Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo ACT Wazalendo waanza ‘kutimua vumbi’ majimboni

Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo

Muktasari:

  • ACT Wazalendo,  imeanza tena ziara mikoa mbalimbali na itawahusisha Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti, Isihaka Mchinjita, Katibu Mkuu, Ado Shaibu pamoja na Kiongozi wa Chama mstaafu Zitto Kabwe ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa chama cha ACT Wazalendo wameanza awamu ya pili ya ziara zao kwa wananchi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Awamu ya kwanza ya ziara hiyo iliyopewa inayoongozwa na kaulimbiu ya “Miezi 10, Wanachama Milioni 10” ilifanyika kuanzia Julai 22, 2024 hadi Agosti 17, 2024 ikihusisha majimbo 125 yaliyopo katika mikoa 22.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo, ziara hiyo itawahusisha Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti, Isihaka Mchinjita, Katibu Mkuu, Ado Shaibu na Kiongozi wa Chama mstaafu Zitto Kabwe

Shangwe ameeleza katika taarifa yake kwamba Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu atatembelea majimbo 25 kwenye mikoa ya Pwani, Dodoma, Manyara, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Amesema Mchinjita atatembelea majimbo 21 katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro wakati Shaibu akitembelea majimbo 29 katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Geita, Mwanza, Simiyu, Kagera na Mara.

Kwa upande wa Zitto, Shangwe amesema atakuwa na ziara kwenye majimbo 29 ya mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe.

Katika taarifa hiyo, Shangwe ameeleza kwamba malengo ya awamu ya pili ya ziara hiyo pamoja na kuendelea kuimarisha chama katika kona zote za Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo la halmashauri kuu ya chama hicho.

“Halmasahuri kuu ilielekeza kwamba kabla ya kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa ni lazima viongozi wakuu wa chama wafanye ziara kwenye kila jimbo katika majimbo yote 214 ya Tanzania Bara. Ziara hii ya awamu ya pili inakamilisha utekelezaji wa agizo hilo,” amesema.

Lengo jingine la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa azimio la halmashauri kuu ya chama la kuhakikisha kila kitongoji, kijiji na mtaa kina mgombea wa ACT Wazalendo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amebainisha kwamba halmashauri kuu imeagiza chama kisimamishe wagombea kwenye vitongoji, vijiji na mitaa yote nchini. Hivyo, amesema ziara hiyo inakwenda kuhakikisha hakuna kitongoji, kijiji wala mtaa unakwenda kwenye uchaguzi huo bila kuwa na mgombea wa ACT Wazalendo.

“Wanachama 418,000 wameandaliwa kuwa wagombea katika ngazi mbalimbali zinazogombewa katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa,” amesema naibu katibu huyo kwenye taarifa yake kwa umma.

Chama hicho kinalenga pia kuhamasisha kampeni ya kusajili wanachama milioni 10 kwa miezi 10 ambayo ilizinduliwa rasmi Julai 22, 2024. Amesisitiza kwamba ACT Wazalendo ilijiwekea lengo la kuwa chama chenye idadi kubwa ya wanachama nchini ifikapo Aprili 2024.

Vilevile, viongozi wa chama hicho wanakwenda kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitolea majawabu kwa kuzingatia ahadi ya ACT Wazalendo kwa Watanzania ya Taifa la Wote, Maslahi kwa Wote.