Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bodaboda wawe na leseni kudhibiti ajali

Kuongezeka ajali za barabarani, hasa zinazohusishwa na madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda, Jeshi la Polisi nchini libuni mbinu mbadala kuwadhibiti, ikiwemo kila dereva kukata leseni ya biashara na kutambulika kisheria.

Imejengeka dhana kuwa kila mwendesha pikipiki ni bodaboda na kila mwenye kuendesha mwendo kasi ni bodaboda na kuiondoshea hadhi sekta hiyo muhimu, hivyo sheria hiyo itaweza kuzuia uvamizi ambapo kwa sasa biashara ya bodaboda inakua kwa kasi maeneo mengi nchini.

Mazingira yalivyo hivi sasa ni vigumu kumtambua mfanyabiashara wa bodaboda na mwendesha pikipiki wa kawaida na hii ni kutokana na kutokuwepo utambulisho, ikiwemo sare na kitambulisho kitakachoaminisha kuwa ni mjasiriamali wa biashara ya bodaboda.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Tiba na Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) Julai mwaka 2024, ilisema inapokea takribani majeruhi wa ajali za barabarani 700 kwa mwezi.

Taasisi hiyo ilibainisha kuwa majeruhi hao ni sawa na asilimia 60 ambayo ni sawa na majeruhi sita kati ya 10 zinazotokana na ajali zinazohusiana na pikipiki, maarufu kama bodaboda.

Matukio mengi ya ajali za barabarani yanatajwa kuwa ni ya madereva wa pikipiki, hivyo ili kuwadhibiti ni vyema kuwa na mbinu mpya itakayoweza kuwa mwarobaini wa ajali kwa kila mfanyabiashara wa bodaboda kuwa na leseni ya biashara mbali na leseni ya udereva.

Pia Jeshi la Polisi liwe msimamizi wa wafanyabiashara hao, pamoja na wa bajaji na kuwa na mikutano angalau mwaka mara mbili, lengo likiwa ni kukumbushana sheria za usalama barabarani na kutambuana.

Licha ya kuwa zipo ofisi za wasimamizi wa sekta hiyo Wilaya na Mkoa kwa baadhi ya maeneo, ila kwa mtazamo wangu ipo haja Jeshi la Polisi kuwa msimamizi mkuu, kwani huenda ikawepo nidhamu kwa madereva wa vyombo hivyo na utii wa sheria bila shuruti.

Ajali za barabarani ni magonjwa yasiyoambukiza yanayoepukika kwa madereva kupatiwa elimu mara kwa mara na kuhakikiwa cheti cha mafunzo ya udereva na leseni yake, vinginevyo upo uwezekano kuongezeka matukio ya ajali hizi.

Siku za hivi karibuni matukio ya ajali za barabarani huripotiwa, ikiwemo vifo na majeruhi na mengi kuhusishwa na pikipiki, kuwepo kwa utaratibu huo kutapunguza matukio.

Machi mwaka 2024, ilielezwa zaidi ya madereva 750 wa bodaboda katika mkoa wa Tanga na Dodoma walipatiwa elimu ya usalama barabarani na matumizi ya alama za barabarani, lengo likiwa ni kupunguza ajali.

Dhamira hiyo ni ya kuungwa mkono na wadau wa maendeleo na kupaswa kuwa endelevu, ila pasipokuwa na mkakati maalumu wa kuwatambua wajasiriamali hao, inaweza kuongeza idadi ya watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza na kuzalisha bodaboda vishoka.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ajali za barabarani zimekuwa zikisababisha vifo takribani watu milioni moja laki tatu kila mwaka na kundi kubwa ni vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 29.

Takwimu hizo zinaonyesha vijana ndio waathirika zaidi na pia ikiwa ndio kundi kubwa la watumiaji wa vyombo hivyo, nashauri uwepo mkakati maalumu wa kuboresha kazi yao kwa kuwatambua na kujuana wao kwa wao.

Pia zipo takwimu za ajali zilizohusishwa na pikipiki kwa mujibu wa mtandao wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA) mwaka 2017, zikionyesha ajali zilikuwa 1,584 na vifo kutajwa 763 kote nchini.

Kwa takwimu hizo na nyinginezo, Jeshi la Polisi lijue kuwa kuongezeka kwa ajali za barabarani ni uendeshaji mbaya wa baadhi ya madereva wa pikipiki na kuwatoza faini pekee haiwezi kuwa mwarobaini wa matukio hayo.

Ili kupunguza au kutokomeza kabisa ajali za barabarani, itungwe sheria kwa wafanyabiashara wa usafirishaji abiria (bodaboda) na kuwadhibiti vishoka ambao hawatambuliki wanaotajwa kuipa sifa mbaya sekta hiyo ambayo imekuwa kimbilio kwa vijana kujiajiri.

Utitiri wa vituo bubu vya bodaboda mitaani, vyote vinatakiwa kutambuliwa na mamlaka, kwani baadhi yake hutajwa kujipenyeza madereva wasio na sifa na pia ndio wanaoongoza kwa uendeshaji mbaya barabarani.

Ni muhimu Serikali kuanzisha chuo maalumu cha wajasiriamali usafirishaji abiria kila mkoa ili kuiwezesha sekta hiyo kuaminika, na kuacha kutoa mwanya kwa madereva vishoka ambao hawana leseni wala mafunzo ya udereva.

Kuwepo kwa vyuo hivyo itaongeza thamani ya kazi hiyo, kila mmoja kuona ni fursa na kuwa kikwazo kwa wavamizi kila mwenye pikipiki kufanya biashara ya bodaboda.