Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi upinzani wafunguka ishu ya 'kuungana'

Muktasari:

  • Juzi Jumatano, Septemba 24, 2024 akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbozi mkoani Songwe katika mwendelezo wa ziara ya kuimarisha chama hicho, Zitto alivishauri vyama upinzani kukaa mezani na kutengeneza mchoro utakaohakikisha wanaibuka kidedea katika ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Dar es Salaam. Wakati Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akivichorea ramani vyama vya upinzani ili kukishinda Chama cha Mapinduzi, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wamesema ni wazo zuri lakini wana hofu kuhusu utekelezaji wake.

Baadhi ya viongozi hao wamesema hofu hiyo inatokana na kilichojitokeza mwaka 2015 katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakidai kulikuwa na mambo ya kusalitiana, huku chama kimoja kujiona bora kuliko vyama vingine.


Juzi Jumatano, Septemba 24, 2024 akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbozi Mkoa wa  Songwe katika mwendelezo wa ziara ya kuimarisha chama chake cha ACT- Wazalendo,, Zitto alivishauri vyama upinzani kukaa mezani na kutengeneza mkakati utakaohakikisha wanaibuka kidedea katika ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD viliungana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambapo kwa mara ya kwanza uliacha historia kwa Bunge kuwa na wabunge wa upinzani 116 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Kwenye uchaguzi huo, uliohusisha majimbo 258, kati ya 262 CCM ilishinda ubunge katika majimbno 188, CUF 35, Chadema 34, NCCR –Mageuzi kiti kimoja, NLD haikupata. Katika mgawanyo wa viti maalumu CCM ilipata wabunge (64), Chadema (36) na CUF (10).

Lakini mwaka huohuo ndiyo kipindi halmashauri nyingi na manispaa katika majiji makubwa ya Dar es Salaam, Mbeya na Arusha zilinyakuliwa na vyama vya upinzani.


Alichosema Zitto

Akiwahutubia wananchi hao, Zitto amesema:”Mkoa wenu wa Songwe mwaka 2015 uligawana nusu kwa nusu kati ya upinzani na CCM, sasa hivi vyama vya upinzani hapa Songwe tukaeni pamoja, tuchore mchoro tugawane majimbo ili tuinyime CCM kura katika mkoa huu.”

“Haya mambo ya kila mtu kujiingilia kivyake katika chaguzi au kujiona bora kuliko mwingine, kujiona mkubwa kuliko mwingine, hayatusaidii lolote badala yake CCM inafaidika,” amesema Zitto.

Zitto aliyehitimisha ziara yake mkoani Songwe, amewaagiza viongozi wa ACT-Wazalendo mkoani humo kukaa na vyama vya upinzani,  kuangalia vijiji, mitaa na vitongoji ambavyo Chadema ina nguvu watoe ushirikiano katika uchaguzi utakaofanyika mwisho mwa mwaka huu.

Mwanasiasa huyo, ameshauri sehemu ambayo ACT-Wazalendo ina nguvu basi vyama vya upinzani viwaunge mkono,  ili kuiondoa CCM katika madaraka kuanzia ngazi ya chini.

“Hii ndiyo kazi tunayoweza kuifanya, sisi hatuwezi kuwa watu wa kurudia mambo yaleyale, kila uchaguzi tunafanya vilevile kwa vyama kuingia kivyake vyake. Tukidhulumiwa ndiyo tunaitisha mkutano na wanahabari tunalalamika, uchaguzi ukiitishwa tunaenda kupambana walewale.

“Tukaeni chini tuisafishe CCM na inawezekana, ila bado hatujifunzi badala yake tunaongoza kwa kupigana vita wenyewe kwa wenyewe,”amesema Zitto.


Kauli yake ilivyopokelewa na  vyama vya siasa

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema kwa mwanasiasa yeyote anayezungumzia masuala ya uchaguzi wa mwaka 2025 hivi sasa, anawapoteza wananchi umakini kuhusu mchakato wa serikali za mitaa.

Amesema hivi sasa Taifa linapaswa kuzungumza uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na kabla hakujawa na mjadala wa vyama kuungana au la katika mchakato huo,  kuna jambo la haraka zaidi kuzungumzwa.

