Muhimu kufahamu hili kabla ya kuwekeza
Changamoto ya kuwa na pesa ya ziada ya kuwekeza ni kubwa, nyie mnaoelekeza kuhusu uwekezaji mnapaswa kutambua hilo, aliongea Hafsa huku akishushia maji baridi. Una maana gani? Akauliza Lucy ambaye alikuwa ametulia akimtazama Hafsa usoni.
Kila siku mnatushauri kuhusu uwekezaji lakini hamuonyeshi maeneo sahihi ya kufanya uwekezaji husika. Nimefuata kila ushauri ninaopewa kuhusu uwekezaji lakini hakuna uliofanya kazi, Hafsa aliongea kwa hisia. Baada ya ukimya, Lucy akamuuliza, umewekeza katika maeneo gani?
Nimewekeza katika hisa za kampuni fulani lakini hakuna kitu cha maana ninachopata. Gawio ninalolipata ni afadhali pesa yangu ningeitumia iishe tu nijue moja, akalalamika Hafsa.
Unafikiri ni eneo gani sahihi kwa mimi kuwekeza? Akauliza Hafsa. Hakuna uwekezaji sahihi na usio sahihi, kila uwekezaji ni sahihi, akajibu Lucy kwa mkato. Kama kila uwekezaji ni sahihi mbona ninaona kabisa huu uwekezaji katika hisa sio sahihi kabisa? Akauliza Hafsa kwa mshangao.
Changamoto ya uwekezaji huja kwa kuwa watu hawajui malengo ya uwekezaji. Watu wengi wanawekeza kwanza na kisha kusubiri uwekezaji ule utimize malengo yao. Hapo ndipo lilipo tatizo, aliongea Lucy huku akimtazama Hafsa. Naona unanichanganya, unataka kumaanisha nini? Akauliza Hafsa.
Malengo ya uwekezaji yanapaswa kutangulia kabla ya kufikiria aina ya uwekezaji. Watu wengi wanatangulia kuwekeza kabla hawajaainisha malengo ya uwekezaji huo, anafafanua Hafsa. Unataka kuniambia kuwa nilipaswa kuwa na malengo kabla sijachagua hisa za kampuni ile? Anauliza Hafsa kwa mshangao.
Ndiyo. Malengo ndiyo yanayoamua aina ya uwekezaji. Inawezekana uliwekeza katika hisa lakini malengo yako yalitaka uwekeze katika uwekezaji wa pamoja. Anafafanua Lucy kwa ufasaha.
Ukiwa na pesa ambayo unahitaji kufanyia shughuli fulani baada ya mwaka mmoja, unatakiwa kuwekeza kwenye uwekezaji wa muda mfupi. Hata kama kampuni husika itakuwa inatengeneza faida kubwa, hisa hazitaendana na malengo yako.
Nikiwa nahitaji pesa kwa muda mfupi niwekeze wapi? Akauliza Hafsa. Unaweza kununua vipande kutoka UTT. Huo ndio uwekezaji gani? Anauliza Hafsa. Huu ni uwekezaji wa pamoja ambao unafanywa kwa kukusanya mitaji midogo midogo kutoka kwa watu binafsi, makampuni na mashirika na kuwekezwa sehemu mbalimbali. Mfuko huu una mifuko tofauti ambayo inakidhi malengo ya uwekezaji wa muda mfupi na mrefu.
Vipi kuhusu hatari za kupoteza mtaji? Anauliza Hafsa. Mtaji hauwezi kupotea kwa maana ni taasisi ya serikali. Unaweza kujipatia kitabu kitakachoweza kukueleza kwa ufasaha kuhusu uwekezaji huu, alimaliza Lucy.