Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Anayeunda Mwenge wa Uhuru' huyu hapa

Shaban Mwinchumu akiwa na mkewe Asha Abbas, walipofika ofisi za gazeti hili Tabata Relini, Barabara ya Mandela Dar es Salaam wiki iliyopita na kutoa malalamiko yake.  Picha ndogo ni Mwenge wa Uhuru unavyoonekana baada ya kuwashwa. Picha na Venance Nestory.

Muktasari:

Licha ya kuteketeza mamilioni unapokimbizwa yeye analipwa sh250,000, sasa ni mlemavu.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zina historia kubwa katika Taifa letu tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipozianzisha Desemba 9, 1961 akisema;

... tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”

Mwenge huo uliwekwa juu ya Mlima Kilimanjaro na shujaa Luteni Kanali Alexander Nyirenda(marehemu), huku baba wa Taifa akisisitiza kuwa una umuhimu mkubwa katika kuijenga Tanzania yenye umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi wake na kusababisha nchi kuwa miongoni mwa zinanzosifika kwa amani na utulivu duniani kote.

Ndiyo sababu, kila wakati Taifa liawajibika kujikumbusha bila ya kuchoka juu ya dhana na falsafa hiyo kupitia maneno ya busara, hekima, uzalendo na upendo yaliyotamkwa na Mwalimu Nyerere kabla na baada ya Uhuru.

Maneno ya Mwalimu yalikuwa na maana kubwa na yanaendelea kuwa na maana hata kwa sasa. Mwenge umekuwa ukikimbizwa nchi nzima ukipita kwenye mitaa, vijiji, wilaya na mikoa na umeendelea kuwakumbusha Watanzania wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo huku ukitumika kuzindua miradi mbalimbali kila mwaka kwenye maeneo unakopita.

 Hata hivyo licha ya heshima unaopata mwenge huo, huku ukichangiwa mamilioni ya fedha kwa ajili ya mafuta yake unapokimbizwa, mamilioni mengine ya Serikali yakitumika kwa posho za wakimbiza mwenge kuzunguka nchi nzima huku ukiacha maswali yanayokosa majibu.

Je, umewahi kujiuliza mwenge huo unatengezwa wapi na nani?

Je, unatengezwa kwa thamani gani? Anayetengeneza analipwa kiasi gani cha fedha licha ya thamani kubwa iliyopo?

 

Mtengenezaji alonga

 Gazeti hili limefanikiwa kumnasa fundi anayetengeneza Mwenge huo, akifanya kazi hiyo kwa miaka 25 sasa baada ya kuirithi kutoka kwa mwasisi aliyeifanya tangu mwaka 1961.

Shaban Mwinchumu (46) mkazi wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam anasema ndiye fundi   anayetengeneza Mwenge wa Uhuru tangu mwaka 1990 hadi sasa.

Anasema alianza kazi hiyo  akiwa mwajiriwa na Kampuni ya Recco Engineering company Ltd, iliyopo Chang’ombe, Wilaya ya Temeke, ambayo hufanya kazi za kihandisi.

Anasema baada ya kuajiriwa na kampuni hiyo mwaka 1990, alifundishwa kutengeneza mwenge huo na mfanyakazi mwenzake wakati huo, Athuman Ali kabla ya kufariki mwaka 1993.

“Baada ya mzee Athumani kufariki, jukumu la kutengeza Mwenge wa Uhuru nikaachiwa kwani hapakuwa na mtu mwingine mwenye uwezo huo,” anasema.

Anasema tangu mwaka 1993 amekuwa mkuu wa kazi hiyo, akiwa mwajiriwa wa kampuni hiyo hadi alipoacha kazi mwaka 2008.

Anasema kutokana na shughuli zake za kutumia moto kuyayusha vyuma, jicho lake moja likapoteza uwezo wa kuona na daktari akamshauri apumzike kufanya kazi hiyo.

“Niliueleza utawala wa kampuni, ukanishauri niandike barua ya kuacha kazi na kuahidi wangenilipa, lakini hawakufanya hivyo,” anasema.

Anasema tangu kipindi hicho, amekuwa akiitwa na uongozi wa kampuni hiyo kutengeneza Mwenge kila wanapopewa kazi hiyo kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.

“Serikali inaipa Kampuni ya Recco kazi ya kutengeneza Mwenge, lakini mimi ndiye mtengenezaji kwa sababu ndiye wanayonitegemea hadi sasa na mwaka huu niliutengeneza,” anabainisha.

