Vyama tisa vya siasa vyaingilia kati kauli ya ACT-Wazalendo

Muktasari:

Vvya tisa vya siasa Zanzibar, vimesema kauli ya Chama cha ACT-Wazalendo ya kupinga uteuzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, haina nia njema kwa Zanzibar.

Unguja. Vvya tisa vya siasa Zanzibar, vimesema kauli ya Chama cha ACT-Wazalendo ya kupinga uteuzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, haina nia njema kwa Zanzibar.


Hivi karibuni, ACT Wazalendo kilisema hakikubaliani na uteuzi wa Faina kwa madai yeye ndiye alikuwa mkurugenzi wa ZEC katika uchaguzi wa mwaka 2020 ambao haukuwa huru na haki.


Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir amesema hayo leo Jumanne Novemba 15, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Unguja kuwa kauli ya Chama hicho inalenga kuwachochea wananchi.


"Kwa mujibu wa taratibu na sheria za Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi anaendesha vizuri serikali ya umoja wa kitaifa na ndio maana tupo na uhuru kwa kufanya mambo yetu,"amesema


"Rais DkMwinyi ana uwezo wa kumteua mtu yeyote ambaye anamuona anafaa kushirikiana naye katika kuwaletea maendeleo wanzanzibar na hiyo ndio dhana ya serikali ya umoja wa kitaifa,"amesema


Amesema kitendo kinachofanywa na ACT-Wazalendo ni kumvunjia heshima Rais Mwinyi na kwamba kinachotakiwa ni chama hicho kurejea kwenye mstari.


Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo amewataka wanzanzibar kutokubali kuyumbishwa, kurudishwa nyuma na kuingizwa kwenye mifarakano isiokuwa na ulazima.


"Sasa hivi Zanzibar tunataka kujenga nchi yetu na Rais ameshasema kuwa tunatarajia kujenga barabara za juu hivyo tumuache Rais afanye kazi zake tusimuungilie,"alisema


Kwa upande wake Katibu Mkuu Jumuiya ya Wanawake UDP, Naima Salum Hamad amesema kwa vyama vya siasa ambavyo vimedhamiria kuichafua serikali ya umoja wa kitaifa vinakumbushwa kutosahau vipindi vilivyopita na kwamba kilichobakia ni kuipeleka Zanzibar mbele.


"Tunaoathirika zaidi ni akina mama na watoto, walemavu na wazee na tukirudi nyuma tutaiweka wapi Zanzibar yetu na kwa sasa Zanzibar ipo vizuri ikilinganishwa zamani tulikuwa hatuzikani hatusalimiani ,"amesema


Amesema vyama vya siasa vipo pamoja na Rais Mwinyi katika kuhakikisha hali ya utulivu wa kisiasa inaimarika siku hadi siku.


Katibu Mkuu wa chama cha UPDP, Hamad Mohamed Ibrahim amesema  ACT-Wazalendo wanapaswa watambue kuwa si wanzanzibar wote wapo kwenye siasa hivyo dhamira yao hiyo itawatesa watu hao.


Amesema vyama hivyo havitakubali kutokea kwa hali hiyo na kwamba wanaungana na Rais Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wanzanzibar ambapo alitoa ahadi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020.


"Inasikitisha kuona Rais anafanya uteuzi ambapo wenzetu hawajaridhishwa waon wanakataa kitendo hicho ni cha kukebei na kuingilia mamlaka na maamuzi ya Rais,"amesema