Ardhi ni mama yetu tuitunze, itatulisha
Kila mwanadamu huishi kwa kutegemea ardhi, iwe ni chakula anachokula, maji anayokunywa, au hewa safi anayovuta. Ardhi si tu rasilimali ni mama tunayepaswa kumheshimu, kumlinda na kumtunza.
Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango alisema taarifa mbalimbali za hali ya mazingira nchini zimedhihirisha kuwapo kwa uharibifu wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo inakadiriwa kuwa takribani asilimia 61 ya ardhi nchini iko katika hatari ya kuharibika.
Alisema uharibifu huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu. Kauli mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka 2025 kwa Tanzania ilikuwa inasema “Mazingira yetu na Tanzania ijayo, tuwajibike sasa, dhibiti matumizi ya plastiki”.
Moja ya changamoto kubwa kwa ardhi yetu leo ni uharibifu unaosababishwa na taka ngumu zisizoharibika kwa urahisi, hususan plastiki na chupa za vioo. Plastiki, hasa ile inayotumika kwa matumizi ya kila siku kama mifuko, chupa za maji na vinywaji, pamoja na vifungashio vya bidhaa, hubaki kwenye mazingira kwa zaidi ya miaka 100 bila kuoza.
Taka hizi, zinapokusanywa ovyo au kutupwa kwenye ardhi wazi, husababisha mmomonyoko wa ardhi, kuzuia ukuaji wa mimea, na hata kuharibu maisha ya viumbe vidogo wa ardhini wanaosaidia katika kurutubisha udongo.
Chupa za vioo, hasa zile za vinywaji vikali na pombe ambazo mara nyingi huagizwa kutoka nje, ni miongoni mwa taka hatarishi zaidi. Mara nyingi, chupa hizi hutupwa ovyo baada ya matumizi, hazina mfumo wa kurejelewa kwa kiwango kikubwa, na zinaweza kudumu kwenye mazingira kwa karne kadhaa bila kuoza.
Tafiti zilizofanyika nchini zinaonesha kuwa maeneo ya mijini na ya utalii hukusanya takribani tani 315,000 za taka ngumu kila mwaka, ambapo asilimia 12 hadi 15 ni plastiki na chupa za kioo.
Mbali na kuchafua mandhari ya miji na vijiji, taka hizi zinachangia kuongezeka kwa joto ardhini (soil heating), kuziba mifereji ya maji na kusababisha mafuriko, pamoja na kuchafua vyanzo vya maji ambavyo jamii nyingi hutegemea kwa matumizi ya kila siku. Zaidi ya hayo, vipande vya chupa vilivyovunjika na plastiki huweza kuwa hatari kwa binadamu na wanyama, na mara nyingine kumepelekea vifo vya mifugo wanaokula plastiki wakidhani ni chakula.
Katika kukabiliana na changamoto ya taka ngumu kama plastiki na chupa za vioo, serikali ya Tanzania kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imechukua hatua kadhaa muhimu. Mojawapo ilikuwa kupiga marufuku mifuko ya plastiki nyembamba kuanzia hatua iliyosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa aina moja ya taka ya plastiki ambayo ilikuwa ikitupwa ovyo
Vilevile, mashirika ya kiraia na baadhi ya makampuni binafsi yameanza kuanzisha miradi ya urejelezaji wa plastiki, hasa za vinywaji, lakini bado kiwango cha urejelezaji ni kidogo, ni chini ya asilimia 10 ya taka zote zinazozalishwa kila mwaka.
Kwa upande wa chupa za kioo, changamoto ni kubwa zaidi kwa kuwa hakuna mfumo madhubuti wa ukusanyaji na urekebishaji wa chupa hizi, huku nyingi zikiishia kutupwa kwenye ardhi na maeneo ya wazi.
Ili kuepukana na madhara ya taka ngumu za plastiki hayo ni vyema kuanzisha mfumo wa dhamana ya urejeshaji (Deposit-Return System). Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaweza kuanzisha mfumo wa “deposit” kwa chupa za plastiki na vioo, ambapo mtumiaji atalipia kiasi kidogo cha fedha kinachorejeshwa baada ya kurejesha chupa iliyotumika. Hii imesaidia sana nchi kama Rwanda na Ujerumani kuongeza urejelezaji wa chupa za plastiki na vioo.
Teknolojia za ufuatiliaji wa taka kwa kutumia GPS au Apps za jamii: Kuanzishwe programu jumuishi (apps) zinazosaidia kufuatilia maeneo yenye taka nyingi, kuripoti kwa haraka, na kurahisisha ukusanyaji. Teknolojia hii inaweza kutengenezwa kwa gharama nafuu na kuendeshwa kwa ushirikiano na halmashauri na wanajamii.
Kuweka kodi au ada kwa bidhaa zisizorudishwa (Environmental Tax): Serikali inaweza kuweka kodi ya mazingira kwa bidhaa zote zinazopakiwa kwa plastiki au chupa zisizoharibika, na mapato hayo yakatumika kufadhili miradi ya urejelezaji na elimu ya mazingira..
Kusaini makubaliano na wasambazaji wa vinywaji: Kufanya makubaliano ya lazima kwa makampuni yanayoagiza au kuzalisha vinywaji kufungua vituo vya kukusanya chupa au kutoa motisha kwa wateja wanaozirejesha.
Kwa muktadha wa mwaka huu wa maadhimisho ya Mazingira Duniani, ni wakati sahihi wa kuunganisha juhudi hizi kwa vitendo vyenye kuleta mabadiliko ya kweli, hasa kwa kushirikisha ubunifu wa kizazi kipya na uamuzi wa kisera wa sasa. Ardhi yetu inaweza kupona, iwapo tutawajibika kwa pamoja.
Frank Abel ni mdau wa maendeleo endelevu, anapatikana kwa kupitia +255 753 73 23 55