 

Analipwa kiasi gani?

Anasema amekuwa akilipwa Sh 250,000 kwa kila Mwenge anaotengeneza na wakati mwingine hutakiwa kutengeneza miwili  mpaka mitatu kwa mwaka.

 

Recco wazungumza

 Uongozi wa kampuni hiyo unathibitisha kupewa kazi ya kutengeza Mwenge na Serikali tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere.

Mhasibu wa kampuni hiyo, Akida Sheffa anasema:  “Ni kweli Mwenge wa Uhuru unatengenezwa katika kampuni yetu.”

Hata hivyo, mmoja wa viongozi ambaye alikataa jina lake lisitajwe anasema: “Masuala mengine kuhusu Mwenge wa Uhuru, hatuwezi kukuambia kwa sababu yanahusu Usalama wa Taifa.”

 

Mwenge unavyotengenezwa

Mwinchumu anasema Mwenge hutengenezwa kwa kutumia madini ya chuma, shaba, bati na mti aina ya mpingo au mninga.

 Anasema mti wa mninga au mpingo hutumika kwa ajili ya kuushikilia mwenge wakati wa kuukimbiza.

Anasema tenki la kuhifadhia mafuta ya mwenge, hutengenezwa kwa chuma na huunganishwa na ndimi za utambi kwa ajili ya kuwaka.

 

Uzito wa Mwenge

Mwinchumu anabainisha kuwa Mwenge ukitengenezwa, kabla ya kuwekwa mafuta huwa na uzito wa kilogramu tano.

Anafafanua kuwa kazi ya kuutengeneza Mwenge huo, huchukua wastani wa wiki moja.

“Nikiitwa na Recco nakwenda kwenye karakana yao na kuutengeneza na kulipwa baada ya kufanya kazi hiyo,” anasema.

 

Anajisikiaje unapokimbizwa?

Mwinchumu anasema akiona mwenge unapokimbizwa maeneo mbalimbali ya nchi, hupata faraja na kuona kwamba ametoa mchango mkubwa kwa Taifa.

Lakini anasikitika akiona miradi ya mamilioni ya shilingi inazinduliwa wakati wa mbio za Mwenge huku aliyeutengeneza akishamiri kwa umasikini wa kipato na ajira.

 

 

 

 

Amwandikia barua Rais Kikwete

 Kutokana na ukali wa maisha, licha ya kufanya kazi inayostahili kutambulika kitaifa Mwinchumu, anasema aliamua kuandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete kuomba msaada kwa imani kuwa kwa nafasi aliyonayo ya urais na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) kilichoasisi mwenge huo na haiba yake anaweza kumsaidia.

Katika barua aliyoiandika kwenda kwa Rais Kikwete Oktoba 9, 2008, Mwinchumu anasema  ingawa anafanya kazi ya kitaifa lakini hana ajira ya kudumu, pia hatambuliki kitaifa.

Anasema hajui kama aliyemfundisha kazi hiyo ndiye mbunifu, bali anaamini ni yeye pekee mwenye utaalamu huo na kuiomba Serikali impe ajira ya kazi hiyo badala ya kuipa kampuni.

 

Mwenge umempa ulemavu

Anasema kazi ya kutengeneza Mwenge ndiyo iliyompa ulemavu wa jicho alionao, hivyo anamwomba Rais Kikwete amsaidie kupata kazi hiyo ya kudumu ili aweze kuendesha maisha yake.

“Sina ajira, lakini kazi ninayoifanya ina faida kubwa kwa taifa. Lakini tangu nimeanza sijawahi kupewa tuzo wala cheti cha kutambua mchango wangu kwa taifa, badala yake wanafaidi wakubwa(Kampuni ya Recco),” anasema.

Anasem:, “Nina watoto watano, miongoni mwao ni yatima nilioachiwa na ndugu zangu waliofariki. Wote ninawalea tangu mwaka 1995.”

“Nimekuwa naona watu wanapewa Nishani za Mwenge  na Rais kwa michango waliyotoa katika jamii,  ingawa nishani haiombwi, lakini nadhani nami nastahili kwa kazi ninayofanya,” anasema Mwinchumu.

Anasema kwa sasa anaishi kwa kazi ya kuchomea vyuma, ingawa ni kwa `kujishikiza’ kwenye karakana za mafundi wengine.

“Nina fani ya uchomeaji wa vyuma, lakini sitachagua kazi nitakayopewa,” anasema.