KUTOKA LONDON : Vinywaji baridi vya kuchangamsha hatari kwa afya zetu
Muktasari:
Kila taifa hutengeneza tamu tamu hizo na kuziita majina tofauti. Vinavyojulikana Ulaya ni “Red Bull”, “Boost”, “Bull dog,” , “Pussy”, nk. Kutahadhari, nchi zenye mtazamo wa kimaendeleo kama Sweden, zimepiga marufuku kabisa mauzo kwa watoto. Sweden na Canada, zina sera za hekima sana zinazokataza watoto wadogo chini ya miaka 12 kutumia simu za mkononi. Mbali ya kuathiri tabia, simu hizi zina mionzi (ingawa utafiti wa kutosha haujakamilika) inayoathiri ubongo, macho na ufahamu.
Oktoba 2014, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya ongezeko la vinywaji vya kuchangamsha. Takwimu za WHO zilinguruma, “energy drinks” (kwa kimombo), hutumiwa zaidi na asilimia 68 ya vijana, watoto chini ya miaka 10 asilimia 18, na asilimia 30 ya watu wazima. Onyo lilizingatia madhara ya vinywaji hivi vyenye ladha tamu inayowavutia watoto.
Kila taifa hutengeneza tamu tamu hizo na kuziita majina tofauti. Vinavyojulikana Ulaya ni “Red Bull”, “Boost”, “Bull dog,” , “Pussy”, nk. Kutahadhari, nchi zenye mtazamo wa kimaendeleo kama Sweden, zimepiga marufuku kabisa mauzo kwa watoto. Sweden na Canada, zina sera za hekima sana zinazokataza watoto wadogo chini ya miaka 12 kutumia simu za mkononi. Mbali ya kuathiri tabia, simu hizi zina mionzi (ingawa utafiti wa kutosha haujakamilika) inayoathiri ubongo, macho na ufahamu.
Karibuni imefahamika kuwa macho ya watoto hudhuriwa kwa kutazama kioo cha tarakilishi (kompyuta) au simu za mkononi muda mrefu. Baadhi ya madhara ni kutolala sawasawa na kuumwa kichwa.
Suala la “vinywaji vya kuchangamsha” au “burudani za kuongeza nguvu” , hata hivyo, ndiyo limesimama dede, Majuu. Karibuni nilikaribishwa kupiga ngoma shule moja ya sekondari. Mwalimu mkuu aliitisha kikao kuwatahadharisha vijana. Mwalimu huyo (mwenye mwamko unaotakiwa kwa wakufunzi) alifafanua kuwa vinywaji vya kuchangamsha huwa bei rahisi. Humfanya mtumiaji kuhisi kazinduliwa. Akataja madhara. Mathalan kahawa (“caffeine”) na viungo vya wanyama (kama uume wa fahali) ambavyo “ ni vibaya kwa sehemu zenu za siri.” Ingawa vijana walicheka, ujumbe ulizama na kukita.
Shule ngapi duniani zinaelemisha wanafunzi kiafya?
Ukweli vinywaji hivi vimeingizwa madukani na matajiri wenye viwanda wanaochuma fedha rahisi. Mara nyingi wasiojali wanachotia mdomoni huwa maskini , sisi watu weusi na watoto wadogo. Kwa vipi? Maskini au mtoto anapotafuta chakula au kinywaji huchagua cha bei nafuu. Haangaiki kusoma kilichoandikwa katika kasha, chupa au mkebe uliokihifadhi.
Siku hizi sheria za kimataifa za biashara huvitaka viwanda na wafanya biashara wa vyakula kueleza yaliyomo ndani. Lakini maskini au Mmatumbi ana muda wa kusoma?
Baya zaidi nini?
Kutokana na wengi nchi tajiri kuanza kuamka na kutaka kujua wanachokula, bidhaa mbalimbali mbaya zinamwagwa kama takataka Afrika. Dawa zisizotakiwa zinauziwa Wamatumbi. Vyakula vilivyoharibika vinatumwa Afrika. Siku moja niliufuma mfuko wa Sembe toka Tanzania hapa London. Nikashtuka.
Nadra kuona bidhaa za “Made in Tanzania” nje. Lakini niliposoma nikakutana na neno GM.
Hii ina maana “Genetically modified”... maelezo yanayoimanisha mmea umekuuzwa katika njia isiyo asilia au kawaida ya maumbile.
Vinywaji vya kuchangamsha vimeenea sana Afrika. Matajiri wanaviuza katika mikebe mizuri mizuri na lugha zinazowavutia mamilioni ya makabwela wasiokuwa na muda wa kuzijali afya zao.
