ANTI BETTIE: Status ya WhatsApp inahatarisha ndoa yangu

Sunday January 24 2021
Anti Bettie pic
By Mwandishi Wetu

Anti naomba ushauri wako niligombana na mume wangu, wakati hatujaanza kuzungumza vizuri nikaweka status WhatsApp , kwa bahati mbaya mume wangu anaamini nilimuwekea yeye ingawa kiuhalisia siku na nia hiyo.

Ninapata shida kujitetea kwa sababu mara nyingi amekuwa akinikataza kufanya hivyo. Sasa kesi ipo kwa wazazi na mimi nimerudi nyumbani anataka tuachane.

Nifanyeje ili anielewe?

Umesikia usemi usemao “Mwanamke mjinga huvunja ndoa yake kwa mikono yake”? kama umeusikia basi unakuhusu moja kwa moja kwa sababu huna adabu.

Kama mumeo alikuwa anakukataza kila siku usiweke hayo mavitu mitandaoni na bado unang’ang’ania unadhani mwisho wake ungekuwa nini kama siyo huo?

Achilia mbali kuweka wakati mmegombana na kuhisi umemuweka yeye, hata mimi naungana naye itakuwa umemuwekea kwa sababu umezoea mambo hayo.

Advertisement

Mwanamke mzima una mumeo unaweka vitu ambavyo ukiacha havina madhara na unavyofanya havina faida zaidi ya kukutia matatani.

Muhimu muombe msamaha mbele ya wazee na uape hutorudia tena mambo hayo, .

Wanandoa wengi, wakiamka hawana uhakika hata kama miguu yao inatembea, lakini wameshafungua WhatsApp.


Ananilazimisha nimuoe, ilihali sina fedha

Sina kazi ndiyo nimemaliza masomo, familia yangu pia haina uwezo, lakini mpenzi wangu ananilazimisha nimuoe katika hali yoyote ile.

Je, hawezi kunisumbua baadaye?

Anaweza asikusumbue, ingawa hakuna mwenye uhakika zaidi ya mwenyewe.

Lakini kama mwanaume hakikisha unajipanga kuitunza familia yako kadri uwezavyo, usikubali kuonewa huruma hata katika vitu ambavyo ni haki yako.

Anataka umuoe kwa sababu vijana wengi wanavumiliwa na wanawake wanapokuwa hawana fedha wakizipata wanawaacha na kuona wanaoona wanawafaa.

Hivyo anakubali kupata shida mtafute wote pamoja ili angalau kuwe na heshima na alinde penzi lake, hivyo ongeza bidii za kutafuta kazi, kubuni vitu vya kufanya.

Ukibwetekwa eti kwa sababu amekupenda mwenyewe ipo siku atakusimanga na mnaweza msiachane kwa sababu anakupenda kwa dhati, lakini maisha yako yakawa ya masimango.

Advertisement