Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muziki una faida kuzidi dansi na starehe

Muktasari:

Karibuni tumeona maafa yanayoendelea Bahari ya Mediterranean. Juma lililopita Waafrika wawili walidondoka toka ndege zilizoanzia Afrika Kusini. Mmoja alifariki juu ya ghorofa karibu na uwanja maarufu wa ndege wa Heathrow, magharibi ya London.

Hamu ya baadhi ya Waafrika kukimbilia Uzunguni imechemka tena.

Karibuni tumeona maafa yanayoendelea Bahari ya Mediterranean. Juma lililopita Waafrika wawili walidondoka toka ndege zilizoanzia Afrika Kusini. Mmoja alifariki juu ya ghorofa karibu na uwanja maarufu wa ndege wa Heathrow, magharibi ya London. Mwingine yuko mahututi hospitali. Mwaka 2012, kijana wa Angola alianguka alipojificha ndani ya ndege pia iliyochapukia Afrika Kusini.

Maisha ya Uzunguni ni mazuri kwa maendeleo ya elimu, kazi, huduma za afya na familia. Pia haki, kisheria. Ukidhulumiwa huna haja ya kuhonga. Maandamano yanaruhusiwa ili mradi huvunji sheria.

Jumamosi tarehe 20 Juni, robo milioni ya wakazi London waliandamana kupinga sera ya serikali ya sasa kukata huduma, ajira na matumizi. Hakukuwa na tukio lolote la vitisho au kuwapiga wananchi shauri maandamano yalikuwa ya amani. Baadhi ya wasanii na watu maarufu pia walihudhuria. Mwimbaji maarufu wa muziki wa “Opera” , Charlote Church aliyekuwemo aliishutumu Serikali kwa kubana bajeti inayowaumiza walala hoi.

Muziki wa Opera hutoa kipaumbele kwa sauti ya juu sana ya mwimbaji. Mara nyingi unapotaka kujifunza kuimba vyema zaidi yakubidi utumie ufundi wa matumizi bora ya uvutaji pumzi, tumbo, mapafu na kichwa. Ufundi huu ni msingi rasmi wa muziki wa Opera. Mwimbaji mashuhuri wa Opera, Luciano Pavarotti, aliyefariki mwaka 2007 aliipa fani hii (ya kale) jina kwa kushirikiana na waimbaji wa kisasa.Baadhi yao ni bendi kubwa ya miziki ya Kizungu (Rock) U2, mwimbaji Vanessa Williams (Marekani) na Mercedes Sosa (Argentina) aliyefariki, 2009.

Muziki ni fani adhimu na muhimu sana.

Moja ya sababu kuu zilizonifanya nihame nyumbani ilikuwa kuendeleza vipaji vyangu mbalimbali ukiwamo muziki. Wakati ninaishi Tanzania ukisema wewe mwanamuziki uliitwa “muhuni” na familia mbalimbali hazikupenda hata kidogo watoto waikumbatie fani hii. Sisemi familia yangu ilinikataza. La hasha. Wazazi na baadhi ya ndugu zangu wengi walipiga magitaa na kuimba. Babu alikuwa na Piano nyumbani. Mmoja wa wajomba zangu alinipa zawadi ya gitaa nilipofaulu vizuri kuingia kidato cha tano. Ila miaka niliyoishi Tanzania wanamuziki kijumla walibaguliwa.

Wanamuziki wenye majina mfano Mbaraka Mwinshehe na Patrick Balisidja waliishia tu kurekodi nyimbo zao Redio Tanzania. Hakukuwa na studio mahsusi. Mbaraka Mwinshehe mwenyewe alifariki Kenya (1979) akijaribu kutoa santuri. Ilikuwa sikitiko shauri alikuwa bado “mbichi.” Hakuwa amefikia kilele cha kazi na uwezo wake kama mwenzake, Tabu Ley (Congo DRC), mathalan. Tabu Ley pamoja na kukulia mazingira ya tafrani na fujo bado kaacha albam na kazi nyingi alipofariki akiwa na miaka 76, mwaka juzi. Vipi Mwinshehe aliyezaliwa taifa la amani afariki na mwenzie wa nchi ya kasheshe amzidi kwa kila kitu, ilhali vipaji vyao havikupishana?

Hebu bofya majina yao mtandaoni.

