Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tujikumbushe nadharia za Uongozi na Utawala Bora

Muktasari:

  • Zipo nadharia mbalimbali za uongozi duniani. Sina nia ya kuzirudia hapa, bali safari hii ninataka nigusie nadharia mbili tatu hivi ambazo kama zikitumika kwa umakini na usahihi zinaweza kuifaa nchi kama yetu na nyingi nyinginezo za Kiafrika na kuwapunguzia Waafrika dhiki, kudharauliwa, kubaguliwa na kunyonywa na mataifa mengine duniani.

PENGINE uongozi na utawala ni eneo ambalo limefanyiwa utafiti mwingi kuliko eneo lingine lolote la menejimenti na utawala katika historia ya mwanadamu. Pamoja na kazi yote hiyo uongozi na utawala hadi wa leo ni eneo lenye matatizo mengi zaidi kuliko eneo jengine la menejimenti duniani.

Ulaya na Marekani Kaskazini ambazo ndizo zinazoongoza katika uzalishaji wa nadharia za menejimenti duniani hivi leo zina matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii. Wanafunzi wa mabara ya Asia na Marekani Kusini wanaonekana hivi leo, kufanya vizuri kuliko walimu wao.

Kuna nadharia lukuki katika eneo hili. Wengi hatuzijui na hatujawahi kuzisoma. Mimi kama mwalimu na mwanafunzi wa utawala na menejimenti kwa taasisi na watu, siku zote hujikuta nina mapya ya kujifunza, sembuse asiyesomea fani hii? Taifa lenye wananchi na viongozi ambao ni wavivu kusoma na kujifunza mapya siyo taifa linaloweza kuendelea hata likipatiwa misaada kiasi gani.

Zipo nadharia mbalimbali za uongozi duniani. Sina nia ya kuzirudia hapa, bali safari hii ninataka nigusie nadharia mbili tatu hivi ambazo kama zikitumika kwa umakini na usahihi zinaweza kuifaa nchi kama yetu na nyingi nyinginezo za Kiafrika na kuwapunguzia Waafrika dhiki, kudharauliwa, kubaguliwa na kunyonywa na mataifa mengine duniani.

Katika kuziangalia nchi nyingi za Asia na Marekani ya Kusini ambazo ama zimo kwenye kundi la BRICs au lile la CIVETs, nimegundua mambo kadhaa. Zote zimetafsiri elimu ya menejimenti na uongozi katika lugha zao mama na kisha kuendeleza pale wengine walipoishia. Fedha wanazotumia katika masuala ya utafiti, uvumbuzi na ugunduzi na sayansi na teknolojia kwa jumla zimeongezeka sana ukifananisha na huko nyuma; wanapeleka zaidi siyo watoto wa sekondari bali wa kiwango cha Chuo Kikuu kwenda kusomea fani maalumu huko nje na siyo kiholela holela tu. Udadisi, uchu wa mafanikio toka udogoni, uzuzi na ujasiriamali ni vitu vinavyopewa aula wa hali ya juu kabisa ikiwa ni pamoja na Benki Kuu za nchi na Hazina kusaidia uanzishaji wa miradi yenye kulipa na kuendeleza nchi na watu wake. Hili hufanyika ikitambulika vyema kwamba nchi itajengwa na wazawa na kamwe haiwezi kujengwa na wageni au watu wa kuja.

Nadharia hizo ni pamoja ya Peter Drucker (gwiji wa menejimenti na uongozi na Mmarekani mwenye asili ya Kijerumani); ile ninayoita ya wahamasishaji mafanikio wa kiimani; ile ya Mintzberg na wenzake inayoshadidia majukumu ya kiuongozi na hatimaye ya Etsuko Okazaki inayoonyesha umuhimu wa ubia kati ya watawala na watawaliwa.

Drucker anasema utamjua kiongozi mzuri si tu kwa kujaribu, kuthubutu na kuweza yeye mwenyewe bali pia kwa kushindanisha watu, kuchochea utundu wa kifikra na kimaendeleo na kwa kuwafanya watu waweze wao wenyewe kufanya chochote kile wakitakacho bila kuitegemea serikali wala nani !

Sifa za kiongozi bora kwake huenda kwa mtu ambaye si dhaifu wala mwoga. Aliyeko madarakani kutokana na uwezo; anayejua kuutumia muda wake vyema kufanikisha malengo mbele yake; anayejua yeye anatakiwa awe anachangia nini ili taasisi yake ishinde au ifanikiwe.Asichagua watu kwa kuwapenda bali kutokana na uwezo wao wa kufanya kazi; anayeweka vipaumbele katika mambo yake na mwisho lakini siyo dogo. Anayefanya uamuzi kwa wakati, uamuzi unayookoa roho za watu na kupunguza gharama na hasara kwa taasisi au nchi husika. Mcheleweshaji uamuzi siyo tu mwizi wa maendeleo ya taasisi au nchi bali pia ni mwizi wa maisha ya wale anaowaongoza.

Inaendelea Wiki ijayo

 

Viongozi wa imani wanaowachochea waumini wao kuamka na kukataa kugandamizwa na umaskini wao wamezigawa sifa za uongozi bora katika ngazi tano. Kwanza, ni mtu kushika nafasi anayoimudu na kuidhibiti na siyo asiyoiweza. Pili, kukubalika na wafuasi au watu walio chini yake.Tatu, ufanikishaji wa utekelezaji wa majukumu mbele yake. Nne, kuendeleza watu na hatimaye tano, kufika anapotaka na kuwafikisha watu pale alikowaahidi.

