Madereva mmeisikia nyakua nyakua ya Musilimu?
Swali kwa madereva wa vyombo vya moto hususan magari; je, mmeusikia wito wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu kuhusu watakaobainika kutofuata sheria za barabarani?
Hivi karibuni Musilimu aliagiza askari wake kuwakamata na kuwaweka mahabusu kisha kuwapeleka mahakamani madereva wote watakaobainika kwenda mwendo hatarishi.
Kamanda huyo aliwataka askari kuacha kuwaandikia faini madereva, badala yake wakamatwe na wakitoka tu mahakamani wafungiwe leseni zao sambamba na kuwaondolea sifa ya kuwa madereva wa daraja C.
Kamanda Musilimu hakuishia hapo, akasema faini wanazopigwa madereva wana uwezo wa kulizipa na kwamba baada ya hapo wataendelea kuwachezea askari kwa kuwa wana uwezo.
Ndio maana akaagiza wakamatwe, huku akitumia kaulimbiu ya ‘nyakuanyakua’ akimaanisha askari wake wawakamate wavunja sheria za barabani.
Wito wangu kwa madereva wa magari ni kuwa msiipuuzie kauli hiyo, bali muichukulie kwa uzito mkubwa katika kuhakikisha sheria za usalama wa barabarani zinafuatwa ili kuepusha ajali, nyingi zikisababishwa na uzembe wa madereva.
Dereva ukiambiwa sehemu hii unatakiwa kuendesha kwa mwendokasi wa spidi 50 fanya hivyo kuliko kuzidisha, maana eneo husika linaweza kuwa ni hatari kwako, watu uliowabeba na wanaotumia barabara wakiwamo watembea kwa miguu.
Kama kweli dereva unaipenda kazi yako kauli ya Kamanda Musilimu hautaipuuzia, bali utaichukulia kwa uzito wa hali ya juu kwa sababu kufuata sheria si jambo gumu hasa kwa maeneo unayotakiwa kufanya hivyo.
Itakumbukwa kuwa Mei 21, maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), walifariki dunia baada ya gari la Serikali aina ya Toyota Land Cruser waliokuwa wakisafiria kupata ajali eneo la Msoga mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna, chanzo cha ajali hiyo kilitajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa gari aliyejaribu kuhama upande wake wakati akiyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kwenda kuligonga lori aina ya Scania.
Ifike wakati madereva mheshimu sheria za usalama barabarani, ili kuepusha ajali zinazosababishwa na uzembe na hilo linawezekana ikiwa tu mtakuwa na nia ya dhati ya kuhakikisha ajali zinapungua.
Hadi Kamanda Musilimu amefikia hatua ya kutaka mkamatwe na kuwekwa mahabusu kisha kupelekwa mahakamani sambamba na kufungiwa leseni zenu, ameona mnabweteka pale mnapopigwa faini na kuzilipa huku mkiendelea na makosa yaleyale yanayosababisha ajali.
Mfano wewe dereva unayelipwa posho ya Sh50,000 kwa siku, ukikamatwa na kuwekwa rumande kisha ukapelekwa mahakamani na kufungiwa leseni yako, utakuwa katika hali gani na ukizingatia kuna kundi la watu wanaokutegemea?
Madereva lazima mzingatie kauli hii katika kuhakikisha mnazuia ajali sambamba na kuokoa vibarua na magari yenu vinavyowasaidia kuendesha maisha na hatimaye kujikwamua na umaskini.
Siyo kwamba madereva wote hawafuati sheria, lakini wale wachache wanafanya wenzao waonekane watu wa ovyo, kutokana na uzembe wanaoufanya mara kwa mara, jambo linalogharimu maisha ya Watanzania.
Ipo kasumba ya Watanzania wengi kupuuza sheria na amri halali za Serikali, hii ndiyo inayoligharimu Taifa na ni wakati sasa wa kuachana na kasumba hiyo ili kujenga maisha na uchumi wa Taifa letu.