Jina la Tabu Ley hutokea na dondoo zote za Wikipedia ilhali la Mbarakah anazungumzia tu alivyokuwa mwanamuziki na kufariki katika ajali ya gari. Huelezwi mengi. Ndiyo utaona alikuwa mmoja wa wanamuziki wa Morogogoro Jazz iliyoasisiwa na hayati Salum Abdallah aliyefariki pia kwa ajali ya gari mwaka 1965. Salim Abdallah naye kasahaulika. Kitabu kimoja tu kimeandikwa kuhusu maisha yake na mwandishi Juma Mkabarah. Nilipomhoji mjane wake Salum mwaka 1983, mjini Morogoro, alikuwa akiuza vitumbua kujisitiri ilhali marehemu mumewe alikuwa babu kubwa enzi zake.

Utaona basi mazingira niliyokulia yalikera na kusikitikisha. Hatimaye nilipofika Uzunguni nilikumbana na hali inayothamini sana sanaa. Namna muziki unavyothaminiwa nchi zilizoendelea si kama kwetu. Kwetu mtu akisema anapiga muziki tunafikiria yale yale. Bangi, bendi, dansi, baa na burudani kwisha kazi. Uzunguni kuna miziki ya kila aina. Ya bendi kubwa zinazotumbuiza viwanja na majumba makubwa makubwa. Bendi kama Rolling Stones. Santana. U2. Wapo wanamuziki waimbaji wanaojulikana kwa utunzi wa nyimbo zao na wapigaji wa kukodishwa. Wanamuziki kama Beyonce na Rihanna.

Mtindo huu umekuwa katika miaka 15 iliyopita na unatekelezwa na baadhi ya wanamuziki wetu wa kizazi kipya, Afrika Mashariki. Pia, upo muziki unaopigwa kwa kusoma, wa matajiri, muziki wa nyimbo za zamani. Mifano ni kama hiyo opera niliyoitaja juu. Au Jazz. Wenzetu hutenga muziki wa kusikiliza na wa kuchezwa; wa matangazo ya biashara na sinema. Upo muziki unaotumbuizwa na mtu mmoja au kundi la wachache. Miziki hii inaweza kuwa ya ala tupu, vyombo vitupu huwekwa mbele zaidi. Ama muziki na mashairi. Mifano mizuri Wamarekani Bob Dylan aliyetimiza 74 mwaka huu na hayati Gil Scott Heron, mtunzi wa mashairi ya kupigania haki za weusi aliyefariki miaka minne iliyopita akiwa na miaka 62. Dylan hutumia gitaa ilhali Heron (niliyemhoji mara kadhaa) mpiga Piano. Mbali na mashairi au ala, muziki huu waweza kuwa wakuimbwa na yote huitwa Acoustic Music.

Nchini Ufaransa, Ureno na Brazili kitengo hiki cha “Acoustic Music” ni kikubwa na tajiri sana. Mfano mzuri ni msanii msifika, Djavan (mtunzi wa Kibrazili wa nyimbo za mapenzi) ambaye akitumbuiza viwanja vikubwa, maelfu ya wapambe humshangilia yeye peke yake na gitaa baridi (“Galatoni” kwa Kiswahili cha mitaani), tu. Pale watu huja kusikiliza maudhui ya tungo zake kuliko kuzicheza. Utashangaa watu wanavyotulia wakipenda nyimbo hizi za uhusiano ya mapenzi wengi (hasa wanawake) wakibubujikwa machozi.

Mwaka 1980 mtunzi wa aina hii ( kwao Cameroon), hayati, Francis Bebey, aliitembelea Tanzania. Akiwa peke yake na gitaa hilo la baridi, alitumbuiza kadamnasi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Bebey aliimba lugha tatu. Kikwao (Douala), Kifaransa na Kiingereza. Utashangaa wasomi wetu walivyomzomea. Kisa? Muziki wake haukuchezeka. Nikiwa mwanahabari pale niliona aibu sana. Nilipokutana naye miaka michache baadaye, nilimwomba radhi kwa niaba ya wananchi wenzangu. Watanzania hatujazoea aina mbalimbali za muziki. Tunategemea tu muziki uwe wa densi, pombe, basi. Lazima tujifunze kuwa hicho ni kipengele kimoja tu. Bahati nzuri leo vijana wachache wa kizazi kipya wanajitahidi kupanua fani hii. Akina Vitali Maembe na Leo Mkanyia. Swali ni je redio na vyombo vyetu vya habari vinawathamini ipasavyo? Tumalizie mada juma lijalo.

-Tovuti: www.freddymacha.com