Prime
Sheria vyama vya siasa tatizo, Msajili atia neno
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (kushoto) akisalimiana na Katibu wa Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipofika ofisini kwake leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Wadau wamevikosoa baadhi ya vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2024, wakidai vinakandamiza uhuru wa kisiasa, huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ikisema wanaoikosoa sheria hiyo hawapendi misingi ya demokrasia.
Ukosoaji wa sheria hiyo, umejikita zaidi katika kipengele cha mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wakisema ni makubwa hasa yale ya uwezo wa kufuta chama, kuingia kwenye mikutano ya vyama na kuomba nyaraka muhimu.
Baadhi ya madai ya wadao hao si mapya, yalijitokeza hata wakati sheria yenyewe inatungwa lakini Bunge lenye wabunge wengi wa Chama cha Mapinduzi likaipitisha.
Wabunge wa vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia walidai wakati huo kuwa sheria hiyo inaleta mazingira magumu ya utendaji wa kisiasa na kuminya demokrasia ya vyama vingi nchini na imeongeza udhibiti wa Serikali kupitia ofisi ya Msajili.
Sheria inampa Msajili nguvu kubwa ya kuingilia mambo ya ndani ya vyama, ikiwa ni pamoja na kusimamisha uanachama wa mtu au kukisimamisha chama chenyewe kisifanye shughuli za kisiasa.
Pia vyama haviruhusiwi kutoa elimu ya uraia bila uratibu au kibali kutoka kwa Ofisi ya Msajili, jambo linalotajwa kuzuia uelimishaji huru wa wananchi na kuna masharti magumu kuhusu ukaguzi wa rasilimali na fedha za vyama vya siasa, ambapo kukiukwa kwake kunaweza kusababisha chama kufutwa au viongozi wake kushtakiwa
Kwa mujibu wa wadau hao, msajili hapaswi kuwa na mamlaka kwenye masuala yanayohusiana na taarifa nyeti au mchakato wa maamuzi ndani ya chama, badala yake aishie kwenye kanuni za usajili, kwa kuwa anateuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama shindani.
Hata hivyo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema pasi na usimamizi huo, ndani ya vyama vya siasa kutakuwa na hali ya kuoneana na watakaoumia ni wanachama wa vyama hivyo.
Mjadala huo unaibuka katikati ya mfululizo wa vitendo vya Ofisi ya Msajili vilivyowahi kulalamikiwa. Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuandika barua kwa baadhi ya vyama vya siasa na kutishia kuvichukulia hatua kwa madai ya kukiuka sheria.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo, ofisi ya Msajili inaangalia makosa ya vyama vya upinzani pekee na haikuwahi kuonekana ikichukua hatua dhidi ya chama tawala, licha ya historia ya makosa yaliyowahi kufanywa na wanachama wake.
Majukumu ya Msajili
Majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yameainishwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa (kifungu cha 4(5) kuwa ni kusajili vyama vya siasa, kufuatilia mchakato wa uteuzi na uchaguzi ndani ya vyama vya siasa,
Vilevile analo jukumu la kuratibu shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa, kufuatilia mapato na matumizi ya vyama vya siasa, kugawa na kufuatilia matumizi ya fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye sifa ya kupata ruzuku;
Pia, kutoa elimu ya uraia kuhusu sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili na mfumo wa demokrasia ya vyama vyingi vya siasa na kuratibu elimu ya uraia inayotolewa kwa vyama vya siasa.
Mamlaka yanapitiliza
Akizungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, Wakili katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), William Maduhu amesema Sheria ya Vyama vya Siasa imetoa mamlaka yaliyopitiliza kwa Msajili kwenye masuala ya ndani ya chama
Amesema Msajili wa vyama ameondoka kwenye majukumu yake halisi (ya usajili) na kuwa mdhibiti ndani ya vyama vya siasa na amekuwa akitoa adhabu kali kwa baadhi ya vyama pekee na vipo vinavyoonekana kupendelewa.
Wakili Maduhu amesema ofisi ya Msajili inatumika kufifisha demokrasia ndani ya vyama vya siasa na ndio chimbuko la migogoro mingi kwenye vyama vya siasa.
Kauli ya Maduhu inashabihiana na ya Dk Paul Loisulie, mwadhiri na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anayesema sheria ya vyama vya siasa haitoi demorasia kwa vyama vya siasa.
Amesema upo mgongano wa sheria na siasa ambapo baadhi ya vitu vilivyoruhusiwa kisheria vinakatwa kisiasa.
