Ni meno ya tembo au pembe za ndovu
Muktasari:
Hapo bila shaka ni sahihi kuziita pembe za ndovu kwa sababu zinaota kichwani Sahihi ni kuziita pembe za ndovu na jamii imezoea kuziita meno kimakosa.
Wako wasomaji ambao wameonyesha nia kuniunga mkono katika baadhi ya masuala mbalimbali ya lugha. Waliochangia kwa wingi wamejikita katika mambo matatu. Moja ni hoja niliyotaka ya kupata ufafanuzi kwa maneno yanayoandikwa tofauti katika magazeti yetu. Maneno haya ni ‘meno ya tembo’ na ‘pembe za ndovu’.
Eneo la pili ni katika upotoshaji wa Kiswahili unaosababishwa na lugha za asili na tatu ni upotoshaji wa Kiswahili katika sarufi.
Katika makala yangu ya wiki iliyopita, niliwaomba wasomaji wangu wachangie mawazo kwa lengo la kuielimisha umma kuhusu upotoshaji maneno ‘meno ya tembo’ na ‘pembe za ndovu’ unaofanywa na waandishi wa habari kwa kisingizio cha mtindo wa uandishi (House Style).
Awali ya yote napenda kuwafahamisha kuwa maneno tembo na ndovu yana maana moja. Kwa hiyo hayatofautiani aslani. Suala la pili ni matumizi ya maneno ‘meno’ na ‘pembe’.
Nawapongeza wote walioniletea maoni yao na ningependa kuyaandika machache kwa muhtasari. Wasomaji walioniletea maoni yao kuhusu meno ya tembo ni saba. Maelezo yao ni haya yafuatayo:
Meno ya tembo
‘Hapa jibu ni meno ya tembo kwa kuwa meno ya tembo yametokeza pembeni mwa mdomo wa tembo.’
‘Kwa usahihi tembo hana pembe bali ni meno. Kwa lugha ya kigeni ni ‘incissors teeth’.
‘Mimi ni mtaalamu wa wanyamapori. Tembo ni mnyama mkubwa kuliko wote nchi kavu na kwa jina jingine anaitwa ni ndovu. Majina yote ya tembo au ndovu ni sahihi. Tembo ana meno mawili ambayo hurefuka kwa ajili ya kujitafutia chakula. Ni kati ya yale meno ya mbele (incissors). Kwa hiyo kinachojitokeza kwa tembo ni meno na siyo pembe kama watu wengi walivyozoea kuita.
Kwa upande wa wale waliopendekeza pembe za ndovu wako wasomaji 18 ambao wametoa maoni yao kama ifuatavyo:
Hapo bila shaka ni sahihi kuziita pembe za ndovu kwa sababu zinaota kichwani
Sahihi ni kuziita pembe za ndovu na jamii imezoea kuziita meno kimakosa.
Majangili wanapoua tembo huchukua pembe na wala si meno. Kwa lugha sahihi ni pembe za ndovu. Jibu sahihi ni pembe za ndovu kwa sababu hazitumiki kutafunia bali kuchimbua ardhi au kupasua vitu vigumu. Meno hukaa kinywani. Hutumika kung’ata au kutafunia, Hivyo hayo si meno ya tembo bali ni pembe za ndovu.
Kitu chochote kinachoota kichwani kwa mnyama ni pembe. Wanaosema ni meno wananishangaza.
Baada ya kupata maoni ya watu saba waliopendekeza kuyaita ni meno ya tembo na 18 wakisema ni pembe za ndovu, hatuna budi kufikia mwafaka. Kwa upande wangu nachukua maelezo na ufafanuzi uliotolewa na wataalaumu wa wanyamapori ambao ni wawili kati wa wasomaji saba, waliopendekeza kuwa yaitwe meno ya tembo na siyo pembe za ndovu kwani hujitokezea kinywani na si kichwani.
Wanasema kuwa tembo ana meno mawili ambayo hurefuka na kwa lugha ya kigeni huitwa ‘upper incissors teeth’.
Suala lingine ambalo ningependa kuwashukuru wasomi wa makala zangu ni kule kuniunga mkono katika kuzingatia sarufi. Msomaji mmoja aliandika kuwa waandishi wa magazeti wanachangia katika kuiharibu lugha ya Kiswahili. Ametoa mifano michache kama ifuatavyo:
“ Kwa waandishi wa michezo mwandishi aliandika, “ Yanga na Simba watakipiga kwenye Uwanja wa Taifa” Alitakiwa aandike. “Yanga na Simba watacheza Uwanja wa Taifa.
AU
“ Timu zitakipiga Uwanja wa Chamazi”.
Vilevile wako waandishi wasiozingatia misingi ya sarufi kwa kuacha herufi ‘H’ kwa baadhi ya maneno au kuongeza ‘H’ pahala ambapo ‘H’ haitakiwi. Kwa mfano:
Mtoto uyu ana hakili sana.
Nakuomba uje ofisini tulijadili jambo ili.
Mambo haya ni vihoja tupu.
Eneo jingine msomaji aliyechangia mawazo ni katika tahajia. Kwa mfano:
Waandishi na pia watangazaji wa runinga walioathiriwa na lugha za asili hushindwa kutofautisha kati ya /l/ na /r/.
Wanatamka:
Tulipokalibia Katolo tulisimama kidogo.
Nitapiga kula wakati ukikaribia
Wasomaji wanashauri kuwa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) wajishughulishe zaidi katika masuala ya ufasaha na usanifi wa lugha kwani wamepewa meno kisheria ya kukuza, kuendeleza na kuratibu lugha ya Kiswahili nchini Tanzania.
0754 861 664.