ONGEA NA AUNT BETTIE: Nimepata mpenzi mpya anataka niache kazi
Swali: Nimepata mpenzi mwekezaji, kwa kweli ananipenda na kunitimizia mahitaji yangu na ya familia. Ila kuna jambo amenishirikisha huu sasa ni mwezi, nashindwa kufanya uamuzi. Nimeajiriwa serikalini kwenye ajira zenye mshahara wa kawaida, hivyo ananiambia niache kazi akaniajiri kwenye moja ya kampuni zake zilizopo mkoani Mtwara.
Amenionyesha hadi mshahara nitakaolipwa, ni mara mbili ya huu wa sasa na marupurupu kibao. Kwa kweli ameahidi kubadili maisha yangu kabisa akishaniajiri. Nimewashirikisha ndugu zangu wote wamenikatisha tamaa, nachanganyikiwa hata sijui nifanyeje. Naomba nishauri.
Jibu: Pole kwa kuchanganyikiwa, ila nami naungana na ndugu zako kuwa usikurupuke kuacha kazi. Huyu anakuajiri kwa sababu ya mapenzi na umesema ni mwekezaji, huna uhakika huo mradi au miradi itadumu kwa muda gani na je, mapenzi yakiisha utaendelea kuwa mfanyakazi wake? Najua utashangaa kusema mapenzi yakiisha. Narudia tena mapenzi huwa yanaisha kabisa, tena mengine huisha vibaya kwa visasi na kununiana, hapo ndiyo itakuwa shida.
Kwa kuwa ameonyesha nia ya kukusaidia uachane na masuala ya kuajiriwa mwambie akufungulie biashara kubwa ambayo utaiendesha ukiwa kazini, ikisimama unaweza kuamua vinginevyo kwa sababu utakuwa na uhakika na biashara ni yako hata mapenzi yakiisha utaendelea kuiendesha.
Zingatia, kumbuka usije kufanya maamuzi yanayoletwa kwako kwa nguvu ya mapenzi, hata kama ni mumeo kuna vitu unapaswa kuviamua kwa umakini sana, kwani hata ndoa huvunjika. Kipimo cha utu ni kazi na kazi ndiyo msingi wa maisha, ukiacha halafu ukaachwa utakuwa mgeni wa nani. Siombei uachwe ila hutokea watu wakaachana.
Swali: Nimejitahidi kila njia lakini mwenza wangu ni kama simridhishi faragha, kiasi imefikia hata mimi naona haniridhishi.Kila nikifikiria ninakosea au tulikosea wapi ninashindwa kupata jibu la moja kwa moja.
Nimefikia mwafaka sitaki kuumiza kichwa sana, nataka nianze upya kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa. Lakini sina mbinu tena kama nilipokuwa kijana, naomba nishauri nifanye nini kuhakikisha mimi na mwenza wangu niliyeishi naye miaka mingi tunaridhishana faraghani.
Jibu: Kabla sijasahau muhimu muwe na mawasiliano mazuri, uelewa na kila mmoja kujali hisia za mwenzake.
Zungumza naye kwa uwazi kuhusu azma yako hii ukilenga kueleza matamanio yako, yaani unachotamani kitokee kuhusu kuridhishana mkiwa faragha.
Mkizungumza usijikite tu kwenye nini unataka, bali pia elewa nini mpenzi wako anataka. Mkijadili kwa pamoja utapata mwanga wapi pa kuanzia, ikiwamo kukubaliana nini kitawafanya mjisikie vizuri mkiwa faraghani na hatimaye kufurahia kupata mlichokikosa muda mrefu.
Inawezekana kuna vitu kila mmoja wenu anavifanya mkiwa faragha havimfurahishi mwingine, lakini mnashindwa kuambiana, hapa ndipo mahali pa kuvisema, pia mnaweza kushirikisha wataalamu wa mahusiano au kujamiiana kwa ujuzi zaidi.
Mjiruhusu kuonyeshana ujuzi wa tendo la ndoa, kama unaona inaweza kuleta shida, mshirikishe kuwa unataka kumuonyesha manjonjo mapya. Hii itamfanya kuwa na hamu na hayo manjonjo na mwili, akili na roho vitakuwa tayari kushiriki vikijua kuna mazuri yanakuja. Hii isiwe ya kupita, bali ya kudumu, kila mara ukijifunza kitu kipya unampa mshawasha wa kukijua na yeye pia halikadhalika.
Si vibaya siku moja moja mkibadilisha mazingira ya kufanyia tendo, simaanishi yawe ya gharama kubwa, ila nasisitiza jitahidini kubadili eneo mnalofanyia mambo yenu kwa kadiri mtakavyojaaliwa.
Muombe maoni siku utakayohisi amefurahia zaidi ujue ulifanya nini hadi kufikia hali hiyo, nawe pia siku ukifurahi zaidi mweleze ashikilie hapo hapo, kwani amekukuna mtima.
Usijipunje, hili suala halitakiwi kusinyaa, linatakiwa kuchanua siku zote, jifunze, tafuta mbinu. Watu wanapojadili masuala hayo hakikisha unakuwa msikilizaji ili ujifunze vitu vipya. Usisahau kumpa nyama ya ulimi, ukimkemea hata ukiwa na mbinu mpya milioni moja, hatofurahia tendo na asipofurahi nawe hutopata unachokitaka kutoka kwake.