Operesheni Majimaji ya ACT- Wazalendo kuanza leo Kigoma

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu
Muktasari:
- Operesheni ya Majimaji ya Chama cha ACT Wazalendo inaanza rasmi katika mikoa 13, ikihusisha viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Kigoma. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, leo Jumanne Julai 1, 2025 anaanza ziara yake ya siku 15 katika mikoa saba nchini, ikiwa ni mwanzo wa Operesheni Majimaji ya chama hicho.
Operesheni hiyo pamoja na mambo mengine, inalenga kutoa elimu na kuwahamasisha wanachama wa chama hicho na wananchi, kulinda kura wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katika ziara hiyo inayoanzia mkoani Kigoma, Dorothy ataambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa na mikoa wa chama hicho, kusambaza ajenda hiyo ikiwa ni rasharasha za kuelekea uchaguzi mkuu.
Ziara hiyo inaanza leo Jumanne Julai 1, 2025 katika Mkoa wa Kigoma kwa mapokezi ya viongozi, vikao vya ndani na mkutano wa hadhara.
Sambamba na Dorothy, viongozi wengine atakaoambatana nao ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Issihaka Mchinjita, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho taifa, Abdul Nondo na Naibu Mwenezi, Shangwe Ayo.
Viongozi wengine ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Kiza Mayeye, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Peter Madeleka na Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Emmanuel Ntobi.
Katika ziara hiyo, viongozi hao watatembelea mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Tanga na kumalizia Dar es Salaam ambalo kote itafanyika mikutano ya hadhara.
Wakati Dorothy akiendelea na ziara katika mikoa hiyo, kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe naye ataanza ziara kama hiyo kesho Jumatano Julai 2, 2025 katika mikoa ya Tabora, Katavi, Mbeya, Mtwara, Lindi na Pwani.
Ziara za viongozi hao zinatarajiwa kukoma Julai 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam, itakakofanyika mikutano ya hadhara Ukonga na Segerea.