Safari za Rais Samia katika tafsiri ya kiuchumi

Septemba 2021, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya Afrika, Rais Samia Suluhu Hassan alihutubia Umoja wa Mataifa, akiwakilisha Tanzania katika mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Sehemu kubwa ya hotuba ile ilikuwa ni kuonyesha utayari na azma ya Serikali yake kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa, akionyesha msimamo wa Tanzania katika kushirikiana na mataifa mengine.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, dhana ya ‘multilateralism’ inahusu hatua mbalimbali za kujenga na kuboresha mahusiano ya biashara kati ya nchi, taasisi za kifedha na biashara, mashirika ya kimataifa na ushiriki katika majukwaa, jumuiya za kiuchumi za kikanda na kimataifa na mengine.

Tangu Rais Samia aingie madarakani, Serikali yake imefanya jitihada kubwa katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia nyenzo za kidiplomasia kwa kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha uwekezaji na mengine.

Akiwa Kenya wakati akitoa hotuba kwenye Jukwaa la Wafanyabiashara kati ya Kenya na Tanzania Mei 2021, Rais Samia aligusia umuhimu wa mazingira mazuri ya biashara kati ya nchi hizi mbili na jukumu la Serikali katika kuboresha, kupitia sheria, mifumo bora ya kodi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Kenya ni mshirika mkubwa kibiashara kuliko yeyote katika ukanda. Ziara yake ya kwanza kama Rais kwenda Kenya ilikuwa mwafaka kwa wakati huo na ilisaidia sana kuponya mvutano wa kibiashara ulioanza kuonekana.

Ziara ya Rais Samia nchini India mwishoni mwa mwaka 2023 ilikuwa ni fursa muhimu ambapo hati 14 za makubaliano zilitiwa saini, zikilenga kuanzisha ushirikiano katika maeneo kadhaa kama viwanda, biashara, afya, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, maji, kilimo na maeneo mengineyo.

Moja kati ya tija kubwa ya ziara hiyo ni makubaliano ya kuanzisha utaratibu mpya kufanya malipo ya biashara baina ya Tanzania na India, ambapo malipo yanafanywa kwa kutumia sarafu za nchi husika, yaani Shilingi ya Tanzania na Rupee ya India, kupitia utaratibu wa akaunti maalumu "Special Rupee Vostro Account".

Itakapokamilika, utaratibu huo inatarajiwa kupunguza shinikizo katika mahitaji ya dola katika kufanya miamala ya biashara, hivyo kusaidia kupunguza changamoto za uhaba wa fedha za kigeni. Mazungumzo na ziara yametumika kama njia ya kidiplomasia katika kufikia malengo hayo ya kiuchumi.

Hivi karibuni diplomasia imetumika vizuri kuvuna matunda mazuri, ziara aliyofanya Rais wa Indonesia, Joko Widodo nchini Tanzania imeibua mafanikio makubwa kihistoria kwa kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania kuongeza umiliki wake katika uendeshaji wa kitalu cha uchimbaji gesi Mnazi Bay.

Kupitia Shirika la Taifa la Petroli (TPDC), Serikali imeweza kuongeza hisa zake kwa asilimia 20 (sasa jumla asilimia 40) katika Kampuni ya Mauril&Prom, ambayo ndiyo inayoendesha kitalu hicho kinachozalisha gesi nyingi zaidi nchini. Kampuni ya Taifa ya Mafuta na Gesi ya Indonesia, PERTAMINA, ni mmoja wa wamiliki wakubwa wa hisa katika kampuni hiyo ya Mauril&Prom.

Katika hafla ya kusaini mauziano hayo, maneno ya shukrani ya Rais Samia kwa Balozi wa Indonesia wakati akitoa hotuba yake, ni ishara ya wazi kuwa ushawishi wa kidiplomasia ulitumika kufanikisha jambo hilo. PERTAMINA ilitumia nguvu yake ndani ya Mauril&Prom kufanikisha mauzo ya hisa kwa TPDC ya Tanzania.

Hotuba ya Rais aliyotoa UN mwaka 2021 imeakisi mwenendo wa Serikali yake katika kipindi cha miaka mitatu iliyofuata, kwa hili, bila kusita naweza kusema Rais Samia ni bingwa wa diplomasia ya uchumi.