Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nguvu ya wananchi Kikatiba inavyopokwa na mihimili

Licha ya kuwa Katiba ndiyo kila kitu na hakuna aliye juu ya Katiba, mwananchi ndiye mwenye kila kitu, ndiye mwenye nchi na mwenye Katiba, hivyo mwananchi ndio kila kitu, Serikali, Bunge na Mahakama ziko chini ya mwananchi. Vyombo hivi vitatu vilipata wapi mamlaka ya kupora haki za mwananchi?

Leo naendelea na somo la uelimishaji umma kuhusu Katiba, sheria na haki, nikijikita kueleza kati ya Katiba, Serikali, Bunge na Mahakama, nani ni bosi wa ukweli anayepaswa kuheshimiwa kuliko wote?

Kwa mtazamo wa juu juu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye “Bosi Mkubwa” ambaye ndiye mkuu wa mhimili wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, akifuatiwa na wakuu wa mihimili ya Bunge, Spika wa Bunge na mhimili wa Mahakama, Jaji Mkuu ambao wote wako chini ya Katiba na mtu mdogo kabisa katika mfumo huu ni mwananchi.

Serikali, Bunge na Mahakama inaweza kufanya chochote kwa mwananchi na mwananchi huyo akawa hana chochote anaweza kufanya kwa sababu anaonekana kama hana madaraka, mamlaka na hana nguvu za kufanya lolote zaidi ya kutumia nguvu ya umma.

Kutokana na mtazamo huo hasi kumhusu mwananchi, naomba kutoa somo la bosi wa ukweli ni nani? Japo ni kweli Rais ndiye mamlaka kuu ya nchi, akifuatiwa na mihimili ya Serikali, Bunge na Mahakama, wote hawa wanapewa mamlaka na Katiba ya mwaka 1977.

Rais, Serikali, Bunge na Mahakama, sio wenye nchi wala sio wenye Katiba, mwenye nchi na mwenye Katiba, ni mwananchi. Hivyo, kikatiba, mtu mkubwa kuliko wote ni mmiliki, mwenye mali, mmiliki wa Tanzania ni mwananchi, ndiye mwenye nchi na ndiye mwenye Katiba.

Rais, viongozi wa Serikali, Bunge na Mahakama ni waajiriwa wa mwananchi na wanapata mamlaka kutoka kwenye Katiba, mwenye Katiba ni mwananchi, hivyo mamlaka inatoka kwa mwananchi.

Katiba ni nini? Katiba ni kitabu kidogo chenye kurasa 43. Kitabu hiki ndiyo kila kitu kuihusu Tanzania yetu, hakuna yeyote aliye juu ya Katiba.

Katiba ni ya kazi gani? Katiba ndio msingi mkuu na mwongozo wa uendeshaji wa nchi yetu ambapo sheria zote, taratibu zote na kanuni zote za kufanya kila jambo lazima zitokane na Katiba.

Katiba yetu imeweka misingi mikuu minne ambayo ni uhuru, haki, udugu na amani. Misingi hiyo inaweza kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi.

Pia, yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu.

Katiba ni ya nani? Katiba hii imetungwa na Bunge maalumu kwa niaba ya wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo na pia kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia.

Hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977, kitu muhimu kabisa kwa Taifa la Tanzania ni watu, Watanzania, hawa ndio wenye Katiba. Katiba ni mali ya Watanzania. Ni watu hawa Watanzania walioweka misingi mikuu minne ya Katiba yetu, uhuru, haki, udugu na amani. Msingi mkuu wa kwanza wa Katiba yetu ni uhuru, wa pili ni haki. Hivyo vitu viwili vikuu vya Katiba yetu ni uhuru na haki.

Hivyo, viongozi wetu tukisha wachagua kwa mujibu wa Katiba katika uchaguzi huru na wa haki, ulioendeshwa na Tume Huru ya Uchaguzi, tunawaapisha kwa Katiba, waape kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba na kuilinda na kuitetea Katiba.

Ni bahati mbaya sana, baadhi ya viongozi wetu nao wako kwenye kundi lilelile la wasoma Katiba wasioielewa Katiba, wanachaguliwa kwa mujibu wa Katiba wasiyoifahamu na wanaapa kuilinda Katiba wasiyoielewa na mwisho wa siku badala ya kuilinda Katiba, wao ndio kwanza wanakuja kuivunja kwa sababu hawajui watendalo kuwa ni kinyume cha Katiba.

Tuna wanasheria serikalini, tuna wanasheria bungeni na tuna wanasheria mahakamani, ambao ndio walipaswa kuijua Katiba, lakini kwa bahati mbaya sana baadhi ya wanasheria hawa nao pia hawaijui Katiba. Matokeo yake Serikali inatunga sheria batili kinyume cha Katiba, viongozi wa Serikali wanavunja Katiba kwa kufanya uamuzi kinyume cha Katiba, huku mihimili ya Bunge na Mahakama ikiangalia.

Bunge linaletewa miswada batili inayokwenda kinyume cha Katiba na inaitunga kuwa sheria, hivyo Bunge letu linatunga sheria batili na kumpa Rais kuzisaini.

Mahakama nayo ina jukumu la kutafsiri Katiba na sheria ambayo imeshehenezwa wanasheria wabobezi na wabobevu, baadhi yao ni ‘vipofu’, haiwezekani Katiba inavunjwa na Serikali, Bunge linatunga sheria batili kinyume cha Katiba, Mahakama ipo tu inaangalia kwa kusema “Mahakama siyo mlinzi wa matakwa ya watu”.

Kama mwananchi ndiye mtu muhimu kuliko wote, ndiye mwenye Katiba na ndani ya Katiba hiyo aliweka haki fulani za mwananchi, ikiwemo haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi anaowataka na kwa mujibu wa Katiba yetu, Mamlaka inatoka kwa wananchi, namalizia kwa swali, je, Serikali, Bunge na Mahakama zimepata wapi mamlaka ya kupoka haki za wananchi zilizotolewa na Katiba?

Ni haki zipi hizo zilizopokwa na zimepokwapokwaje?

Itaendelea wiki ijayo.