Ninaamini, pamoja na ufupi wa maelezo hayo hapo juu, dhana nzima iko wazi kwa mtu anayefikiri na kutafakari kwa kina na kwa uhakika.

Kwa mujibu wa Mintzberg, uongozi unasemakana kuwa na majukumu kadhaa. Majukumu hayo ni yale ya uongozi, mawasiliano na uamuzi. Katika uongozi, kiongozi mzuri huonekana kwa kuwa mtu anayeonyesha mfano na njia kwa wale anaowangoza ili watatue matatizo au kutumia fursa zilizopo mbele yao ili kuendelea; kuwa kiungo kinachofanya kazi kwa umakini kati ya watu wa ndani na nje na tatu, kuwa ni mwakilishi mzuri katika mambo ya kijamii kwa niaba ya wale anaowaongoza.

Katika majukumu ya kimawasiliano, kiongozi mzuri ni yule ambaye hachoropokwi na habari yoyote (huipata kwa udi na uvumba) na siyo mtu anayedanganyika kirahisi na walio chini yake. Hali kadhalika yeye ndiye mgawaji na msambazaji wa habari zote kwa namna inayoongeza ufanifu na ufanisi wa kazi zake na za wengine na tatu, kwa kawaida huwa msemaji wa kutegemewa wa taasisi anayoongoza.

Katika uamuzi, kiongozi mzuri huonekana kwa kufanya uamuzi kwa wakati, uamuzi unayoweza kuokoa roho za watu au gharama mbalimbali na kuiepusha taasisi au nchi na balaa mbalimbali. Kadhalika huzigawa rasilimali za taasisi au nchi kwa namna ambayo walio wengi ndiyo wanaonufaika zaidi na siyo watu wachache wanaojichagua na kujiweka mbelembele. Kadhalika ndiye mpatanishi mkuu kati ya watu wa ndani na nje katika ugomvi au migogoro mbalimbali na mwisho huwa mtu ambaye siku zote anatatua au kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya watu na siye anayemwaga petroli kwenye moto.

Nadharia za Etsuko Okazaki (Mjapani toka Chuo Kikuu cha Kobe) zikiangaliwa kwa undani itamjulisha mtu kuwa na uwezekano wa kuwepo na aina kama nane za uongozi ambazo ni: 8. ujanja, kuzaini na kudanganya; 7. Kuhonga na kuganga njaa: 6. kutaarifu, kujitangaza na kujisifu sana; 5.Kushauriana, kusaidiana, kuelimishana na kuendelezana; 4. Kutafadhalisha na kuelewana kabla ya kufanya kitu; 3. Ubia au ushirikiano; 2. Kukaimu madaraka/madaraka mikoani au vijijini au mitaani; na ngazi ya juu kabisa kufikiwa kiuongozi ni ile ya kukubali mamlaka ya watu au raia, kiasi hata rais na mawaziri wake wote wakawa chini ya sheria na katiba.

Tatu za mwanzo ndizo zenye hadhi ya chini kabisa. Na kwa bahati mbaya sana, hapo ndipo ambapo leo Tanzania na uongozi wake ilipo hivi leo. Ni kichekesho basi ikiwa tutakuwa tunajiuliza kwa nini hatuendelei kwani ukweli ndiyo huu au nasema uongo? Uendeshaji wetu mbovu wa kiuchumi, kisiasa, ajali za kila siku, uongo, kumkataa kadhi leo na kumruhusu kesho bila maelezo.Pia migomo ya madaktari na walimu, kukwama pembejeo na kukosa masoko kwa wakulima wetu. Vilevile unafiki na machozi ya mamba katika siasa na uongozi yote ni vidonda vya ugonjwa mkuu wa kuwa na uongozi dhaifu na kukosa uongozi bora. Turudi darasani kujipiga msasa jinsi ya kuongoza nchi na watu wetu kwa ufanifu na ufanisi zaidi.

Nihitimishe kwa kumnukuu Kristin Zhivago ambaye amejaribu kujumuisha sifa 10 ambazo kiongozi bora au mzuri kwa kawaida huwa hazikosi. Sifa hizo ni pamoja na mnyenyekevu kiukweli na siyo kinafiki; hamhukumu mtu kirahisi; gwiji wa kukubali kukosea, kusahihisha na kutafutia matatizo ya watu au wafanyakazi wake ufumbuzi.Hakubali kusifiwa kirahisi, haridhiki na alipofika na anataka kuwa bora zaidi kila kukicha; mwingi wa iktisadi na mwoga wa matumizi makubwa na matanuzi yasiyo na maana. Anawekeza kwa watu siyo kwa vitu tu; anawasiliana na wote walio chini yake mara kwa mara, kwa kifupi lakini kwa ufasaha na uhakika wa jambo.Anajua anakotaka kuipeleka nchi au taasisi yake; anajua kulea na kuendeleza watu na huwa mchekeshaji mzuri, akipenda kujicheka mwenyewe, kuchekana na kuwacheka wengine kama njia ya kumfunza na kumuendeleza mtu.

Ni matumaini yangu kwamba endapo tutajikumbusha nadharia hizi na kutokubali zibakie vichwani na moyoni tu, bali ziwe zatafsiriwe kwa vitendo. Nchi hii, mikoa yake, wilaya zake, miji yake, vijiji vyake, kata zake, mitaa yake na nyumba zake zote zinaweza kufanikiwa kuwa na uongozi bora, madhubuti, imara na usiotetereka au kuyumbishwa na tamaa za kibinadamu na kiakili ujinga kama ilivyo hivi sasa. Mungu aibariki Tanzania. Mungu awabariki Watanzania !