Muda wa dirisha dogo utendewe haki

Monday January 11 2021

Dirisha la usajili wa wachezaji linafungwa ndani ya siku nne zijazo. Tarehe 15 ndio siku ya mwisho ya dirisha dogo la uhamisho ambalo lilifunguliwa Desemba 16, 2020.

Klabu za ligi zinapaswa kuchanga vyema karata katika kutumia muda huu mfupi uliobaki kukamilisha mipango ambayo haijakamilika kwa kuwa muda si rafiki tena.

Mavuno ambayo kila timu imeyapata kuanzia mwanzo wa msimu ni wazi yalishazipa picha klabu husika kutambua nafasi zao katika kampeni za ubingwa wa ligi au katika kuwania kutimiza malengo, iwe ni kubaki kwenye ligi au kumaliza katika nafasi za juu.

Klabu ambazo zilidhamiria kuimarisha vikosi vyao katika dirisha hili na bado hazijakamilisha dili zao, zinapaswa kuchangamka sasa ili kuzikamilisha.

Matokeo ya timu katika raundi 18 za kwanza yameongea kila kitu kuhusu ubora wa vikosi katika mbio za mwaka huu na kila klabu imeshafahamu ubora wake uko katika eneo gani na udhaifu wake uko katika maeneo gani ambayo yakiboreshwa zinaweza kuimarika zaidi.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 44 baada ya mechi 18 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 35 baada ya mechi 15.

Advertisement

Simba ikishinda mechi zake tatu za mkononi itaifikia Yanga kileleni. Azam iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32 baada ya mechi 17.

Katika kuimarisha kikosi kwenye dirisha dogo, Yanga ilimsajili straika Said Ntibazonkiza ambaye mchango wake umeshaonekana haraka.

Nyota huyo licha ya kucheza mechi tatu tu za mashindano tangu asajiliwe Yanga, ameshashinda tuzo ya Shirikisho la Soka (TFF) ya Mchezaji Bora wa Mwezi Desemba baada ya kuhusika katika mabao matano, akifunga mawili na kusaidia mengine matano.

Wakati straika wa Yanga, Michael Sarpong akiomba kuondoka, miamba hiyo ya soka inajaribu kusaka mbadala wake sokoni.

Mabingwa mara tatu mfululizo Simba, katika dirisha dogo wameshamnasa mkata umeme, Taddeo Lwanga kuziba pengo lililoachwa na Gerson Fraga, raia wa Brazil, aliyeomba kuvunja mkataba wake huku akiwa majeruhi.

Azam imemsajili kiungo wa ushambuliaji, Mpiana Mozizi katika dirisha dogo wakidhamiria kufufua matumaini yao ya kupigania ubingwa wao wa pili tangu walipoutwaa kwa mara ya kwanza na ya mwisho msimu wa 2012-2013.

Sajili hizo ni kwa uchache tu zilizofanyika katika dirisha hili dogo.

Klabu nyingine ambazo pia zilikuwa na matokeo mchanganyiko katika mechi zao msimu huu ni muhimu kuchanga karata zao haraka kuwahi muda huu mfupi uliobaki kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho Ijumaa hii.

Ni jambo muhimu pia kwa timu kama Mwadui, Mbeya City na Ihefu ambazo zinashikilia nafasi tatu za chini katika msimamo, kusajili ili kujiimarisha na kufufua matumaini yao ya kubaki kwenye ligi.

Msimu huu, timu nne zitashuka daraja na zitapanda mbili katika mkakati wa kuirudisha Ligi Kuu Bara ambayo sasa ina timu 18, iwe na timu 16 kama ilivyokuwa zamani.

Ndiyo maana tunazikumbusha klabu kuonyesha dhamira zao za kufikia malengo tofauti waliyonayo kwenye ligi kwa kuzichangamkia siku chache zilizobaki za dirisha hili la usajili wa wachezaji kuimarisha vikosi vyao.

Lakini katika kulifanikisha hilo, ni vizuri pia klabu kuangalia aina ya wachezaji wa kusajili ili kuleta changamoto kwa waliopo na si bora mchezaji tu kutoka katika taifa jingine.

Advertisement