Kama hupendi vitabu utataka kweli kusoma mkebe ulioandikwa maneno ya kuinusuru afya yako?
Maneno hufafanua lishe au virutubishi (“nutrition”) kwa uzito wa gramu au miligramu. Huwa nguvu, protini, wanga, sukari na mafuta. Kisha huandikwa maneno ya kitaalamu kama vitamini, kemikali na dawa. Juu yake ufafanuzi zaidi kuhusu maji, sukari, madini (Inositol, Niacin, Nitrites) rangi, vihifadhi kinywaji au chakula (“preservatives”), ladha (flavouring), nk. Kama kampuni ina maadili mazuri hutoa maonyo kama “ usinywe ukiwa mja mzito au unanyonyesha mtoto au kabla ya kulala.”
Maneno muhimu. Lakini je wangapi Afrika wana tabia ya kusoma (ili kujua) tunachokitia mdomoni? Huwa Kiingereza. Kutokana na kukua kwa Kiswanglish, tunapoandikiwa sasa Kiingereza fasaha huwa mtihani. Kiswanglish hakisaidii pale unapotakiwa kuelewa mazito. Kiswanglish ni ubabaishaji maana maneno huandikwa kitaaluma.
Taaluma gani?
Mosi tuzingatie maana ya kinywaji. Vichangamshi huzindua mishipa ya fahamu. Baadhi ya vichangamshi vilivyozoeleka ni sigara, pombe, dawa za kulevya (mfano, bangi) kahawa, chai na soda zenye mapovu mazito kama Cocacola. Sisi wanadamu tumejenga tabia ya kujichangamsha shauri ya uvivu, uchovu, matatizo ya kifikrana kutofanya mazoezi.
Huwa suluhisho la muda mfupi. Hujenga tabia tegemevu (“addiction”). Ukikosa unashindwa kufanya shughuli zako. Kama ni mtoto hasomi.
Anafanya vitu vya hatari mithili 21 . Au kusema uongo.
Kingine ni sukari.
Karibuni sukari imepigiwa kelele sana Uzunguni. Sukari, chumvi, mafuta, nyama na Gluten (iliyoko katika ngano)vikizidi huchangia kifo. Utafiti uliofanywa Uingereza 2009 hadi 2011 uligundua kuwa asilimia 51 ya wagonjwa waliopiga simu dharura hospitali kutokana na sumu ya vinywaji vichangamfu vya sukari walikuwa vijana.
Walipata kiharusi au tatizo la mapigo ya moyo.
Uchunguzi uliofanywa Marekani mwaka 2005 ulikiri kuwa vinywaji hivi hutibua mishipa ya fahamu na kumpa mtumiaji wasiwasi usio na kiini. Hatimaye halali au hatendi kazi sawasawa.
Mwili je, huathirikaje? Huwashwa, meno kuharibika (kutokana na sukari na kahawa), umio (linalopeleka chakula tumboni tokea kooni), harufu ya mdomo na ushuzi unaonuka.
Hayo ni baadhi ya madhara.
Nini hasa kinachoyasababisha?
Vitu vingi vinavyowekwa katika vinywaji hivi ni vizuri vikitumiwa kwa uangalifu. “Niacin” ni kichangamshi kinachosababisha kizunguzungu, kuwashwa washwa, kuharisha na jongo. “Caramel” ni sukari ya rangi (hutumiwa katika bia).
Utafiti uliofanywa na jarida la Afya Marekani mwaka 2005 ulithibitisha “Caramel” huchangia maradhi ya moyo. “Taurine” ni protini katika nyama na mimea. Huwa katika ubongo, moyo, macho na damu. Wanamichezo hutumia “taurine” kuboresha ushindani. Ikizidi huharibu viungo. “Inositol” ni wanga ndani ya wanyama na mimea kama machungwa na matikitiki maji. Ikitumika vizuri ni safi kwa mishipa ya fahamu, ikizidi yaweza kuathiri ufahamu, ugonjwa wa akili.
“Inositol” si nzuri kwa watoto wanaonyonya.
Mwisho ni “preservatives” ambazo ni hifadhi mbalimbali. Wanadamu tumekuwa tukihifadhi vyakula toka zamani. Zamani tulitumia chumvi , kuchoma au kufukia. Leo hifadhi huwekwa dawa zinazodhuru.
-London, 21 Septemba, 2015
-Bpepe: [email protected]
-Tovuti: www.freddymacha.com