Tuanzie alipoishia Samia kuhusu vumbi la kongo

Muktasari:

  • Septemba 30, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan, alionyesha kushtushwa na jinsi taifa la Tanzania linavyotengeneza vijana balehe wenye matatizo ya nguvu. Akashauri utafiti ufanyike.

Septemba 30, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan, alionyesha kushtushwa na jinsi taifa la Tanzania linavyotengeneza vijana balehe wenye matatizo ya nguvu. Akashauri utafiti ufanyike.

Hofu ya Rais Samia ni kuwa kama hali itaendelea ilivyo sasa, kuna uwezekano wa Tanzania kuwa taifa goigoi. Mtazamo wa Rais ni kwamba tatizo la lishe ni kubwa kwa vijana, na ndio sababu kuna shida ya nguvu na uwezo wa kupata watoto.

Suala kama hilo lilishazungumziwa na Mwanasheria wa Ufaransa, Anthelme Brillat-Savarin, alitoa andiko kwa lugha ya Kifaransa lenye kichwa “Fiziolojia ya Ladha, au Tafakuri ya Ulaji Unaonenepesha.”

Ndani ya andiko hilo la mwaka 1826, Brillat-Savarin, alisema “Niambie unakula nini nami nitakueleza jinsi ulivyo.” Ni tafsiri kuwa ulaji humpambanua binadamu alivyo.

Kutoka mwaka 1826 katika andiko la Brillat-Savarin mpaka 1930, ni miaka 104. Mtaalamu wa lishe wa Marekani, Victor Lindlahr, alianza kutoa machapisho ya “Wewe Ni Kile Unachokula”.

Mwaka 1942, Lindlahr aliendeleza msemo wa You Are What You Eat alipotoa kitabu chenye kichwa “You Are What You Eat: how to win and keep health with diet.” – “Wewe Ni Kile Unachokula: jinsi ya kushinda na kutunza afya kwa lishe.”

Kwa mantiki hiyo, Rais Samia anaamini kuwa ulaji mzuri unaweza kuwa suluhisho la mteremko wa sasa wa nchi kuelekea kuwa taifa la vijana goigoi, kuzaa watoto wenye afya na pasipo changamoto.

Rais Samia aliyazungumza hayo kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamiaji shughuli za lishe, Dodoma. Kwa mantiki hiyo, alikuwa kwenye jukwaa sahihi, kutoa neno lake kuhusu kile ambacho kimekuwa mjadala mkubwa mitandaoni.

Mapokeo anuwai

Kukazia hoja yake, Rais Samia aligusia wimbi la vijana kutumia vumbi la kongo na supu ya pweza kama kielelezo cha tatizo kuwa kubwa, lakini linafanywa siri.

Karne ya 21 ilipowadia na fujo za majukwaa ya kimtandao ziliibuka. Mark Zuckerberg na wenzake walianzisha Facebook mwaka 2004, kisha Jack Dorsey na washirika wake walileta Twitter, Julai 2006. Ongeza na mingine.

Matumizi ya majukwaa ya mtandao yamekuwa sababu ya uhuru mkubwa wa mawazo. Kila mtu kwenye ukurasa au akaunti yake anaweza kutoa mchango wake kwa namna inavyompendeza. Kuna makosa lakini utamu wa dunia umeongezeka.

Sasa, kitendo cha Rais Samia kugusa vumbi la kongo na supu ya pweza, hotuba yake yote ikamezwa hapo. Mitandao ikacharuka. Hata vyombo vya habari, hasa redio na magazeti, mjadala ukawa hapo.

Ni mapokeo anuwai. Rais Samia aliposema vumbi la kongo na pweza kama matokeo ya lishe duni kwa Watanzania, mjadala ulipaswa kutanuliwa kuhusu madhara makubwa ya ulaji.

Mathalan, ukipitia hotuba ya Rais Samia kwa mtindo wa kati ya mistari (between the lines), utagundua kuwa aligusia ulaji wa kujibana ili kuzuia kunenepa na vyakula visivyo na rutuba. Alisema kuhusu chips.

Ingevutia kuona vyombo vya habari vikijitokeza na mijadala mbalimbali. Wanaokula kwa kujibana ili wawe wembamba, wataalamu wangeulizwa watoe maoni yao. Ingesaidia kupanua maudhui ya kile ambacho Rais Samia alikizungumza.

Kuhusu chips kuwa chakula kisicho na rutuba. Wataalamu wa lishe wangetafutwa watoe majibu. Au na wao wenyewe kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii, wangejitokeza kutoa mchango wao na kusaidia kuelimisha.

Kinyume chake, mantiki ya lishe imefunikwa na vumbi la kongo. Na ujuavyo binadamu, hupenda masuala mepesi. Basi kila mmoja akajadili vumbi la kongo kwa namna yake.

Huwezi kulaumu. Chochote ambacho humfariji binadamu, humpotezea mawazo, humsahaulisha machungu kwa muda au chenye kumchekesha, hiyo ni tiba ya ubongo. Kuna faida zake.

Binadamu wengi hutumia mitandao kufurahi kuliko kuelimika. Kulainisha vifua badala ya kutafuta taarifa za msingi. Kauli ya Rais Samia kuhusu vumbi la kongo iliwezesha wengi kufurahi na kulainisha vifua vyao.