“Kuanzia Oktoba 11 hadi 20 kuna uandikishaji wa wapiga kura nchini watakaoshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, mchakato utakaowahusu wananchi wote, kwa sababu Daftari la Kudumu la Mpiga Kura halitatumika kwenye uchaguzi utakaofanyika Novemba 27.

“Ni jambo kubwa linalohitaji mjadala wa kitaifa na nguvu kubwa kwa kila chama katika mikutano pamoja na wadau, hivyo kwa sasa tujielekeze kwenye uhamasishaji wa uandikishaji wa daftari la wapiga kura wa Oktoba 11 hadi 20,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema baada ya uandikishaji itaonekana uwajibikaji wa kila mtu katika mchakato huo, ndipo watu wataanza kutamka masuala ya wagombea watakaoanza kuchukua fomu Novemba Mosi hadi 7 na uteuzi Novemba 8, wakati kampeni zikianza Novemba 20.

“Katika hatua ya sasa haipaswi kuzungumza matukio yanayohusu wagombea kabla ya kuzungumzia mambo yanayowahusu wapiga kura. Tujielekeze kuhamasisha wananchi kujiandikisha hiki ndicho kiwe kipaumbele kwenye hotuba ya kila kiongozi.

“Mimi kutolea maoni kuhusu wagombea wa serikali za mitaa hivi sasa ni kuhamisha mjadala, baada ya uandikishaji unaweza kunipigia simu kuniuliza masuala hayo mengine (ushirikiano),” amesema Mnyika.

Wakati Mnyika akieleza hayo, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi-Bara, Joseph Selasini amesema sheria ya vyama siasa hairuhusu vyama kuungana, ingawa vyama hivyo vinaweza kutengeneza muungano kwa kufuata taratibu za Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa.

Hata hivyo, Selasini amesema tayari vyama vya siasa vilishirikiana mwaka 2015, kupitia Ukawa, lakini baadaye ikatokea watu kusalitiana, kunyang’anya’na hata kile walichokubaliana na matokea yake vyama vyenye nguvu vilichukua maeneo ya vyama vingine vidogo.

“Kile kidonda kipo hadi leo, watu bado wana hofu kuhusu ushirikiano, lakini kuna vyama vilishatangaza vitasimama vyenyewe haviko tayari kushirikiana na vyama vingine.

“Hakuna ushirikiano mbaya kwa sababu umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, lakini hiyo nia njema ipo? Je, nani atakayeviweka vyama pamoja ili kutengeneza muungano huo,” amehoji.

Selasini ambaye ni mbunge wa zamani wa Rombo (2015/20), ameongeza: “Unajua kuna mambo ya ruzuku, wakati wa Ukawa baada ya matokeo kutoka, chama kimoja kilipata zaidi na kilichukua kila kitu, hakikufikiria kuna nguvu kidogo iliyowekwa na vyama vingine.”

“Zitto amezungumza kitu kizuri, lakini kinahitaji mkakati mkubwa wa kukiendea hasa baada ya kilichotokea mwaka 2015.’’

Amesema muungano ni mzuri kwa sababu kila chama kina maeneo kinapokubalika zaidi, hakuna chama cha siasa cha upinzani kinachokubalika nchi nzima, hivyo kukiwa na ushirikiano kutakuwa na matunda mazuri.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NLD, Hassan Doyo hakuwa mbali na mawazo ya Selasini akisema kuachiana majimbo, mitaa, kata siyo jambo baya kwa lengo la upinzani kupata uwakilishi katika maeneo hayohayo ikiwemo bungeni.

Kwa mujibu wa Doyo, anachotofautiana na Zitto ni namna alivyolizungumza suala hilo jukwaani wakati vyama vina ofisi zake, kwani angeweza kuviandikia barua kuvitaarifu kuhusua wazo hilo.

“Kuachiana ni wazo zuri kama mimi Handeni (Tanga), nakubalika waniachie waje na nguvu na kama Mluya (Abdul-katibu mkuu wa DP) anakubalika Mwanza wamuachie kwa nia ya upinzani kupata uwakilishi mkubwa,” amesema Doyo.

