Prime
UCHAMBUZI WA MAYALA: Wito wa kuimarisha uwajibikaji na nafasi ya vyombo vya habari
Muktasari:
- Pamoja na kwamba uchunguzi rasmi kupitia tume mbalimbali bado unaendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo, baadhi ya wadau wa maadili ya uongozi wanasema ni muhimu pia kuangalia mwenendo wa kauli za viongozi kabla ya tukio hilo.
Mjadala unaoendelea kuhusu tukio la Oktoba 29 umeibua tena mjadala mpya kuhusu nafasi ya kauli za viongozi wa umma kwa wananchi na mchango wake katika kuathiri mwenendo wa matukio ya kitaifa.
Pamoja na kwamba uchunguzi rasmi kupitia tume mbalimbali bado unaendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo, baadhi ya wadau wa maadili ya uongozi wanasema ni muhimu pia kuangalia mwenendo wa kauli za viongozi kabla ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa wadau hao, baadhi ya viongozi wa umma walikuwa wakitoa kauli ambazo zinapingana na misingi ya maadili ya uongozi, hali ambayo inaweza kuwa na athari kwa ustawi wa jamii endapo haitadhibitiwa kwa wakati.
Wito umetolewa kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuimarisha zaidi juhudi zake za kuwafunda na kuwajengea uelewa viongozi kuhusu maadili ya utumishi wa umma, sambamba na kuweka utaratibu wa kutoa tahadhari, au kukemea mapema pale inapobainika uwepo wa kauli au mienendo inayoweza kuathiri maadili ya uongozi.
Wadau hao wamehoji iwapo Sekretarieti hiyo inaweza kuiga utaratibu wa taasisi nyingine kama Msajili wa Vyama vya Siasa katika kutoa msimamo wa haraka pindi zinapojitokeza kauli au vitendo vinavyokiuka maadili, badala ya kusubiri malalamiko rasmi au madhara kujitokeza kabla ya hatua kuchukuliwa.
Mjadala huo umetolewa kufuatia kikao kazi cha mwaka kati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, chini ya Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji (Mstaafu) Sivangilwa Mwangesi.
Katika kikao hicho cha nne mfululizo, Sekretarieti imekuwa ikiendelea kujenga ushirikiano na wahariri kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kupokea maoni na kuongeza uelewa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uadilifu nchini.
Kamishna Mwangesi aliipongeza sekta ya habari kwa mchango wake katika kuimarisha uwajibikaji na maadili ya viongozi wa umma, akisema vimekuwa mstari wa mbele kuripoti masuala yanayosaidia kubaini changamoto za kimaadili zinazojitokeza kwa viongozi.
Hata hivyo, wadau wameeleza kuwa licha ya jitihada hizo za elimu kwa umma zinazotolewa kupitia warsha, semina, makongamano na vyombo vya habari, bado hazitoshi kuleta mabadiliko ya kina yanayotarajiwa katika kuimarisha maadili ya uongozi.
Wamependekeza Sekretarieti hiyo kuwa na Mkakati wa Mawasiliano (Communication Strategy) wenye malengo mahsusi ya kimkakati yatakayojumuisha si tu utoaji wa taarifa, bali pia programu za elimu kwa umma kupitia redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii ili kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu maadili ya uongozi.
Kwa upande wa vyombo vya habari, imeelezwa kuwa pamoja na kuwa na maadili yake ya kitaaluma, bado kuna changamoto ya kuripoti kwa kiasi kikubwa taarifa zinazotolewa na viongozi, huku maeneo ya ukiukwaji wa maadili yakipata nafasi ndogo zaidi ya uchambuzi na ufuatiliaji.
Wadau wamesema endapo waandishi wa habari na taasisi za vyombo vya habari zingekuwa na mtazamo wa pamoja wa kuchangia uadilifu wa kitaifa kwa kuripoti na kuchunguza vitendo vya ukiukwaji wa maadili, baadhi ya changamoto za kijamii na kisiasa zingepungua, ikiwemo migogoro na malalamiko ya wananchi dhidi ya viongozi.
Uadilifu wa viongozi wa umma umeelezwa kuwa msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, kwani huimarisha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wote badala ya kundi dogo.
Kwa mujibu wa wadau hao, kukosekana kwa uadilifu husababisha manung’uniko, upendeleo na mgawanyo usio sawa wa rasilimali, hali inayoweza kuathiri amani na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, wamehimiza waandishi wa habari kutumia taaluma yao kwa weledi katika kuripoti masuala ya maadili, huku wakisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kitaaluma pindi viongozi wanapotoa kauli au kufanya vitendo vinavyoweza kukiuka misingi ya maadili ya umma.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni chombo kilichoanzishwa chini ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, ikiwa na jukumu la kusimamia uadilifu katika utumishi wa umma.
Ndiyo maana wadau wamesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Sekretarieti, vyombo vya habari na taasisi nyingine za umma ni muhimu katika kujenga jamii yenye viongozi na wananchi wanaozingatia maadili, uwajibikaji na mshikamano wa kitaifa kwa maendeleo endelevu ya nchi.