Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Mwiba mdogo-3

ILIPOISHIA JANA...

“Huenda ameuliwa baba yake,” mmoja alitoa wazo.

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Ni wazi walishirikiana kumuua baba yake, hivyo analipa kisasi.”

“Maneno yako yanakaribiana na ukweli, tukiwajua watu wao wa karibu tutaujua ukweli.”


Endelea

Wakati huo gari lilikuwa likiingia geti la ofisi za upelelezi makao makuu, Shila baada ya kuwapa majukumu vijana wake kuwajua watu wa karibu wa mchungaji, aliamini watakapojua watu wa karibu wa Mchungaji Samweli itasaidia kuwalinda hao wanne kabla mtoto wa marehemu kuwafikia.

Mkuu wa upelelezi Shila baada ya kuachana na vijana wake alibaki ofisini akitafakari matukio mawili yaliyopishana siku mbili;  la kutekwa kwa mwanamke albino mwenye ujauzito na kifo cha Mchungaji Samweli.

Tukio la kifo cha mchungaji kilimtisha na kukumbuka kazi nzito aliyoifanya kwenye mkasa wa Operesheni Rwanda ambayo ilipoteza watu wengi.

Alijiuliza vipi kama itakuwa kama Operesheni Rwanda angefanya nini ikiwa kikosi kamili alikuwa amekituma kufuatilia kutekwa kwa mwanamke albino.

Bado aliamini vijana wake watakabiliana na muuaji kwa kuamini ile ilikuwa ngoma ya kitoto.

Kikosi kamili kilichoongozwa na mpelelezi machachari Malik na binti mrembo raia wa Rwanda, Queen Bizimana, hakuna haja ya kukizuia na kukiacha kifanye kazi ya kutekwa mwanamke albino.

Wazo la haraka aliamini huenda ni washindani katika huduma za kiroho waliofanya vile ili kupunguza kasi yake. Jina la Mchungaji Samweli liliwatisha kutokana na kila kukicha watu kufurika kwenye kanisa lake.

Siku zote watu hufuata huduma bora, hivyo kama mbabaishaji utajikuta ukibakia na familia yako, huku waumini wako wakiondoka kufuata huduma kwenye makanisa mengine.

Kwa vile muuaji aliahidi kuwaua wengine wanne, wazo la haraka ni kuzungumza na familia yake na wasaidizi wake wa karibu ili kujua washirika wake wa karibu, pia kujua kama Mchungaji alikuwa na uhasama na mtu gani ili waweze kuzima tukio lingine linaloweza kuzuka haraka.

Alipanga majira ya saa moja na nusu usiku afike msibani aweze kuzungumza na familia ya marehemu na watu wake wa karibu. Kwa vile tukio lile lilifanana na tukio la nyuma katika Operesheni Rwanda,  alikwenda kwa tahadhari kwa kuwatanguliza vijana wake eneo la tukio na mwingine walimfuata kwa karibu ili kumlinda kwa chochote kitakachoweza kutokea.

Majira ya saa moja na nusu usiku, mkuu wa upelelezi Juma Shila aliwasili maeneo ya Mbezi Kibanda cha Mkaa na kwenda mpaka kwenye nyumba ya marehemu Mchungaji Samweli iliyokuwa jirani na kanisa lake aweze kuzungumza na familia yake ili kujua mengi juu ya marehemu, pia aweze kupata mwanga wa kuanzia, hasa kutokana na kutishwa na taarifa ya kuuawa watu wengine wanne.

Aliamini akimpata mtu wa karibu atajua nani mtu wa karibu wa Mchungaji ambaye yupo kwenye hatari ya kuuawa kutokana na taarifa ya muuaji kuwa kuna watu wengine wanne wa kuuawa baada ya kifo cha mchungaji Samweli.

Aliamini kuwafahamu watu wake wa karibu ingesaidia kuwalinda na kutengeneza mtego wa kumkamata muuaji. Alisimamisha gari mbali kidogo na sehemu ya msiba ambako kulikuwa na maturubai na watu wengi waliokuwepo pale msibani.

Alitembea taratibu, viongozi wa kanisa walipomuona walisimama na kumkaribisha kwa heshima zote.

“Karibu mheshimiwa.”

“Asante, poleni kwa msiba.”

“Asante.”

Mkuu Shila aliwaeleza sababu ya yeye kuwepo pale muda ule.

“Nina imani mnajua tukio la kifo cha Mchungaji si cha amri ya Mungu, hivyo tangu tulipopata taarifa hatujatulia. Kuna vitu ninahitaji kuvijua kutoka kwenu ili kutuwezesha kupata mwanga kumjua muuaji na kwa nini amefanya unyama ule.”

“Sawa mkuu, tupo tayari kukupa msaada wowote unaouhitaji,” alisema msemaji wa familia.

“Nitashukuru, naomba kwanza kuzungumza na mke wa marehemu kisha nanyi nitawahitaji.”

“Sawa mkuu.”

Shila alipelekwa kwa mke wa marehemu, aliingia chumba walichokuwa wamejaa wanawake wengi waliokuwa wakimfariji mfiwa.

Baada ya kuwasalimia wote, aliwageukia na kuwaomba wawapishe ili azungumze na mfiwa, wanawake waliokuwa mle ndani walitoka nje ya kuwaacha wawili.

Shila alimsogelea na kuchuchumaa pembeni yake.

