Malipo kwa simu nayo yaondolewe makato
Hatua ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuzuia gharama za ziada katika malipo kupitia mashine za POS kwenye biashara, ni ya kupongezwa kwa kuwa inahamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali, kuelekea katika kujenga uchumi wenye matumizi kidogo ya fedha taslimu.
Wakati BoT inafuta makato kwa malipo ya kadi, ilieleza lengo ni kuweka msingi wa kuhakikisha malipo ya kadi za benki yanakuwa salama, rahisi na bila gharama za ziada.
Hii ni hatua muhimu ya kujenga imani ya wananchi katika matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Pamoja na mafanikio haya, ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya miamala ya kifedha nchini hufanyika kwa njia ya simu.
Hivyo, hatua hii ya kutumia kadi inapaswa kuendelezwa kwa kuangazia malipo yanayofanywa kwa njia ya simu, ambayo ni maarufu zaidi miongoni mwa Watanzania wengi kama Lipa Namba.
Hadi Septemba 2024 kulikuwa na akaunti hai za miamala ya simu zipatazo milioni 60.8 ambazo zilifanya jumla ya miamala ipatayo milioni 310.8 na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila siku.
Idadi hiyo ya akaunti ni kubwa na inaonyesha Watanzania wengi wanatumia huduma za fedha kwa njia ya simu kuliko nyinginezo, hivyo ni dhahiri kuwa juhudi hizi za kuondoa makato zinapaswa kupanuliwa kufikia sekta hii muhimu.
Zipo jitihada kubwa za watoa huduma kuwa na suluhu ya malipo kwa njia ya simu na hivi sasa maeneo mengi ya huduma kuna lipa namba.
Hata hivyo, watoa huduma hutoza kiasi fulani cha pesa kama makato kwa kila muamala wa malipo na kiwango hicho huongezeka kulingana na ukubwa wa muamala, hivyo njia hii ikiondolewa gharama itakuwa na manufaa makubwa kwa nchi na jamii.
Hii ni kwa sababu makato haya huwafanya watu wengi kupendelea kutumia pesa taslimu badala ya malipo ya kidijitali.
Hali hii si tu inakwamisha juhudi za Serikali za kukuza uchumi wa kidijitali, bali pia inaongeza hatari ya usalama kwa wananchi wanaotembea na fedha taslimu.
Kwa kuzingatia umuhimu wa huduma za simu, ni wakati muafaka kwa BoT na wadau wengine kuchukua hatua za kuondoa makato kwenye miamala ya malipo kwa simu ili kuendana na azma ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu.
Hatua hii itakuwa na manufaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kutumia huduma za simu kwa malipo ya kila siku na watu watapunguza kutembea na fedha, jambo ambalo litapunguza visa vya wizi na uporaji.
Vilevile, Serikali itaongeza mapato kwa kuwa itaweza kufuatilia kwa urahisi kila muamala, na hivyo kuongeza mapato ya kodi kupitia uwazi wa shughuli za kifedha, lakini pia kuondolewa kwa makato kutaleta neema kwa watu wenye kipato cha chini.
BoT inapaswa kuandaa mpango wa kupunguza au kuondoa kabisa makato ya miamala ya simu, ikishirikiana na watoa huduma za simu na taasisi za kifedha.
Pamoja na hatua hizo, elimu kwa umma kuhusu faida za kutumia mifumo ya kidijitali katika malipo inapaswa kuimarishwa ili kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia hizi.
Kuondoa makato kwenye miamala ya simu kutakuwa ni hatua ya kimkakati ya kufanikisha lengo la kuongeza ujumuishi wa kifedha, hivyo kuleta ustawi kwa kila Mtanzania.