Likizo ni fursa wazazi kuwatambua watoto wenu

Kipindi hiki wanafunzi wa shule za msingi ya sekondari wapo katika likizo ya mwisho wa mwaka, pamoja na mambo mengine kujitathmini miezi 12 ya darasani na kujiandaa kwa mwaka mpya wa masomo mwakani.

Hiki ni kipindi muhimu ambacho mzazi au mlezi anapaswa kuhakikisha anatenga muda maalumu wa kukaa na mtoto au watoto wake, ili kujua mambo mbalimbali ikiwemo masomo yao darasani na kuwasoma tabia hasa wanaokaa shule za bweni.

Ni muda wa kuelekezana kuanzia suala la usafi wa ndani hadi mapishi, kwani wako baadhi ya wasichana wenye zaidi ya umri wa miaka 15 hawajui mapishi, hivyo ni kipindi muafaka cha kukaa nao na kuelekezana hayo na mengineo.

Pia wako baadhi ya watoto wa kiume hawana utamaduni wa kufungamana na wazazi wao kusaidia baadhi ya kazi na badala yake muda mwingi hupoteza katika makundi ya vijana wa mitaani na mabanda ya kuangalia filamu na michezo isiyo na faida.

Wako baadhi ya wazazi jawana utaratibu wa kukaa na watoto wao nyumbani kufahamishana kwa baadhi ya mambo ikiwemo nidhamu, upendo na kukinai pamoja na ada ya ufuatiliaji wa maendeleo ya darasani na nyumbani na kuwa moja ya sababu ya watoto kuwa na matokeo mabaya katika mitihani ya mwisho wa mwaka.

Sio vibaya kipindi hiki mtoto kutembelea ndugu na jamaa, ili kuimarisha mshikamano katika familia na kujuana, lakini pia ni muhimu kuhakikisha popote mtoto anapokwenda kufatiliwa nyendo zake pamoja na kufundishwa maadili mazuri.

Ni kipindi kizuri pia kwa mzazi na mlezi kuwajua marafiki za watoto wao kuanzia nyumbani hadi wanapotoka nje. Hii itasaidia kuwafahamu na kumrekebisha baadhi ya mapungufu.

Hakuna ubaya kwa mzazi kufanya upekuzi kwenye begi la madaftari la mtoto wake, kwani wapo wanaomiliki simu na vifaa vingine vya gharama bila mwalimu wala mzazi kujua. Suala la malezi si la mzazi wala la mwalimu pekee, bali ni jukumu la kila mmoja.

Kuna mengi ambayo mzazi au mlezi huhitaji kujua kutoka kwa mtoto wake na kutoona aibu kumuliza, kwani utamaduni huo utamkuza katika maadili mazuri.

Wako baadhi ya watoto pia hujisikia aibu kumueleza mzazi wake jambo linalomkera na badala yake kusema kwa watu wa nje. Hali hii kwa kiasi kikubwa inatokana na kutokuwepo kwa utamaduni wa wazazi kukaa na watoto wao na kuzungumza mambo mbalimbali yakiwemo ya shule na ya kifamilia.

Kama nilivyosema awali hakuna ubaya kwa watoto kufanya ziara ya kutembea kwa ndugu na jamaa kipindi hiki cha likizo, ila muhimu ni kuwachunga watoto huko waendako ikiwemo kuepuka vishawishi na makundi ya watoto watukutu mitaani.
Kipindi hiki, Zanzibari kuna idadi kubwa wanaosafiri ni wanafunzi kwa wanaotoka

Pemba kwenda Unguja na wanaotoka Unguja kwenda Pemba na wasafirishaji abiria kuongeza ratiba za safari kutokana na wingi wa wasafiri.

Wana kauli yao "Desemba twaja" kwa maana ni mwezi kusafiri na kutembeleana ikiwa na pamoja na kujuana na kufahamishana na familia kuzidi kushikamana na kupendana.

Tanga pia kipindi hiki idadi ya wasafiri kwenda sehemu mbalimbali ikiwemo mikoani na wilayani imeongezeka na wengi wao ni wanafunzi wanaokwenda matembezi kwa ndugu na jamaa, jambo ambalo ni zuri ila wasiachwe wakapoteza mud, bali wanatakiwa kubidiishwa kwa mambo yenye faida nyumbani na ya shuleni.

Ni muhimu kwa mzazi au mlezi kumbidiisha mtoto kujisomea kwa masomo ambayo wamesoma shule na si vema kuachwa kuitumia likizo kwa kutembea barabarani na mitaani.

Kwa mtazamo wangu, si kipindi cha watoto kutafutiwa twisheni, bali ni kipindi cha kuwa karibu na wazazi, kwani kuna mengi ya kufahamishana, huku akitumia muda mwingine kujisomea akiwa nyumbani.

Sikatai twisheni, kwani ni moja ya mbinu ya mwanafunzi kufanya vizuri darasani na mitihani ya mwisho, ila maoni yangu masomo hayo yawe nyumbani na si kwingineko kwani muda huo unaweza kutumika vibaya na mtoto ikiwemo michezo na soga mitaani.

Likizo ya mwisho wa mwaka ni siku za mzazi na mtoto kuelekezana kama nilivyosema, kwani yapo mapungufu ambayo hujitokeza hivyo ni kipindi cha mtoto kusahihishwa, ili anaporejea shule awe na nidhamu na tabia nzuri.

Baadhi ya shule huwa zina utaratibu wa kuwapatia kazi za kufanya wakiwa nyumbani na utaratibu huu ni mzuri, kwani unamwezesha mtoto kutokuwa na fikra nyingine zaidi ya masomo na kusahau michezo isiyo na tija kwake.

Salim Mohammed ni mwandishi wa kujitegemea mkoani Tanga. Anapatikana 0655 902929