Wabunge waibana Serikali uboreshaji elimu maeneo ya pembezoni

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza wakati akijibu swali kwenye kikao cha 36 cha mkutano wa bunge la bajeti leo Jumatano, Mei 29, 2024. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Wabunge wataka Serikali ije mpango maalumu wa kuinua elimu kwenye mikoa iliyo nyuma kielimu. Yajibu ikieleza mipango yake ya kuweka usawa utoaji elimu katika maeneo yote
Dodoma. Wabunge wamehoji kuhusu mikakati ya kuboresha elimu kwenye maeneo ya pembezoni, huku Serikali ikianisha mipango na mikakati inayotekelezwa nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 29,2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mwanaisha Ulenge amehoji ni lini Serikali itakuja na mpango maalumu wa kuinua elimu kwenye mikoa iliyo nyuma kielimu.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema utekelezaji huo unafanyika kutokana na taarifa za tathmini ya ubora wa elimu zinazofanyika ili kubaini changamoto zinazoikabili sekta hiyo nchini.
Aidha, Kipanga amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu katika kuweka mipango ya kuboresha na kuinua ubora wa sekta hiyo nchini.
Serikali pia inaweka sawa utoaji wa elimu na mafunzo katika mikoa yote nchini kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha.
“Serikali imekuwa ikitekeleza mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuboresha na kuinua viwango vya elimu na mafunzo nchini, kwa ujumla ambayo inahusisha kuwekeza katika miundombinu ya sekta hiyo,” amesema.
Amesema miundombinu hiyo ni kama vile ujenzi na ukarabati wa shule na vyuo vya elimu, kutoa mafunzo na rasilimali kwa walimu ili kuboresha uwezo wao wa kufundisha.
Mikakati mingine ni kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia katika elimu pamoja na kuweka sera na mikakati ya kuhakikisha inapatikana kwa uswa kwa wote.
Katika maswali ya nyongeza Mbunge wa Viti Maalumu, Cecil Pareso amesema utekelezaji wa sera mpya umeanza ambayo ni pana na imebeba mambo mengi, hivyo ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kutokana na malengo waliojiwekea kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
Pia amesema suala la kuinua ubora wa elimu ikiwemo maeneo ya pembezoni ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu.
“Ni nini mkakati wa Serikali kutoa motisha kwa walimu waendelee kufundisha ili elimu iwe katika ubora unaotakiwa,”amehoji.
Akijibu maswali hayo Kipanga amesema utekelezaji unakwenda kwa awamu ili kuwezesha kufanya tathmini, kujenga uwezo na kupeleka vifaa.
“Tukiendelea kutekeleza awamu kwa awamu tunaweza kufanya tathmini ya kina kwa kila awamu,”amesema.
Aidha, amesema Serikali imekuwa ikiendelea kutoa motisha kwa walimu katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na stahiki zao na mwaka juzi baada ya sensa ya watu na makazi waliwapatia vishkwambi.
Amesema Serikali itakuwa inafanya hivyo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Naye Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Kikoyo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuwapa posho ya mazingira magumu.
“Serikali ina mpango gani ya kuwapa walimu wanaopangwa kwenye maeneo ya pembezoni posho ya mazingira magumu ambao wanakuwa tayari wamekata tamaa. Lengo kuwatia moyo ili kufundisha watoto wetu,”amesema.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema wanachukua ushauri wa mbunge huyo na watakwenda kufanyia tathimini ili kuona ni namna gani wanaweza kutekeleza.
Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Christina Mzava amesema Chuo cha Ualimu cha Shycom ni kikongwe lakini miundombinu imechakaa na kuhoji Serikali ina mpango gani wa kukikarabati.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema wamefanya ukarabati na wanaendelea kuongeza miundombinu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Amesema si kwa chuo hicho bali na vyuo vingine vya ualimu ambapo wanakarabati, kuongeza miundombinu na kuweka mkongo wa Taifa wa mawasiliano.