Tuepuke aibu hii Bunge EALA

Muktasari:

  • Awali niweke wazi kabisa kwamba mimi si mwanachama wa CCM. Ni mwana UDP pamoja na migogoro inayoendelea kwa muda mrefu sasa bila kupata ufumbuzi kutoka mamlaka husika.

Awali niweke wazi kabisa kwamba mimi si mwanachama wa CCM. Ni mwana UDP pamoja na migogoro inayoendelea kwa muda mrefu sasa bila kupata ufumbuzi kutoka mamlaka husika.

Yangu kwa leo, ni juu ya yaliyojiri kwenye mchakato wa kuwapata wajumbe wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki au EALA.

Nafanya hivi kwa kuzingatia ile kauli ya marehemu Rais John Magufuli kuwa “maendeleo hayana chama”.


Kwa nafasi ya CCM katika mustakabali wa nchi, hatuna budi kuwapongeza wanapostahili na kuwamulika pale mambo yanapoenda ndivyo sivyo kama kwenye hili la EALA.

Kwa mtazamo wangu mchakato wa kuwapata wajumbe wa EALA ulianza kwenda mrama kuanzia hatua ya kutoa taarifa. Yaani ni jambo la kushangaza kwamba ofisi ya Bunge ilishindwaje kutangaza nafasi hizo kupitia magazeti tangu Agosti mwanzoni kama ambavyo ilipaswa. Haiwezekani jambo ambalo linahusu masilahi ya nchi kupitia uwakilishi wake EALA uishie tu kwenye gazeti la Serikali.

Wenzetu Waganda kwa mfano walitoa taarifa ya kina kwenye gazeti la The EastAfrican. Hatua zote za mchakato ziliainishwa. Hii ilinishangaza kiasi nilitamani wanasheria wetu hapa Tanzania wangeenda mahakamani ili kuilazimisha ofisi ya Bunge kufuata utaratibu sahihi. Sijui ofisi hiyo nyeti hapa nchini ilikuwa inakwepa gharama ya matangazo au kitu gani hasa?


Sasa twende kwenye mchakato wenyewe ndani ya CCM. Sio siri kwamba kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu hapa nchini kuhusiana na aina ya watu ambao kwa ujumla wanatuwakilisha EALA. Kubwa kabisa ni kwa upande wa lugha tu ya Kiingereza. Ni aibu pande zote!


Najua kuna watu kadhaa ambao kwa sababu nzuri tu wanasema Kiswahili kilipaswa kutumika. Ni jambo ambalo lina mantiki kubwa, ila kwa sasa hatuna namna ya kukwepa matumizi ya Kiingereza.


Na kuhusu lugha sina budi kusema ni kitu cha ajabu kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano inazungumzia sifa ya kuwa mbunge wa kitaifa ni ‘kujua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza’.
Yaani karne ya 21 tunatumia kigezo hicho?
Hapa nitataja kesi iliyomkuta marehemu Al Noor Kassum, ambaye alikuwa kwenye baraza la mawaziri kuanzia mwaka 1977 hadi 1990.
Katika kitabu cha maisha yake, Africa’s Winds of Change, Kassum, anaeleza jinsi ambavyo Mwalimu Nyerere alitaka awe waziri na alijikuta anamjibu kwamba, ‘lakini Mwalimu, sijui lugha ya Kiswahili vizuri, nitawezaje kufanya kazi yangu?’


Mwalimu alinijibu, ‘sikuteui kuwa waziri au mbunge kutokana na uwezo wa kuongea Kiswahili. Wabunge wote wanapaswa kukijua Kiingereza, hivyo unaweza kufanya mawasiliano kwa Kiingereza.’ (Tafsiri yangu).


Nilijiuliza sana kama wabunge wote walipaswa mwaka 1977 kukijua Kiingereza, mbona sasa kinawapiga chenga, pamoja na wasomi?


Ukiondoa hiyo unakuta hata kwa lugha ya Kiswahili, waombaji wengi wa nafasi za uongozi wanakuwa na hoja dhaifu.

Mfano tu ni baada ya Spika Job Ndugai kujiuzulu na CCM kumpitisha Tulia Mwansasu kama mgombea pekee, wagombea wa upinzani waliobaki walikuwa kama wanagombea nafasi kwenye uongozi wa chuo.


Vilevile, aina ya maswali kwenye chaguzi zetu bungeni ni ya kiwango cha chini sana hadi kuhuzunisha. Inafikia hatua ya kutamani zoezi zima lisitishwe.


Kwa vyovyote vile mabadiliko ya msingi ni jambo la lazima kuhusiana na namna tunavyowapata wawakilishi wetu nje ya nchi ambao tija yao ni ndogo sana.

Kabla sijatoa mapendekezo yangu niseme tu safari hii nilikuwa na hamu ya kuona kutakuwa na utofauti gani kati ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na ule wa waliomtangulia.

Mama Samia au shangazi wa Afrika Mashariki kama ambavyo Rais wa Kenya, William Ruto alivyomuita siku ya kuapishwa kwake alipaswa kuonyesha utofauti katika masuala mbalimbali.

Hayati Benjamin Mkapa, katika kitabu alichokiandika cha My Life, My Purpose, alionyesha masikitiko yake ya kutopigania kwa namna ilivyopaswa utengamano wa Afrika Mashariki.

Rais Samia kwa kweli kwenye masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki amejitahidi sana kuonyesha maono thabiti kiasi kwamba ilikuwa muhimu sana wapatikane wajumbe makini EALA kuungana naye kwa vitendo. Kwa bahati mbaya sikuliona hili katika vigezo.
Tofauti kubwa nimeiona tu katika ada ya kuchukua fomu.

