Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia anastahili shukrani hotuba ya kulivunja Bunge la 12

Nilisikiliza hotuba ya Rais Samia aliyotoa bungeni ile siku alipozindua rasmi utawala wake wa Awamu ya Sita, na pia nikaisikiliza tena juzi Ijumaa alipolivunja Bunge kuhitimisha nusu ya kwanza ya awamu yake. Nikitumia tafakuri ya kina na uchambuzi wa makini, kiukweli kabisa Rais Samia anastahili pongezi na shukrani zake stahiki, kwa maneno mengine, apewe maua yake!

Kuna maneno viongozi huyasema kwa sababu yameandikwa na wasaidizi wao kwenye hotuba na kuna maneno yanayotoka moyoni mwao. Rais Samia alizungumza kwa zaidi ya saa mbili, lakini kwa muhtasari nitagusia yale machache ambayo kwa maoni yangu yalionyesha utu na ukomavu wa uongozi wake, hasa ule upole na moyo wa shukrani.

Niliguswa sana na namna alivyoonyesha shukrani za dhati kwa wapinzani, kwa waliomkosoa, kwa waandishi wa habari na hadi kwa familia yake, akimtaja waziwazi mpendwa wake.

Ni nadra sana kwa marais wetu kuwasema hadharani wanafamilia zao kwa namna ya shukrani.

Kwa mara ya kwanza nimesikia Rais Samia akiwaambia wapinzani kwamba wote ni Watanzania na tunajenga nyumba moja, hatuna sababu ya kugombea fito.

Hili ni jambo lenye faraja kubwa kwa wapinzani na ishara ya siasa zenye ustaarabu na maridhiano.

Vilevile, kwa mara ya kwanza nimesikia Rais akiwashukuru wakosoaji wake kwa sababu ukosoaji unamsaidia kurekebisha na kujenga. Hili linaonyesha kuwa wakati mwingine malalamiko juu ya "watu wasiojulikana" wanaowabughudhi wakosoaji hayamhusu yeye binafsi, bali watu wengine wenye nia tofauti.

Sisi waandishi wa habari pia tumeshukuriwa rasmi kwa kazi yetu. Ni jambo dogo lakini lina maana sana, hakuna kinachotia moyo kama mtu kuthamini na kushukuru kazi yako. Asante sana Rais Samia kwa kutambua mchango wa mhimili wa nne.

Hata hivyo, tunapaswa kusema wazi kuwa ili tuwe na siasa za kisasa na za uwajibikaji, viongozi wanapaswa kuandaliwa hotuba zenye malengo ya maalum yanayopimika na yanayoweza kufikiwa huku yakiwa na uhalisia na muda maalum.

Wasaidizi wa viongozi wanapaswa kuwasaidia kuahidi kwa uwazi na kupanga malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Hii itaturahisishia wananchi na wanahabari kufanya tathmini, kwamba kiongozi alipoingia aliahidi nini, ametimiza nini na amekwama wapi. Hata kwenye ilani ya uchaguzi, lazima tuangalie ni kwa kiasi gani yale yaliyoahidiwa katika ilani iliyopita yametekelezwa kabla ya kuidhinisha ilani mpya.

Mfano mzuri ni suala la Katiba Mpya. Tuliahidiwa mchakato ukamilishwe, tukapiga kura tukiamini hivyo, lakini baadaye tukasikia ‘katiba sio kipaumbele changu’ na ahadi hiyo ikafa kifo cha mende.

Tukiingia kwenye uchaguzi mpya, ilani mpya haikuzungumzia tena Katiba. Hapa tunahitaji uwajibikaji na muendelezo wa ahadi.

Vyombo vya habari navyo vina wajibu mkubwa. Tunapaswa kuandika kwa mtindo wa kisasa wa ‘data journalism’ tukiweka kumbukumbu kwa uwazi.

Ahadi za kiongozi ziorodheshwe waziwazi ili zikae kwenye kumbukumbu sahihi kimaandishi. Tukifika katikati ya muhula wa uongozi wake, basi tuone kama ametimiza nusu ya alichokisema na kukiahidi. Mwisho wa muhula tuje na tathmini kamili ya alichotekeleza na alichoshindwa.

Kwa upande mwingine, Rais Samia alipokabidhiwa madaraka alikuta mipango na miradi ambayo tayari ilianza chini ya mtangulizi wake.

Tunapaswa kumpongeza kwa busara na moyo wa kuyakubali na kuyaendeleza yale yote mazuri na kisha kuongeza mapya yake.

Kwenye hotuba yake ya kwanza, alileta falsafa ya 4R. Kwenye hotuba hii ya kulivunja Bunge tulitarajia pia tupate tathmini ya 4R imefanikisha nini? Imejenga nini? Imekwama wapi?

Nihitimishe kwa kutoa wito kwamba tuwe watu wa shukrani. Unapotendewa wema, ukashukuriwa nawe toa shukrani. Tusiwe watu wa kukosa fadhila. Rais Samia amestahili kwa haya yote kupewa shukrani. Tumpe maua yake.