 Hata hivyo, Zitto alimjibu Doyo akisema:“Nilichokifanya ni kutoa ushauri tu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa, amesema chama hicho ni taasisi ambayo uamuzi wake unatokana na zao la vikao, si mtu mmoja.

“Hata hivyo, chama kilishawahi kuweka wazi msimamo wake endapo kutakuwa na dhamira ya dhati ya kuing'oa CCM madarakani. Muhimu kwetu ni kujiridhisha juu ya udhati wa dhamira na kutokuwepo kwa ajenda za siri,” amesema Ngulangwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amezungumza kwa ufupi akisema wazo  hilo zuri, huku  akiahidi kufanya naye mawasiliano ili kujua mchakato huo kwa undani zaidi.

 “Ni wazo zuri lakini amesema au kupanga namna ya kukutana au lini amesema tukutane tupange huu mchakato? Hata hivyo, nitajitahidi kuwasiliana naye,” amesema Rungwe.


Mitizamo ya wachambuzi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Lugome amesema kuungana kwa vyama vya siasa ni jambo jema kwa mazingira ya sasa, lakini kuna faida na hasara kadhaa.

Dk Lugome ametaja faida tatu ambazo ni, kuwa na nguvu ya pamoja kushindana na chama tawala kwa sababu kutokana na uchanga wao, vyama vingi vya upinzani havina ushawishi kila mahali nchini.

“Watasaidiana kimkakati na kifedha na hivyo kuwapa nguvu wagombea wao. Itaepusha vyama vya upinzani kugawana kura wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,” amesema.

Mwanazuoni huyo, ametaja hasara akisema vyama vya upinzani havina nguvu inayofanana, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa vyama vikubwa kuvimeza vidogo.

Aidha, amesema kuna hofu ya viongozi wa vyama vya upinzani kutoaminiana na kushutumiana usaliti na ukibaraka kwa chama tawala.

 “Wasiwasi wangu ni kuwa wanaweza kuanza vizuri lakini hapo baadaye wakiwa katikati ya utekelezaji wa mipango yao, wataanza kusambaratika kwa sababu ya kutoaminiana,’’ ameeleza.

Dk Lugome amesema kutokana na kukosekana kwa uwazi wa mapato na mgawanyo wa matumizi ya pesa wakati wa kampeni, kuna uwezekano mkubwa baadhi ya wagombea wakaachwa wapambane peke yao hasa ikionekana hawana nguvu ya kuwashinda wagombea wa chama tawala.

Amesema mwaka 2015 kuna baadhi ya vyama vililalamika kuwa viliachiwa majimbo ambayo haikuwa rahisi kuwashinda wagombea wa CCM.

 Naye, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Ali Makame Issa amesema vyama vinaweza kuungana baada ya kujipima uwezo wa kisiasa na ushawishi wa chama kilichopo madarakani kwamba ni mkubwa kuliko vyama vyao,  hivyo pasipo ushirikiano hawawezi kukiondoa.

 “Mfano vyama vya upinzani vikiwa sita na cha saba ni CCM, sasa kila kimoja kikiwa na ushawishi wake mnaweza mkapoteza kura na chama tawala kikaendelea kushinda na nguvu za upinzani zikapungua,” amesema.

“Lakini wote mkiwa na nguvu moja, mtaweza kumshambulia adu mmoja na nguvu zenu haziwezi kugawanyika kwa sababu wote mtakuwa kitu kimoja,” ameongeza Makame.

Hata hivyo, Issa amesema katika siasa muungano wa kweli unakuwa na mafanikio, lakini usio wa kweli hauna mafanikio. Alisema muungano wa kweli wote mnakuwa kitu kimoja na malengo yanakuwa sawa.

“Ikiwa mmoja wenu atakuwa na malengo au nia tofauti, matokeo yake nguvu yenu inakuwa ndogo na mnashindwa kutimiza malengo, lakini mkiwa na lengo moja hamtashawishika jambo lolote litakalowatoa kwenye umoja na mshikamano,”amesema Issa.

Issa amedai kuwa vyama vya upinzani vinashindwa kufikia malengo ya kuungana kwa sababu vinashindwa kuaminiana na kila chama kina malengo yake badala ya kuwa na lengo moja la kuiondoa CCM.