada ya mchungaji feki kuwaingiza waumini kwenye mikataba ya kishetani, kuwapiga ukwasi wao na kuwachoma moto baada ya kuwadanganya kuwa hiyo ndio njia yao ya kwenda peponi. Hivi karibuni aliibuka mchungaji kule Mexico aliyewapiga mamia ya matajiri baada ya kuwatangazia “mnada wa viwanja vya mbinguni”! Ama kweli dunia ina mambo.

Kuna mambo ya wazi kabisa yanayoendelea hapa nchini, ambapo viongozi wa imani wanazuga kutatua matatizo ya waumini kwa kugawa shilingi elfu tano tano barabarani, lakini wakati huohuo wakiwapangisha foleni kwa tozo ya ada inayokadiriwa kufikia shilingi laki tano kwa kila kichwa. Kwa kuwa waumini hao wameshaaminishwa “kupokea utajiri”, imewapelekea kuingia kwenye mikopo ya hatari kama “kausha damu”.

Serikali yetu haina dini pamoja na kwamba wananchi wanaruhusiwa kufuata imani walizozichagua. Inawezekana kabisa Serikali ikakusanya kodi nyingi kwenye taasisi ambazo zinafanya madudu kwenye jamii, zikiwemo baadhi ya dini. Lakini mafundisho ya viongozi wa kiimani kuwa kuna kupokea bila kufanya kazi yanazidi kushusha ustawi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kiujumla.

Wapigaji hawa wanatumia kigezo cha uhuru wa kuabudu kujitengenezea njia za kuwadhulumu wananchi. Kutokuwepo kwa mamlaka zenye kudhibiti shughuli zao zisizo halali kumekuwa chachu ya wao kutembea vifua mbele bila kubanwa na sheria. Afya ya akili imezidi kudorora miongoni mwa Watanzania, na uchumi wa Taifa unazidi kutetereka kutokana na mambo haya.

Nashauri elimu mbadala isisitizwe ili kuirudisha jamii kwenye mstari. Watu waelewe kuwa hakuna kipato bila kazi, ilinenwa: “Asiyefanya kazi na asile”. Waeleweshwe kuwa imani bila matendo haina faida hata inapofundishwa na wataalamu nguli. Serikali iwe macho na wadanganyifu, hasa wale wanaoyaanzisha matatizo ndani ya jamii na kuongopea kuyatatua. Tusiuache moto ukolee kisha tuhangaike kuuzima.