Tanzania na misukosuko yake. Changamoto za kimaisha ni nyingi na mahitaji ni mengi kuliko vipato. Tatizo la afya ya akili pengine lingekuwa kubwa zaidi kuliko sasa kama vituko, visa, vitimbi, kejeli na mauzauza ya mitandaoni isingekuwepo.

Na uongozi wa serikali, unahitaji watu wawe wanapumua na kulainisha vifua kuliko kujaza sumu za chuki na maumivu. Hivyo, ni kweli mitandaoni kuna upotoshaji mwingi na uharibifu wa maadili. Hata hivyo, isisahaulike; mitandao imekuwa tiba.

Lishe ni nguvu za kiume tu?

Ni swali; kauli ya Rais Samia haijaelekezwa hata kwenye changamoto ya watu kujipunguza wawe wembamba. Kila kitu kimebebwa ndani ya vumbi la kongo. Ni kwa sababu linagusa nguvu za kiume.

Naam, nguvu za kiume ni mjadala mzito. Kelele ni nyingi mitandaoni mpaka kwenye vyombo vya habari. Mada zinatengenezwa redioni na kwenye televisheni. Madaktari wanazungumza. Watu wa tiba mbadala wanatengeneza utajiri wa haraka.

Matangazo mengi na mijadala mfululizo kuhusu tatizo la nguvu za kiume, ni sababu ya wanaume wengi kupoteza hali ya kujiamini. Wanajiona wana upungufu. Wasichojua ni kuwa hata wanaopiga kelele nao wanakimbilia njia mbadala.

Kwani kipimo cha nguvu za kiume ni nini? Kurutubisha yai la mwanamke na kutunga mimba? Mbona wanaume wengi wenye watoto nao wanakutana na changamoto? Wanaambiwa hawajiwezi, kisha wanakwenda kuvamia tiba mbadala.

Wasio na watoto lakini hawana kasoro yoyote ya kimaumbile katika ushiriki wa tendo la kutafuta mtoto, nao hawana nguvu. Mwingine ushiriki wake ni mzuri lakini anapata hofu anapoingia mitandaoni na kukuta matangazo kuwa ushababi ni kuzunguka mara nyingi kwa kuunganisha.

Wengine wapo imara kabisa lakini uwezo wao unazorota kwa sababu ya kasoro za wanawake. Uchafu na hata maumbile. Hata hivyo, mwisho kabisa, kila hali ya kushindwa au kwenda chini ya kiwango, inatafsiriwa ugonjwa wa mwanamume.

Ijenge picha kuwa tatizo la upungufu wa nguvu za kiume halipingiki kuwa lipo. Isipokuwa linakuzwa mno kwa sababu limeshafanywa fursa kubwa ya kifedha. Na wanaume kwa sababu imani yao ni kuwa uanaume unatafsiriwa na hilo tendo, kuna wakati wanageuka kama vichaa. Chochote watakula.

Wakiambiwa wale kinyesi cha kenge watakula. Akitokea mhuni akisema lami nyeusi ukiiyeyusha kuwa kimiminika na kunywa vijiko vitatu kwa siku, watatii maelekezo. Vumbi la kongo linakosaje wateja? Wanatafuta ushababi.

Tukuze mjadala

Maradhi yasiyoambukiza (noncommunicable diseases ‘NCDs’), kama kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi, kansa na ugonjwa wa mapafu, yanatajwa kuchangia asilimia 70 ya vifo vyote duniani kila mwaka.

Magonjwa ya NCDs, kwa sehemu kubwa ni matokeo ya ulaji mbaya. Hapa ilitakiwa wataalamu wa lishe na madaktari waanzie alipoishia Rais Samia kwa kutoa elimu pana jinsi mtindo wao wa kula unavyoweza kuwapa maradhi yasiyoambukiza.

Kama Lindlahr alivyosema “You Are What You Eat”, wataalamu wa lishe wangeeleza kwa upana ni kwa kiasi gani hotuba ya Rais Samia ni muhimu kuzingatia kwenye mtindo wa kila siku wa maisha.

Hapohapo inafahamika kuwa magonjwa hayo yasiyoambukiza kwa wanaume yamekuwa sehemu ya punguzo kubwa la nguvu. Mtu mwenye kisukari na ugonjwa wa moyo, anawezaje kuwa timamu kimwili?

Kumbe lishe ni muhimu mno kuchambuliwa katika uwanda mpana. Watanzania wengi wanakosa maarifa haya kwa sababu tatizo la nguvu za kiume linajadiliwa kama ulemavu au ugonjwa unaojitegemea. Wakati ni matokeo ya shida nyingine ambayo tayari ipo ndani ya mwili.

Kumekuwa na ulemavu mkubwa kwenye vyombo vya habari. Kutotengeneza matawi na kujenga uchambuzi wa kila tawi ndani ya habari. Tunajikita zaidi katika mambo mepesi. Kwa mwendo huu, Rais Samia anahofia lishe duni kujenga taifa goigoi, binafsi naona vyombo vya habari vikijenga nchi ya watu wenye fikra dhaifu.

Ni kweli watu wa mitandao wanapenda vitu vyepesi. Hata hivyo, kumekuwa na ukosefu mkubwa wa maudhui ya kujenga fikra za kuelimisha. Matokeo yake wenye wajibu wa kuelimisha nao wanabebwa na mkumbo wa mambo mepesi. Tunaunda taifa la vitu vyepesi.