Namna ya kusherehekea sikukuu kiuchumi

Mwisho wa mwaka umekaribia na sikukuu ya Noeli ipo karibu. Baada ya wiki moja kuna mwaka mpya. Ni jambo la heri kusherehekea baada ya mwaka wa pilikapilika nyingi.

Mambo ni mengi kwelikweli yanayohitaji fedha. Watu wengine hawakujipanga vizuri kusherehekea sikukuu.

Hata hivyo, wapo waliojipanga kwa mambo mengi. Kwa wengine ni wakati wa kwenda kusherehekea na ndugu, jamaa na marafiki.

Wakati wa likizo hizi za mwisho wa mwaka ni vizuri kufanya yafuatayo yatakyosaidia kuimarisha hali yako ya kifedha, epuka matumizi yasiyo ya lazima na pia kuhakikisha kuwa unaishi kulingana na bajeti yako.

Kuwa na orodha ya vitu unavyovihitaji kwa ajili ya sikukuu, hasa kwa wale ambao wanapanga kusafiri. Mfano inaweza kuwa mavazi, vyakula, vifaa vya nyumbani na kadhalika.

Unaweza kuvinunua kabla au vingine ukavinunua sehemu unayokwenda.

Panga kuwawezesha kiuchumi wale ambao wanaendesha biashara zao sehemu unayoenda kwa ajili ya mapumziko. Inawezekana ni kijijini ulipozaliwa au walipozaliwa wazazi wako.

Kuna vyakula na vifaa vidogovidogo vya nyumbani unaweza kununua maeneo yale ili kuboresha kiuchumi maeneo hayo pia.

Usinunue kila kitu mijini na kwenda kusherehekea navyo vijijini. Inajenga pia uhusiano mzuri na majirani na wanavijiji ukiwa unatumia sehemu ya manunuzi yako pale ulipopanga kwa ajili ya mapumziko.

Weka mpango wa matumizi kwa siku za sikukuu ukijua kuwa matumizi ya lazima kwa ajili ya mwezi Januari yalishafanyika kabla ya kufikiria kwenye kutumia kwa ajili ya shughuli za mapumziko.

Hii ni pamoja na ada ya shule, bima ya afya, kodi ya pango la biashara ama nyumba unayoishi.

Hakuna mtu atakuelewa kuwa ulikuwa kwenye mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka na baadhi ya mahitaji muhimu ya Januari hukuyatimiza.

Kama ulikuwa umepanga bajeti ni vizuri kufuata yale uliyojipangia pekee kwenye matumizi yako ya mwisho wa mwaka.

Ni vizuri pia kuangalia ulipanga nini na ulifanikiwa kwenye nini, iwe ni fedha (mapato na matumizi), ama uwekezaji mwingine ulioufanya.

Usisherehekee kupita kiasi, sherehekea kistaarabu, ukiwa na malengo na pia ukijua kusherehekea kwako hakuumizi wengine, wala kukusababishia matatizo ambayo yatakugharimu.

Kuwa sehemu ya baraka kwa ambao walitamani kusherehekea lakini hawana uwezo. Jali wazee, yatima na wajane.

Jifunze kitu kipya wakati huu wa mapumziko. Mfano kujifunza mapishi, kusoma vitabu, kupiga vifaa vya muziki ama kujadiliana mada mbalimbali na familia au marafiki.

Panga mikakati kwa ajili ya mwaka ujao, mikakati kuhusiana na mambo mbalimbali ya kifamilia na mambo binafsi.

Panga kuwekeza, kuimarisha ama kuanzisha biashara, kupunguza matumizi, kutafuta mbinu mpya za kuvutia wateja, kujiendeleza kimasomo, kusafiri, na kadhalika.

Niwatakie Noeli Njema na mwaka 2024 wenye kheri na baraka