Prime
Ushahidi kupinga ubunge wa Baba Levo kuanza kutolewa Juni 18
Muktasari:
- Kesi ya uchaguzi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini mwaka 2025, ambapo mgombea wa CCM alitangazwa mshindi, sasa imepangwa kuanza kusikilizwa katika hatua ya ushahidi baada ya taratibu za awali kukamilika.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, imepanga kuanza kusikiliza kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini katika hatua ya ushahidi kuanzia keshokutwa, Alhamisi, Juni 18, 2026.
Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa taratibu za awali na za msingi za usikilizaji wa kesi hiyo, ambazo zimehitimishwa katika hatua ya usikilizwaji wa awali iliyofanyika jana Jumatatu, Juni 15, 2026 jioni.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo na hivyo kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Baba Levo alitangazwa kushinda kiti hicho akimzidi mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne, Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, wamefungua kesi dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi, mbunge huyo Chipando na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakipinga uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, wadai hao, ambao wanajitambulisha kuwa wapiga kura katika jimbo hilo, wanadai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.
Wanabainisha kasoro hizo kuwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo, wanaiomba mahakama hiyo, pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Serikali kwa upande mmoja na Baba Levo kwa upande mwingine wamekuwa wakiibua mapingamizi mbalimbali wakiishawishi mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo bila kusikiliza ushahidi wa madai hayo, wakidai kuwa imegubikwa na kasoro mbalimbali za kisheria.
Hata hivyo, jitihada za wadaiwa hao kutaka kuimaliza kesi hiyo kwa mbinu za kiufundi, kupitia mapingamizi ya awali ya hoja za kisheria, zimegonga mwamba, kwani mara kadhaa mahakama hiyo imekuwa ikiyakataa mapingamizi hayo.
Kutokana na mvutano huo, muda wa awali wa usikilizwaji wa kesi za uchaguzi uliisha hata kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa katika madai ya msingi, jambo ambalo limemlazimu Jaji Mkuu, George Masaju, kwa mamlaka aliyo nayo kisheria, kuongeza muda wa miezi sita wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Baada ya kupenya katika mapingamizi hayo, hatimaye jana kesi hiyo iliingia katika hatua ya usikilizwaji wa awali ikiwa ni maandalizi ya usikilizwaji kamili wa madai ya msingi.
Katika hatua hiyo, wadaiwa wamesomewa muhtasari wa madai ya kesi hiyo na kisha wakatakiwa kubainisha mambo au hoja wanazokubaliana nazo na zile wasizokubaliana nazo katika maelezo hayo, ambazo ndizo upande wa wadai watakuwa na wajibu wa kuzithibitisha.
Wakili wa wadai, John Seka, ameieleza mahakama hiyo kuwa wadai wanatarajia kuwaita mashahidi wasiopungua 20 na kuwasilisha vielelezo mbalimbali.
Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo alipanga kuanza rasmi usikilizaji wa kesi hiyo, ambapo sasa upande wa wadai wataanza kutoa ushahidi wao na kuwaita mashahidi wao wengine kuunga mkono ushahidi na madai yao kuanzia keshokutwa, Alhamisi.
Kesi hiyo, ambayo imefunguliwa na wanachama wa ACT-Wazalendo, inaingia katika hatua hiyo ya usikilizwaji kamili wakati chama hicho kikiwa na kumbukumbu ya kushinda kesi moja kati ya tisa za uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wa mwaka 2024.
Katika shauri hilo lililofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa uenyekiti katika Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Lovi Omary Lovi, Mahakama ya Wilaya ya Kigoma ilitengua ushindi wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Hassan Mlai Mashoto.
Katika shauri hilo, Lovi alikuwa anapinga mwenendo na matokeo hayo akidai kuwa mchakato wa uchaguzi na uchaguzi wenyewe ulikiuka kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi kwa kuwa uligubikwa na ulaghai kutokana na kuwepo kwa kura bandia na hivyo kuufanya kutokuwa huru na wa haki.
Alidai ukiukwaji huo wa sheria, kanuni na taratibu ulisababisha madhara kwake na kwa wananchi kwani walinyimwa haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Hivyo, aliiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, imuamulie msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku saba na kwamba ndani ya siku 60 uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo uendeshwe.
Mahakama hiyo, katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu Katoki Mwakitalu Februari 24, 2025, ilitengua ushindi wa Mashoto na kubatilisha uchaguzi katika mtaa huo baada ya kukubaliana na madai na ushahidi wa Lovi, ikisema kuwa imeridhika kuwepo kwa ulaghai na kura bandia.