Awamu hii, fomu peke yake ilikuwa Sh1 milioni! Nilifikia hatua ya kusema, Mungu wangu! Ina maana kama EALA tu ni kiwango hicho, mwaka 2025 fomu ya ubunge wa kitaifa inaweza kuwa ni kiasi gani? Na vipi kuhusu ya urais hapo 2025? Ndipo nikamkumbuka Mwalimu Nyerere. Nikajiuliza, leo hii Mwalimu Nyerere angejisikiaje kuwa kile chama chake alichokiita cha Wafanyakazi na Wakulima kimefikia hapo.


Mwalimu alituasa sana kwamba ‘fedha si msingi wa maendeleo’. Sasa kama uchukuaji wa fomu tu ni Sh1 milioni, maana yake CCM wanaamini mambo tofauti kabisa na aliyokuwa akiyaamini Mwalimu. Pia hivi kweli chama ambacho kinahitaji wanachama wake kujaza nafasi za umma kifikie hatua ya kuwataka waingie gharama kubwa kiasi hicho. Kwa maoni yangu fomu ilipaswa kutolewa hata bure kutokana na wanachama wake kuwa mtaji wa chama. Haiingii akilini kabisa kulipia fomu.
Hata hivyo, nilifikiria kwamba pengine CCM safari hii wanataka wanachama wao kujipima sana kabla ya kukimbilia kuchukua fomu. Nilisubiri kuona matokeo yake. Kilichotokea ni yaleyale ya watu kukimbilia fomu yalitokea. Wanachama zaidi ya 150 waliingia kwenye kinyang’anyiro.


Hakika tatizo la ajira hapa nchini ni bomu! Haiwezekani watu kuchukua fomu kwa nafasi chache kama hizo iwe ni gharika!
Zaidi ya hapo, tulisikia kuhusu utaratibu wa mahojiano ya wagombea Dodoma. Inaonekana haikusaidia kutokana na majina mengi yaliyoingia kwenye mchujo kuwa mepesi mno.
Yaani huwezi kutegemea hata siku moja kukutana na makala kutoka wengi wao inayoelezea changamoto za EAC, hususan za kiuchumi.
Nikajiuliza hivi kweli CCM kwa mfano, wanashindwa kuzingatia uzito wa biashara katika nchi za Afrika Mashariki na kumpa nafasi mtu mzoefu kwenye masuala hayo kama Godfrey Simbeye ambaye aliomba kutuwakilisha. Ana uzoefu mkubwa wa kuongoza taasisi ya sekta binafsi na matokeo ni wazi. Ni dhahiri alikuwa anashabihiana na maono ya Rais Samia kuhusu EAC.


Au vilevile, Lathifa Sykes ambaye ni mdau mkubwa katika sekta ya utalii ndani na nje ya nchi. Yaani Rais Samia kama balozi wetu namba moja wa utalii nchini angekuwa na mtu wake wa “mkono” nikitumia lugha ya Rais Ruto alipokuwa naibu rais. Haya basi kuna Balozi Dk James Msekela wenye uzoefu wa kidiplomasia.

Pia ni mwenyekiti wa mabalozi wastaafu. Naye aliishia kuwa msindikizaji tu. Mwishoni, tulisoma kuwa majina ya wagombea wa CCM yaliyofikishwa kupigiwa kura na Bunge la Jamhuri ya Muungano ni manane. Na hiyo ndiyo idadi kamili ya wajumbe wa EALA wanaotakiwa kwa upande wa CCM. Kwa hiyo kazi ilikuwa ni kuwathibitisha tu na si uchaguzi. Kwa lugha ya kigeni ni ‘fait accompli’ na ni dhahiri mahojiano yalikuwa kiinimacho. Kutokana na hiyo hali ni vyema wagombea wa CCM ambao hawakufanikiwa watafutiwe njia nzuri ya kurudishiwa fedha zao.

Hiyo Sh1 milioni, nyingine walizotumia kwa safari, malazi, chakula na huduma nyinginezo zingeweza kuwasaidia watu kadhaa kama mtaji wa kufanya biashara ndogo. Fikirieni jamani ni leseni ngapi za biashara zingepatikana hapo.

Cha kufanya
Napendekeza mambo mawili yafanyike ili kuepuka aibu inayojirudiarudia kwa wawakilishi wetu.

Wagombea wote wa nafasi za uwakilishi wa nchi kama EALA na wale wa Bunge la Afrika (PAP) iliyopo Afrika Kusini, wapitie kozi kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi kilichopo Kunduchi.

Kama mtu hajafaulu kozi basi aachane na habari ya uongozi. Ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna changamoto lukuki za ulinzi na usalama, hivyo kuwa na wawakilishi wenye uwezo wa kuyaelewa tu ni hatua nzuri sana.

Pili ni kuhusiana na kuruhusu wagombea nje ya vyama vya siasa. Haiwezekani watu wote watokane na chama cha siasa kama vile nje ya wigo huo hatuna wanaofaa. Kuna watu wazuri sana nje ya vyama vya siasa ambao wanaweza kutusaidia kupitia kwa jumuiya zao mbalimbali kama ya wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi. Hapo pia hata asasi za kiraia. Wapewe jukumu la kupendekeza baadhi ya watu ambao lazima waende NDC.


Andrew Bomani ni mwanasayansi wa siasa na Kaimu Katibu Mwenezi wa UDP: 0784219535