Prime
Sababu Mchungaji Malisa kufutiwa kesi ya uhaini
Dar es Salaam. Mchungaji Godfrey Malisa aliyekuwa anakabiliwa na kesi mbili za jinai ikiwamo ya uhaini, yuko huru kwa masharti, baada ya kuachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, iliyokuwa ikisikilisha kesi hizo.
Kesi ya uhaini namba 28333 ya 2025 iliondolewa mahakamani Mei 19, 2026 baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kuiondoa kesi hiyo chini ya kifungu 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) marejeo ya 2023.
Wakili Deogratious Matata aliyekuwa anamtetea Mchungaji Malisa amelithibitishia Gazeti la Mwananchi Mei 20, 2026 kuwa, DPP amemfutia kesi ya uhaini mteja wake, lakini akapatikana na hatia katika kosa moja la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Hiyo ni baada ya Mei 19,2026, DPP kuwasilisha maelezo kuwa, hana nia ya kuendelea na kesi hiyo na ndipo Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama akaifuta kesi hiyo iliyofunguliwa Desemba 2, 2025 na kumwachia huru kutoka gerezani.
Chini ya kifungu hicho, katika kesi yoyote ya jinai na katika hatua yoyote kabla yake hukumu, DPP anaweza kuingiza Nolle Prosequi, ama kwa kusema mahakamani au kwa maandishi kwamba, Jamhuri haina nia ya kuendelea na shauri lililopo kortini.
Katika kesi ya uhaini, Mchungaji Malisa alishitakiwa chini ya Kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali hapa nchini Tanzania.
Kulingana na hati ya mashitaka, ilikuwa inadaiwa kuwa, Novemba 16, 2025 huko eneo la Miembeni katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, akiwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, alitenda kosa hilo la uhaini.
Jamhuri ilidai kuwa, alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kushiriki kusanyiko lisilo halali kwa lengo la kumtisha mtendaji wa Serikali ya Tanzania na alidhihirisha nia hiyo kwa kitendo chake cha kutamka na kuchapisha maneno yafuatayo.
“Samia Suluhu Hassan…Kabla ya kufika tarehe 9 Desemba uwe umekwishajiuzulu. Kama utang’ang’ania madaraka itakapofika tarehe 9 Desemba kutakuwa na maandamano ambayo hayajawahi kutoka katika Bara la Afrika.”
Mchungaji Malisa alidaiwa kunukuliwa akisema: “Lengo la maandamano ni kumuondoa Samia Suluhu Hassan madarakani na maandamano hayo yatakuwa ni maandamano ya muendelezo mpaka utakapotoka madarakani.”
Atiwa hatiani makosa ya mtandao
Hata hivyo, Mchungaji Malisa aliyekuwa ni Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kufukuzwa uanachama baada ya kupinga uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais 2025, ametiwa hatiani katika kosa lingine.
Kesi hiyo ni namba 28411 ya 2025 ilikuwa na makosa mawili; Hakimu Mkama aliyekuwa akiisikiliza alimtia hatiani katika kosa la kwanza la kutoa taarifa za uongo mtandaoni na kuhamasisha kutendwa kwa makosa hayo.
Katika hukumu hiyo aliyoitoa Mei 12, 2026 ( kifungo cha nje kwa kosa la mtandao).
Hakimu Mkama alisema upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa, alitenda kosa hilo na kumwachia kwa masharti ya kutotenda kosa lolote la jinai kwa miezi 12.
Halikadhalika katika masharti hayo, Hakimu Mkama alimwamuru Mchungaji Malisa kuwa katika kipindi hicho cha miezi 12, anatakiwa kujiepusha na matumizi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp, FaceBook na Instagram kwa nia mbaya.
Hiyo ni pamoja na kutotumia mitandao hiyo kutunga, kuwasiliana, kushiriki na au kuchapisha hadithi, makala, taarifa na maelezo ya sauti (voice note) yanayokusudiwa kupotosha, kuudhi au kusababisha chuki kwa umma kwa jumla.
Kuhusu simu yake ya kiganjani aina ya Infinix Note 10 na kompyuta mpakato (Laptop) zilizokamatwa na kutolewa na kupokewa mahakamani kama kielelezo PE1, Hakimu Mkama ameamuru vitu hivyo virejeshwe kwa Mchungaji Malisa.
Baada ya kutiwa hatiani na kabla ya kutolewa kwa adhabu, Malisa aliwasilisha maombolezo yake (mitigation) akiomba Mahakama izingatie muda aliokaa gerezani, ana umri wa miaka 72, ni mgonjwa na mkosaji wa mara ya kwanza.
Mahakama ilimuona hana hatia katika kosa la pili la kuhamasisha umma kutenda kosa la mkusanyiko usio halali au unlawfull assembly kinyume na kifungu 390 na 35 cha Kanuni ya Adhabu.
Katika kosa la kwanza, upande wa mashitaka ulidai kuwa, Mchungaji Malisa alitenda kosa hilo Novemba 15, 2025 huko Miembeni katika Wilaya ya Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya YouTube yenye jina Godfrey Malisa.
Hati ya mashitaka iliyofunguliwa Novemba 3, 2025 inanukuu maneno aliyoyachapisha kuwa amesema: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.”
Upande wa Jamhuri ulidai pia alichapisha maneno hayo akijua fika kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa Watanzania.
Katika kosa la pili, anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na Kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15, 2025 huko Miembeni Wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.
Mchungaji Malisa ni nani
Mchungaji Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alipogombea ubunge Moshi Mjini kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) na mwaka 2015, aligombea urais kupitia CCK na baadaye kugombea uspika.
Mwaka 2018 aligombea ubunge Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa TLP na mwaka 2020 aligombea ubunge Moshi Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi na baada ya uchaguzi ule alijiunga na CCM hadi mwaka 2025 alipotimuliwa.
Mwaka 2022 Malisa alijitosa kuchukua fomu na kuwa miongoni mwa makada tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Hata hivyo, Februari 10, 2025 Mchungaji Malisa ambaye ni mwanazuoni mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kupinga uamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Uamuzi wa kumfukuza uanachama ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel akiegemea uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.
“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Januari 19,2025,”alieleza Mollel.
Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja Katiba jambo ambalo si la kweli.
Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kujaribu kufungua kesi mahakamani ambazo hata hivyo hakufanikiwa na alihamia katika mitandao ya kijamii akiendelea kupinga uteuzi huo.