“Kuanzia kwenye Katiba hadi sheria unatolewa uhuru wa vyama vya siasa, lakini siasa inakataza. Mfano mikutano ya hadhara iliruhusiwa kisheria, lakini siasa ilikuja kukataza,” amesema.
Hata hivyo, masuala mengine yamedhibitiwa moja kwa moja kisheria, kama anavyosema Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Magabilo Masambu, kuwa kifungu cha 3(b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinampa nguvu Msajili kuathiri chaguzi za ndani ya vyama.
Pia, amesema kifungu cha 3(g) kimemgeuza Msajili kuwa mshauri wa Serikali badala ya mlezi huru wa vyama.
Aidha, amesema vifungu vya 5A (i) na 5B(i) vinatajwa kubana uhuru wa vyama kupata mafunzo, kushirikiana na taasisi za nje pamoja na kulazimisha kutoa taarifa za ndani za chama chini ya vitisho vya faini kubwa.
Pamoja na hayo, amesema sheria bado haijatoa mwanya sawa wa vyama vya siasa kufanya siasa kwa usawa, akisisitiza hilo ni eneo muhimu la kuangaliwa zaidi.
Mtazamo huo ni tofauti na anaoutoa Addo November, mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, ambaye amesema Sheria ya Vyama Siasa ni nzuri na inatoa nafasi na fursa kwa vyama vya siasa kutimiza majukumu yake, ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara kwa kufuata sheria.
“Pia, sheria imepiga marufuku kwa vyama vya siasa kuhubiri fujo au kuvunja Muungano wetu, sasa hili ni jambo zuri kama sheria yetu imetaka tuulinde Muungano ni jambo zuri,” amesema.
Amesema sheria ya vyama vya siasa ina matokeo mabaya kwa mtu anayetaka kuichezea, hasa kuondoa amani ya taifa, lakini kama mtu anayehubiri amani, sheria hiyo ni nzuri.
Sheria ifumuliwe
Pamoja na uzuri unaotajwa, sheria hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatib amesema kulingana na mahitaji ya sasa ni muhimu sheria ya vyama vya siasa ifanyiwe maboresho.
Amesema kwa mazingira ya sasa hitaji ni kubwa kufanyika mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa kwa kuwaita wadau na kutoa mapendekezo ya vifungu vya kubadilishwa.
“Ukiangalia wenzetu wa Kenya sheria zao zinawaruhusu kuungana wakati wa uchaguzi na kumweka mgombea mmoja na kuunda Serikali kwa kugawana nafasi, hapa ni tofauti na hata mgombea binafsi haruhusiwi,” amesema.
Sheria inaruhusu demokrasia
Akijibu hoja hizo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema sheria ya vyama vya siasa inaruhusu demokrasia na wale wanaosema hairuhusu ndio wasiopenda demokrasia.
“Sheria imewekwa kuhakikisha demokrasia inakuwa kwenye vyama vya siasa, ndio maana kuna sheria ambayo inataka mgombea atoke kwenye chama cha siasa na awe amepitishwa na wanachama, hii tunaondoa ule utaratibu wa mtu kuamka na kujipitisha peke yake ndani ya chama,” amesema.
Nyahoza amesema endapo msajili asiposimamia vyama vya siasa uoneaji utakuwepo na watakaoumia ni wanachama.
Amesema dhana ya kuwa Ofisi ya Msajili imepewa madaraka makubwa kisheria hadi kuingia kwenye vikao vya ndani ya vyama va siasa si sahihi na kuwa lengo la kifungu hicho ni ni kusimamia vyama vifuate taratibu walizojiwekea.
Nyahozya amesema vyama visipofuata katiba zao wanaoumia ni wanachama na hakuna eneo lingine la kwenda kulalamika bali ndani ya ofisi hiyo.
“Lazima kuwepo taasisi inayohakikisha vyama vinafuata taratibu zao, amesema.
Amesema wapo watu wanazungumza mambo wasiyoyafahamu kwamba hatuna mamlaka ya kufuata chama cha siasa, unawezaje kuwa na mamlaka ya kukisajili ukakosa mamlaka ya kukifuta? Ni kama kazini tu, umeajiri mfanyakazi, mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni nani? Si aliyemuajiri?” amehoji.
Suala hili liliwahi kutinga kwenye vyombo vya maamuzi, ambapo Machi 25,2022, Mahakama ya Afrika Mashariki ilimpa ushindi Freeman Mbowe na wenzake watatu, Seif Sharif Hamad (marehemu), Zitto Kabwe, Hashim Rungwe, Salum Mwalimu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) kwenye kesi juu ya Mamlaka ya Msajili wa Vyama vya siasa, ikisema baadhi ya vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa vinakiuka mkataba wa EAC.