“Pole mama,” alimsemesha kwa sauti ya chini.

“Asante,” alijibu kwa sauti ya mafua ya kilio.

“Mimi ni mkuu wa upelelezi, naitwa Juma Shila, inawezekana mimi nikawa wa kwanza kujua kifo cha mumeo.”

“Una maanisha nini kusema wewe ndiye wa kwanza kujua taarifa ile ikiwa wewe hukuwepo?”

Shila alimweleza alivyopokea simu na kufika kanisani bila mtu yoyote kujua kuwa Mchungaji alikuwa ameuawa ofisini mwake.

“Sasa muuaji amekosewa nini na mume wangu, mtu wa Mungu, mtu wa watu, Mungu atalipa kwa shetani aliyefanya unyama ule.”

“Nipo hapa kutaka msaada wako.”

“Msaada gani utakaorudisha roho ya mume wangu?”

“Si kurudisha roho bali kutusaidia kumjua muuaji wa mumeo na kumchukulia hatua za kisheria.”

“Mi nitamjuaje ikiwa muuaji nasikia alijifunika uso pia sikuwepo eneo la tukio.”

“Ni kweli hukuwepo ila nataka kujua jana au leo kabla ya kuelekea kanisani mlizungumza kitu gani na mumeo ambacho hakikuwa cha kawaida.”

“Kwa kweli siku zote mume wangu alikuwa mtu mwenye maneno matamu kwangu na familia yake, pia alikuwa mtu wa watu, tena hakuchagua kipato, rangi wala dini, wote walikuwa watu wake.”

“Hakuna siku aliyoonyesha kukwazwa na watu.”

“Mmh! Hakuna, siku zote alikuwa mstari wa mbele kusema wacha neno la Mungu lifanye kazi yake.”

“Nani rafiki wa karibu na mumeo?”

“Kwa kweli mume wangu alikuwa rafiki wa kila mtu.”

“Hakuna aliye na marafiki watupu, lazima kutakuwa na maadui wasiopenda huduma yake, pia kuna rafiki, ndugu ambaye hawezi kupitisha siku bila kuwasiliana nao?”

“Rafiki ndugu ni mchungaji msaidizi ambaye wamekuwa pamoja.”

“Ooh! Sawa, nashukuru kwa ushirikiano wako, nitakapokwama nitakurudia.”

“Sawa, nakutakia kazi njema ili muuaji ajulikane.”

“Hakuna tatizo.”

Shila aliachana na mke wa marehemu na kuwataka radhi wafiwa kwa usumbufu wa kuwatoa nje ili warudi ndani. Alikwenda kuonana na rafiki wa marehemu ambaye alikubali kutoa ushirikiano.

“Unaitwa nani?”

“Naitwa Mchungaji Lusajo.”

“Unamfahamu vipi marehemu?”

“Naweza kusema marehemu hakuwa rafiki, bali ndugu, nimekuwa naye tangu tukiwa vijana wadogo, tumesoma shule moja ila yeye alinizidi darasa moja. Alipofika kidato cha nne aliondoka Mbeya sikujua amekwenda wapi, baada ya muda nilipata taarifa yupo Mirerani kwenye machimbo kama fundi wa mitambo.

“Alipokuwa akija likizo aliniletea vitu vingi, kipindi hicho mimi nilikuwa mtumishi katika kanisa moja dogo pale Mbeya. Hata yeye naye alipenda kazi za kiroho, hata tulipokuwa shule alipenda kutoa mahubiri, mpaka anaondoka shule tulikuwa tunamwita Mchungaji Samweli.

“Miaka ilikatika bila kuwasiliana, kwani hata namba zake za simu zikawa hazipatikani, siku moja nilipata simu ya Samweli na kunitaka nije Dar es Salaam mara moja. Kwa vile nilikuwa tayari nimeanzisha familia nilimweleza siwezi kuondoka bila kujipanga.

“Lakini alinisisitizia kila kitu amekipanga, alinitumia pesa za nauli na za kuiachia familia yangu.

“Wakati huo nilikuwa sijui nakuja kufanya kazi gani, nilipofika ndipo nilipokuta surprise ya kanisa hili. Lakini wakati nafika lilikuwa halijakamilika, hivyo tulishirikiana kulitangaza neno la Mungu na kuweza kulifikisha hapa lilipo.”

“Alikueleza ilikuwaje akaachana na kazi ya machimboni na kujikita kwenye huduma za kiroho?”

“Mmh! Huwezi amini sikuwahi kumuuliza zaidi ya kumshukuru Mungu kuwa ndoto yangu ya kulitangaza neno lake kwa mapana ilitimia.”

“Kanisa kubwa kama hili lazima kuna watu wamemsaidia kulifikisha hapa, unaweza kuniambia nani mshirika wake?”

“Kanisa lile ni lake wala halina mshirika, kila kitu alimiliki yeye.”

“Unajua kanisa mpaka kufikia hapa kumetumika kiasi kikubwa cha pesa, unataka kuniambia mshahara wa ufundi mitambo unaweza kumuwezesha kufanya haya?”

“Kwa kweli siwezi kudanganya, sikuwahi kuwaza kuuliza chochote juu ya kuanzisha kanisa, niliamini Mungu alitenda ili tumtangaze kwa mataifa.”

“Mmh! Sawa, nina imani wewe ulikuwa mtu wake karibu sana hivyo hakuwahi kukuficha siri zake?”


Itaendelea